Mastaa walioshabikia timu pinzani utotoni

Muktasari:

Andres Iniesta ni mmoja wa mastaa wa soka maarufu duniani waliokuwa wakishabikia timu pinzani walipokuwa watoto

WAKATI mwingine mastaa wa soka huwa wanaishia katika klabu ambazo hawakutarajia kuzichezea utotoni. Kama ni mapenzi kwa klabu fulani, basi kumbe walikuwa na mapenzi na klabu ambazo baadae hawakujua kama zingekuwa timu pinzani. Wafuatao ni baadhi ya mastaa ambao walikuwa mashabiki wa timu pinzani utotoni.

Gareth Bale (Arsenal)
Staa wa kimataifa wa Wales ambaye alijenga jina kubwa katika klabu ya Southampton baada ya kuibukia katika timu ya vijana ya Southampton. Licha ya kucheza kwa mafanikio Tottenham lakini kitu ambacho mashabiki wa timu hiyo hawakujua ni ukweli kwamba staa huyo alikuwa shabiki mkubwa wa timu pinzani ya Tottenham, Arsenal. Aliwahi kukiri kwamba alikuwa shabiki mkubwa wa Arsenal huku akikoshwa na kiwango cha mastaa wa zamani wa timu hiyo akina Patrick Vieira na Thierry Henry. Mwaka 2013 alijiunga na Real Madrid kwa rekodi ya uhamisho ya dunia pauni 85 milioni.


 Isco (Barcelona)
Kabla ya kusaini Real Madrid kutoka Malaga katika dirisha kubwa la majira ya majira ya joto mwaka 2013 akinunuliwa kwa dau la Euro 30 milioni, Isco aliweka wazi kwamba hakuwa shabiki wa Real Madrid huku akidai kwamba klabu hiyo ilikuwa imejaa watu wajinga. Mapenzi yake kwa Lionel Messi wa Barcelona yalikuwa makubwa kiasi kwmaba hata mbwa wake alimuita jina la staa huyo wa kimataifa wa Argentina huku akiitakia mema Barcelona.

 Ole Gunnar Solskjaer (Liverpool)
Staa wa zamani wa kimataifa wa Norway ambaye ni  kipenzi kikubwa cha mashabiki wa Manchester United kutokana na tabia yake ya kutupia mabao ya mara kwa mara akitokea katika benchi. Mashabiki wa United hawakujua kama Ole Gunnar Solskjaer alikuwa shabiki mkubwa wa Liverpool kabla hajajiunga na timu yao mpaka pale alipotoa kitabu cha maisha yake alichokiita ‘Baby Faced Assassin’. Mwenyewe anadai kwamba alikoshwa zaidi na mafanikio ya Liverpool katika miaka ya 1980.

 Jamie Carragher (Everton)
Kwa mashabiki wa Liverpool, Jamie Carragher ni mwenzao wa damu. Na yeye kwa sasa ni shabiki mkubwa wa Liverpool huku akiwananga mashabiki wa timu pinzani Everton kila anapopata nafasi. Hata hivyo Carragher alikuwa shabiki mkubwa wa Everton utotoni mpaka alipopata fursa ya kujiunga na Liverpool na kuibuka kuwa staa huku akiichezea timu hiyo zaidi ya mechi 700. Kwa sasa familia yake pia imekuwa Liverpool.

 Mario Balotelli (AC Milan)
Super Mario Balotelli ni mmoja kati ya wachezaji watukutu katika soka la kisasa. Aliibukia katika klabu ya Inter Mlan lakini kama ilivyo kawaida yake ya kuongea anachojisikia, aliwahi kuweka wazi kwamba yeye ni shabiki mkubwa wa timu pinzani ya Inter, AC Milan. Kitendo hicho kilizua chuki kubwa kwa mashabiki wa Inter dhidi yake. Baadaye Balotelli alitimiza ndoto yake ya kukipiga AC Milan wakati alipochukuliwa kwa mkopo kutoka Liverpool.

 Raul (Atletico Madrid)
Mmoja kati ya wachezaji wakongwe wanaoheshimika zaidi katika viunga vya Santiago Bernabeu. Raul alianzia soka katika klabu pinzani ya Atletico Madrid huku yeye na familia yake wakiwa mashabiki wakubwa wa Atletico. Ni Real Madrid ndio ambayo ilimpatia mafanikio makubwa katika soka na mpaka sasa anaheshimika zaidi huko hata hivyo familia yake imebakia kuwa mashabiki wa Atletico Madrid.

 Paolo Maldini (Juventus)
Kauli yake ilileta utata kwa sababu familia ya Maldini inajulikana zaidi kwa kupenda AC Milan. Katika kipindi chote cha maisha yake ya soka Maldini alichezea klabu moja tu ya AC Milan ambayo anapendwa na kuhusudiwa kwa kiasi kikubwa mpaka sasa. Hata hivyo aliwahi kutoa ushuhuda kwamba utotoni aliwahi kuwa shabiki mkubwa wa Juventus lakini aliamua kukipiga katika klabu ya AC Milan ambayo hata baba yake Cesare aliwahi kuichezea na kupata nayo mafanikio.

 Andres Iniesta (Real Madrid)
Mmoja kati ya wachezaji wanaoheshimika zaidi katika historia ya Barcelona. Ameondoka katika dirisha kubwa lililopita kwenda Japan baada ya kuichezea Barcelona kwa miaka 17. Katika moja ya ushuhuda wake Iniesta aliwahi kukiri kwamba alikuwa na mapenzi makubwa na Real madrid. Angeweza kwenda Santiago Bernabeu na kuendelea kipaji chake lakini mwenyewe aliamua kutua katika shule ya soka ya Madrid

 Adam Lallana (Everton)
Kiungo wa kimataifa wa England ambaye kwa sasa anauguza majeraha ya mara kwa mara Liverpool. wakati akisaini Liverpool mwaka 2014 akitokea Southampton staa huyu alikiri wazi kwamba utotoni alikuwa shabiki wa Everton ambao ni wapinzani wa Liverpool. “Baba alikuwa ananisimulia mambo mazuri kuhusu Everton wakati huo ikiwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuchukua ubingwa wa FA miaka ya 1970 na 1980. Lakini hata hivyo Everton hawakuwa wazuri wakati nilipoanza kuwashabiki.” Alisema Lallana wakati huo.

 John Terry (Manchester United)
Akiongea na waandishi wa habari mwaka 2006, nahodha huyu wa zamani wa Chelsea ambaye ni mmoja kati ya wachezaji wanaoheshimika zaidi katika historia ya klabu hiyo aliweka wazi kwamba utotoni alikuwa shabiki mkubwa wa Manchester United. Mpaka sasa ana kumbukumbu ya kukutana na Sir Alex Ferguson akiwa mtoto. “Nilikuwa shabiki wa Manchester United wakati nakua. Unajua inakuaje wakati unapokuwa mtoto, unataka kushabikia timu ambayo inashinda kila kitu. Na baba yangu na babu walikuwa mashabiki wa man United. Hata hivyo siku yangu ya kwanza Chelsea nilijua kwamba hii ndio sehemu ambayo nilitakiwa niwe. Lakini hata Manchester United nao walinitaka. Nilikutana na Sir Alex Ferguson nikafurahi kusalimiana naye. Wakati wa likizo za shule ningeweza kwenda Manchester kwa treni na vijana wenzangu tukafanya mazoezi na kurudi nyumbani.”