Mastaa waliokoleza chuki

Muktasari:

 

  • Mashabiki wa timu kama za Arsenal na Tottenham hawezi kupikika chungu kimoja, sawa na mashabiki wa Manchester United na Manchester City au wa Real Madrid na Atletico Madrid. Hao ni wapinzani wakubwa.

 

LONDON, ENGLAND.MAISHA ndivyo yalivyo. Huwezi kupendwa na kila mtu na kwamba hakuna asiyekuwa na adui hata kama hana kitu kikubwa alichomtendea.

Kwenye soka mambo yamekuwa hivyo hivyo. Mashabiki wa timu kama za Arsenal na Tottenham hawezi kupikika chungu kimoja, sawa na mashabiki wa Manchester United na Manchester City au wa Real Madrid na Atletico Madrid. Hao ni wapinzani wakubwa.

Lakini, jambo hilo limefanya kujengeka kwa chuki moja kubwa sana na hali inakuwa mbaya inapotokea mchezaji mmoja anakuwa na chuki na timu fulani, akiwaombea dua mbaya tu kila siku ili wachapwe. Ikitokea timu hiyo asiyoipenda inashinda, basi anaumia moyo balaa.

Jack Wilshere vs Tottenham

Kiungo, Jack Wilshere hawapendi Tottenham. Mwaka 2015, wakati kipindi hicho akiwa Arsenal na kufanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la FA, kiungo huyo wakiwa mtaani na basi lao kutembeleza kombe kwa mashabiki, aliamua kuchukua kipaza sauti na kuanza kuimba nyimbo za kuwadhihaki Tottenham. Wilshere aliwakusanya mashabiki wa Arsenal waliokuwa wakiwashangilia mitaani na kuwaambia kwamba anaswali moja analotaka kuwauliza, swali moja tu kwamba wanawafikiriaje Tottenham?”. Kisha alitoa kauli ya kama tusi hivi na hiyo inatokana na chuki yake kwa timu hiyo. Alipigwa faini ya Pauni 40,000 kwa kitendo chake hicho. Alihama Arsenal kwenda West Ham na kuendeleza chuki zake kwa Spurs.

Gary Neville vs Liverpool

Gary Neville aliwahi kusisitiza kwamba kitu asichokipenda ni Liverpool. Beki huyo wa zamani wa Manchester United aliwahi kusema kwamba hakuna kitu anachokielewa kuhusu Liverpool, haipendi timu, hawapendi watu wake, kwa kifupi hakuna anachokipenda kuhusu timu hiyo. Chuki yake dhidi ya Liverpool iliwahi kumgharimu Neville na kupigwa faini ya Pauni 10,000 baada ya kushangilia kishabiki mbele ya mashabiki wa timu hiyo wakati Rio Ferdinand alipofunga bao dakika za mwisho dhidi ya Liverpool huko Old Trafford.

Jamie Carragher  vs Everton

Ni hivi, Gary Neville haipendi Liverpool, sawa na ilivyo kwa beki wa zamani Jamie Carragher haipendi Manchester United. Lakini, unaambiwa hivi kwa Carragher anakuwa na furaha kubwa zaidi kama Everton ikiwa inafungwa. Beki huyo wa zamani ameweka wazi hilo kwenye kitabu chake akidai kwamba anakuwa mtu mwenye furaha sana wakati Everton wanapofungwa, iwe kwenye mechi walizocheza na Liverpool au kwenye mechi yao na timu nyingine yoyote ile. Carragher alisema kwake yeye kuna Everton za aina mbili, ile ya kwanza kabla ya Liverpool na ile ya baada ya Liverpool.

Gerard Pique vs Real Madrid

Beki wa kati wa Barcelona, Gerard Pique aliwahi kukiri huko nyuma kwamba siku zote amekuwa akitaka mambo yawaendee hovyo Real Madrid, hiyo ndio dua yake ya kila siku. Kwa chuki aliyokuwa nayo Pique kwa Real Madrid ni kwamba hata kama watacheza mechi dhidi ya jiwe, basi yeye atakuwa upande wa hilo jiwe. Kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2015, Pique hakutaka kuleta uzalendo sijui wa timu ya Hispania, yeye aliamua kuvaa jezi ya kipa wa Juventus kwa wakati huo, Gianluigi Buffon wakati timu walipowachapa Los Blancos kwenye mechi za michuano hiyo ya Ulaya.

Wayne Rooney vs Liverpool

Straika, Wayne Rooney amekulia kwenye familia ya mashabiki wa Everton watupu. Jambo hilo limemfanya staa huyo kuwachukia sana Liverpool hasa ukizingatia ndio wapinzani wakubwa wa Everton, timu ambayo aliichezea pia katika awamu mbili tofauti. Hata alipoondoka Everton, Rooney alikwenda kujiunga na Manchester United, ambao pia ni wapinzani wakubwa wa Liverpool. "Nimekuwa nikishabikia Everton, familia yangu wote ni Everton na nimekuzwa nikiwachukia Liverpool. Hiyo haijawahi kubadilika," alisema.

Wachezaji wengine

Kwenye orodha hiyo ya kushuhudia mchezaji mmoja akiwa na chuki na timu fulani inamhusu pia staa wa Tottenham, Dele Alli, ambaye hawapendi kuliko maelezo Arsenal, sawa na ilivyo kwa mkongwe Teddy Sheringham, ambaye hataki kabisa kuwasikia Arsenal. Steven Taylor amekuwa na chuki dhidi ya Sunderland, wakati Carlos Tevez hawezi kukuelewa kabisa ukianza kumletea habari zao za River Plate, hawapendi kwelikweli sawa na

Ian Wright na Theo Walcott wanavyoichukia Tottenham.