Maswahiba wanaotesa England msimu huu

Muktasari:

Urafiki wa Pogba na Lukaku umedaiwa kuwa chanzo kikubwa cha wawili hao kucheza pamoja huko Manchester United baada ya mmoja kumshawishi mwingine

UNAAMBIWA hivi, kwenye Ligi Kuu England maswahiba hawajawahi kukauka na kila msimu wamekuwa wakitamba kwenye mikikimikiki ya ligi hiyo.
Huko nyuma kuliwahi kutokea maswahiba kama Dwight Yorke na Andy Cole. David Beckham na Gary Neville na Frank Lampard na John Terry, waliokuwa maswahiba wakubwa ndani na nje ya uwanja.
Kwa sasa zikiwa zama za mitandao ya kijamii, urafiki wa wachezaji umekuwa bayana kutokana na kupenda kuposti matukio mengi wanayofanya pamoja nje ya uwanja kwenye mitandao hiyo. Hawa hapa maswahiba watano wanaotamba kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

1.Alexandre Lacazette na Aubameyang
Wamekamatia fowadi ya Arsenal kwa sasa hasa baada ya kocha wa Kihispaniola, Unai Emery kutua kwenye kikosi hicho chenye maskani yake Emirates. Tangu alipoungana na Alexandre Lacazette huko Arsenal Januari mwaka huu, Pierre-Emerick Aubameyang amekuwa kwenye urafiki mkubwa na mshambuliaji huyo wa Ufaransa. Mwanzoni kocha Emery alikuwa akimweka benchi mmoja, lakini alipowapanga kwa pamoja na kisha akaona ushirikiano wao ulivyo ndani ya uwanja, basi tangu wakati huo amekuwa akiwapanga pamoja na kumletea matokeo mazuri kwenye mechi. Washambuliaji hao wameanzisha hata staili yao ya kushangilia wanapofunga mabao yao huko kwenye kikosi cha Arsenal huku Aubameyang akisema anamchukulia Auba kama kaka yake na anapenda jinsi wanavyoelewana na kufanya kazi pamoja kwenye kikosi.

2.Romelu Lukaku na Paul Pogba
Kwenye malumbano ya Paul Pogba na kocha wake Jose Mourinho, straika Romelu Lukaku ameamua kukaa kimya na kushindwa kuchagua upande, lakini ukweli wawili hao ni marafiki wakubwa sana na ndio chanzo cha straika huyo wa Kibelgiji kuchagua kuja kuichezea Manchester United badala ya kurudi zake Chelsea. Lukaku anafahamu wazi alishawahi kutibuana na kocha Mourinho walipokuwa pamoja huko Stamford Bridge, lakini ilikuwa rahisi kwake kukubali kwenda kucheza chini yake huko Trafford baada ya fowadi huyo kushawishiwa na Pogba walipokuwa pamoja huko Marekani kwenye mapumziko ya mwisho wa msimu. Pogba amekuwa na urafiki pia na Jesse Lingard, lakini huo si wa karibu sana na ule wa Lukaku, ambapo mara nyingi mitoko yao wamekuwa wakiifanya pamoja. Lukaku wamekuwa marafiki hata kabla ya kukutana katika kikosi cha Man United.

3.Dele Alli na Eric Dier
Wote ni Waingereza na wapo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England. Kitu kizuri zaidi hata klabu wanacheza moja, Tottenham Hotspur. Dele Alli alishawahi kusema kwamba Eric Dier ni mmoja kati ya watu wenye moyo safi aliowahi kukutana nao kwenye maisha yake. Urafiki wao umewafanya wachezaji hao wawili, kulala kwenye chumba kimoja pindi Spurs inapokuwa na mechi za ugenini. Ukiweka hilo kando hata kwenye mitoko yao ya kwenda kufanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali wamekuwa wakifanya pamoja na wamekuwa wakipongezana kwa karibuni sana mmoja wao anapofunga bao au Spurs inaposhinda. Mara nyingi wawili hao wamekuwa pamoja, hata wakati Dier alipotibuana na Danny Rose, Dele alikuwa wa kwanza kukimbilia kugombelezea, huku akiwa upande wa swahiba wake.

4.Richarlison na Yerry Mina
Wachezaji hao wote wamesajiliwa na Everton kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi huko Ulaya. Richarlison ni Mbrazili na Yerry Mina ni Mcolombia, lakini wawili hao ni marafiki wakubwa. Wachezaji hao wawili wamekuwa wakituma picha zao kwenye mitandao ya Instagram na mara kadhaa wamekuwa wakionekana wakiwa pamoja kwenye migahawa na maduka mbalimbali ya huko Liverpool. Mina bado hajaanza kuichezea Everton, lakini atakapokuja kucheza na kama mmoja atafunga bao, basi bila ya shaka wataonekana wakishangilia pamoja.

5.Benjamin Mendy na Bernardo Silva
Wachezaji hao wawili urafiki wao ulianzia Monaco na sasa wanaendeleza baada ya wote kuhamia kwenye kikosi cha Manchester City. Ni marafiki ambao wamekuwa wakiuweka wazi urafiki wao. Aprili mwaka huu, wakati Bernardo Silva alipofunga bao kwenye ushindi wa 5-0 dhidi ya Swansea City, alikimbia moja kwa moja kwenda kushangilia na Mendy, ambaye baadaye aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, kwamba anampenda Silva kuliko hata mpenzi wake. Wengi walilichukulia hilo kama utani, lakini ukweli ni kwamba Mendy na Bernardo Silva ni marafiki wa nguvu.


SUMMARY
Urafiki wa Pogba na Lukaku umedaiwa kuwa chanzo kikubwa cha wawili hao kucheza pamoja huko Manchester United baada ya mmoja kumshawishi mwingine
 
...