Mastraika Simba wana kazi spesho

Saturday November 10 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN

Dar es Salaam.Ligi Kuu Bara imesimama kupisha maandalizi ya timu za Taifa katika mechi za kuwania fainali za Afcon 2019, huku Simba ikiwakosa nyota 12 wakiwamo waliopo Taifa Stars na timu nyingine za taifa zinazowania fainali hizo za Cameroon.
Nyota hao wa Simba waliopo timu za taifa ni;  Aishi Manula, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Shiza Kichuya na John Bocco waliopaa na Taifa Stars.
Wengine Cletus Chama aliyepo na Zambia, Meddie Kagere (Rwanda) Juuko Murshid na Emmanuel Okwi wote (Uganda) wakati kipa Ally Salim na Adam Salamba wapo katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (U-23).
Wakati mastaa hao wakikosekana kocha wa Simba Patrick Aussems ameliamsha upya huko kwa kuwapa kazi maalumu mastraika wake wanne akiwapa kazi ya kufumania nyavu zaidi ya inavyofikiliwa.
Mastraika hao ni Kagere, Okwi waliofunga mabao saba kila mmoja sambamba na Bocco na Salamba wenye mabao mawili kila na mastraika wote hao wanne katika mechi 11 ambazo Simba wamecheza msimu huu wamefunga jumla ya mabao 18.
Iko hivi, msimu uliopita Okwi ambaye alikuwa mfungaji bora wa ligi alifunga mabao 20, Bocco alifunga 14 wakati Kichuya alifunga saba na watatu hao mpaka msimu unamalizika walifunga jumla ya mabao 41 na kuisaidia Simba kubeba taji.
Kkatika kuhakikisha msimu huu mambo yanakuwa vizuri, Kocha Aussems amesisitiza anataka vijana wake wafunge mabao mengi zaidi na kuwapa kazi maalumu nyota hao wanne.
“Msimu uliopita kwenye ligi timu zilikuwa 16 kwa maana hiyo mechi zilikuwa 30 msimu mzima na katika eneo la ushambuliaji Okwi, Bocco na Kichuya ndio walikuwa wakifanya vizuri walifunga idadi hiyo, msimu huu kuna mastraika wanne ambao wanafanya vizuri na wengine bado hawajapata nafasi ya kucheza.”
Alisema ni ngumu kuwawekea idadi ya mabao lakini angependa wafunge mengi hata ikiwezekana 60 kwa ujumla wao na kudai anatamani kuona wanafunga idadi kubwa ya mabao katika mashindano yote.
“Kama kocha jukumu langu ni kuhakikisha timu inatengeneza nafasi nyingi ili wao waweze kupata nafasi ambazo wanatakiwa kuwa makini ili waweze kuzitumia na kufunga katika kila mechi ambayo tutacheza,” alisema Aussems.

MAGOLI AIBUKA
Katika hatua nyingine Mtendaji Mkuu (C.E.O) wa Simba, Crescentius Magori aliibuka katika mazoezi ya klabu hiyo yaliyofanyika katika Uwanja wa Gymkhana jana Ijumaa ambapo Simba walicheza mechi ya kirafiki na vijana ya Azam (U-20).
Magori ambaye alikuwa amekaa zake pembeni alishuhudia Simba wakishinda 1-0 katika mechi hiyo na timu ya vijana ya Azam bao ambalo lilifungwa na Said Ndemla ambaye alipiga shuti kali nje ya boksi kipindi cha kwanza.
Mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo Magori alikaa pembeni na kuzungumza na kocha wa Simba Aussems ambaye walionekana kuelekezana jambo fulani kutokana na ishara zao za mikono ambazo walikuwa wakizionesha.
“Aaah! Nimekuja tu kuangalia mazoezi ya vijana na wanavyo endelea wala sina jipya lolote,” alisema Magori ambaye mara baada ya kumaliza kuongea na Aussems aliingia katika gari yake na kuondoka.

Advertisement