Mastaa walioweka vipengele vya ajabu katika mikataba yao

Saturday November 10 2018

 

PARIS, UFARANSA. MAJUZI imebainika staa mpya wa PSG, Kylian Mbappe alitaka viingizwe vipengele vya ajabu katika mkataba wake wa sasa wakati alipokuwa anahamia klabu hiyo akitokea Monaco ya Ufaransa.

Mbappe alitaka awe mchezaji anayelipwa zaidi klabuni hapo, lakini pia alitaka apewe ndege yake binafsi kwa ajili ya matumizi yake. Hayo sio madai ya kwanza kwa mastaa wa kisasa kutaka yaingizwe katika vipengele vya mikataba yao.

Neymar vs Barcelona

Uhamisho wa staa wa kimataifa wa Brazil, Neymar kutoka klabu ya Santos kwenda Barcelona mwaka 2013 ulikumbwa na mikasa mingi pamoja na tuhuma za rushwa. Lakini ndani ya hilo kulikuwa na madai ya ajabu kutoka kwa staa huyo kwenda Barcelona akidai alihitaji marafiki zake wa karibu wawe naye.

Neymar alitaka Barcelona ilipie gharama za safari za marafiki zake ambao wangemtembelea kutoka kwao, Sao Paulo Brazil kwa ajili ya kumliwaza. Rais wa zamani wa Barcelona, Sandro Rosell ndiye ambaye alitoboa siri hii wakati akiwa mahakamani kukabiliana na kesi ya rushwa katika uhamisho wa Neymar ambaye kwa sasa yupo PSG. Rosell alimwambia Jaji mwendesha mashtaka kwamba klabu hiyo iliwahi kulipa kiasi cha Pauni 430,000 kwa ajili ya kusafirisha kundi la marafiki zake Neymar kwa ndege binafsi kutoka Brazil mpaka Barcelona.

Dennis Bergkamp vs Arsenal

Wakati staa wa zamani wa Arsenal, Marc Overmars alijulikana kama Mdachi anayepaa, staa mwenzake wa kimataifa wa Uholanzi, Dennis Bergkamp aliyekuwa akikipiga naye Arsenal alijulikana kama ‘Mdachi asiyepaa’. Hii ilitokana na tabia yake ya kutopenda kupanda ndege. Alikuwa na hofu na ndege na hakutaka hofu hiyo iiishie mdomoni tu. Aliamua kuweka katika maandishi kabisa ya mkataba wake na Arsenal kuwa hatapanda ndege katika safari za ndege za timu hiyo nje ya England.

Katika kitabu cha maisha yake, Bergkamp aliweka wazi sababu za kutopanda ndege tena na Arsenal iliheshimu mawazo yake. “Nimewahi kupanda ndege kubwa na ndogo, na ndogo zaidi. Wakati fulani mara moja nikiwa na Ajax tuliwahi kupaa juu ya Milima Etna karibu na Naples. Hali ambayo tuliipata ilinitisha sana. Kuhusu suala la kuruka na ndege nadhani sitaruka tena na ndege,” alisema Berkamp katika kitabu hicho. Kisha akaongeza: “Katika maongezi yangu na Arsenal kama nilisema neno ‘milioni’ basi watanirudisha mpaka ‘mia’ kwa sababu sipai na ndege. Na nilikubali.”

Ronaldinho vs Flamengo

Kipaji cha Ronaldinho, tabasamu lake, uwezo wake wa kushangaza uwanjani vilimfanya awe shujaa wa vijana wengi waliomuona akicheza mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Hata hivyo, nje ya uwanja bado Ronaldinho alikuwa na akili za ajabu ajabu. Ni wazi Ronaldinho alipenda sana starehe nje ya uwanja. Alitoa madai ya kushangaza wakati aliporudi kwao Brazil kukipiga klabu ya Flamengo akitokea AC Milan mwaka 2011. Ronaldinho aliwaambia Flamengo kuwa katika mkataba wake alitaka aruhusiwe kwenda out kujirusha katika klabu za usiku mara mbili kwa wiki.

Kutokana na Flamengo kumhitaji sana Ronaldinho ilikubaliana na sharti hilo bila ya kusita.

 

Giuseppe Reina vs Arminia Bielefelf

Kuna mambo yanachekesha sana linapokuja suala hili. Sikia hii. Ilikuwa kali zaidi. Mshambuliaji wa Kijerumani, Giuseppe Reina aliamua kwenda njia tofauti na maombi mengi ya mkataba ya wenzake wakati alipokuwa anahama Klabu ya SG Wattenscheid 09 kwenda Arminia Bielefeld hapohapo Ujerumani mwaka 1996. Wakati akiwa katika mazungumzo ya maslahi binafsi na timu hiyo, Reina aliomba ajengewe nyumba katika kila mwaka wa mkataba wake wa miaka mitatu na klabu hiyo. Ilionekana kama jambo zito kwa klabu hiyo lakini kumbe ambacho Reina alisahau ni kuelezea ukubwa wa nyumba au ubora wa nyumba hiyo.

Arminia wakaguna na kufanya ujanja wa ajabu. Kila mwaka walikuwa wanamjengea nyumba nzuri ya nyasi!

 

Guie-Mien

Nyota wa zamani wa Timu ya Taifa ya Congo Brazzaville alitumia akili nzuri kuhakikisha mke wake ananufaika na uhamisho wake kutoka Karlsruher SC kwenda Eintracht Frankfurt mwaka 1999.

Rolf-Christel Guie-Mien alihakikisha familia yake itaendelea kuwa bora hata akiachana na mpira baada ya kuweka kipengele katika mkataba wake kwamba klabu ya Frankfurt italazimika kumpeleka shule mkewe akasomee masomo ya upishi wakati yeye akipiga soka katika klabu yao.

Georg Koch vs PSV Eindhoven

Kuna wanadamu hawataki kabisa ujinga. Huyu ni mmojawapo. Kipa wa Kijerumani, Georg Koch mwaka 1997 aliamua kwenda nchi jirani ya Uholanzi kukipiga katika Klabu ya PSV Eindhoven akitokea Fortuna Düsseldorf. Moja kati ya kipengele ambacho alikiweka klabuni hapo ilikuwa ni kukatisha mkataba wake endapo kama angefanyiwa vitendo vya ubaguzi wa rangi. Ni kweli, alidumu PSV kwa kipindi cha miezi mitatu tu kabla ya kuvunja mkataba wake kutokana na kufanyiwa kitendo cha ubaguzi. Alirudi kwao Ujerumani kukipiga Klabu ya Arminia Bielefeld akiachana na upuuzi wa ubaguzi wa rangi wa majirani zao. Shukrani kwa mkataba wao.

 

Eto’o vs Anzhi Makhachkala

Uhamisho ulioshagaza wengi huu hapa. Wengi hawakuutarajia. Ni wakati staa wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto'o alipoamua kutua Anzhi Makhachkala ya Russia akitokea Inter Milan ambayo msimu mmoja uliopita ilikuwa imechukua ubingwa wa Ulaya. Mkataba wa staa huyu wa zamani wa Barcelona ulikuwa mnono sana huku akiingiza zaidi ya Pauni 20 milioni kwa mwaka. Lakini kama vile aitoshi aliingiza kipengele cha ajabu ndani yake.

 Mkataba wa Eto’o uliweka wazi staa huyo angekuwa anasafirishwa na ndege binafsi kutoka Mak​hachkala kwenda Moscow ambako alipendelea zaidi kuishi.

Kylian Mbappe vs PSG

Madai ya ajabu zaidi kuwahi kutolewa na mchezaji katika zama mpya. Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi wa kidaku kutoka katika Gazeti la Der Spiegel la Ujerumani, staa wa PSG, Kylian Mbappe ambaye alikuwa anatakiwa na klabu mbalimbali akiwa na Monaco inadaiwa aliipa PSG sharti la kukodiwa ndege binafsi kwa saa 50 kila mwaka katika mkataba wake wa sasa.

Hata hivyo, PSG ilikataa madai hayo ya Mbappe ingawa baadaye iligundulika ilikubali kugharimia kiasi cha Pauni 26,000 kila mwezi kwa ajili ya mfanyakazi wake binafsi, dereva na mlinzi wake.

 

Advertisement