Mastaa waliokalia moto Ligi Kuu

DODOMA. LIGI Kuu Tanzania Bara inaendelea baada ya pazia lake kufunguliwa Septemba 6 na ndio kwanza timu zinasaka matokeo bora ukijumlisha na ushindani kwenye michezo miwili ya mwanzo, ni wazi zimepania msimu huu.

Makala haya yanaangazia wachezaji ambao wana kila sababu ya kushinda presha za kusajiliwa kwenye timu zao wakiwa na lengo moja tu - kuhakikisha wanathibitisha ubora wao ambao mashabiki na hata viongozi wa timu husika wanatarajia kutoka kwao.

Bernard Morrison-Simba

Achana na mechi aliyong’ara dhidi ya Vital’ O ya Burundi ukiwa ni mchezo maalum wa kirafiki katika kunogesha tamasha la ‘Simba Day’ bado winga huyu mshambuliaji aliyesajiliwa kwa mbwembwe akitokea kwa wapinzani wao wakubwa nchini, Yanga SC.

Aina iliyotumika kumsajili, ndivyo ambavyo inawapa sababu kubwa wapenzi wa soka nchini na haswa wa timu yake Simba, wanaosubiri kuona akitesa mabeki wa timu pinzani na kuisaidia pia timu hiyo kuendeleza ubabe wao na hata Ligi ya Mabingwa Afrika.

Alain Akono-Azam

Jina lake ni Alain Thierry Akono, mzaliwa wa Bafang nchini Cameroon, aliyesajiliwa na ‘waoka mikate’ hao kutokea timu ya kwao Fortuna Du Mfou, anasubiriwa na wapenzi wa soka nchini na zaidi timu yake Azam, akitarajiwa kuthibitisha ubora wake uliomfanya asajiliwe na timu hiyo.

Prince Dube, Mzimbabwe huyu aliyesajiliwa pamoja na Akono msimu huu, ameshafanya yake kwa kufunga mabao mawili kwenye mchezo uliopita, akimuachia msala Mcameroon aliyesajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili kuitumikia Azam.

Yusuph Soka-Coastal Union

Kabla ya kutangazwa kutua kwake Coastal Union, Yusuph Soka alitajwa kwa muda mrefu kuwa kwenye rada za kusajiliwa na Yanga ikiwemo kufanya maandalizi ya msimu pamoja na timu hiyo lakini haikutosha kupewa mkataba na mabosi wa timu hiyo ya Jangwani.

Matokeo yake amekwenda kuziba pengo la Ayoub Lyanga aliyetimkia Azam, ambapo aina yake ya uchezaji inafanana na ya Lyanga aliyekuwa staa wa wagosi hao wa kaya, Soka pia anakabiliwa na kazi mpya ya kuwaonyesha wapenzi wa soka nchini, kwa nini alikuwa anatajwa kuwa kwenye kiwango sawa na Mbwana Samatta.

Mbaraka Yusuph- Kagera Sugar

Kama sio majeraha yaliyomweka nje kwa zaidi ya msimu mzima akiitumikia kwa mkopo Namungo ya Lindi msimu uliopita akitokea Azam, pengine tungeweza kuendelea kupata ya kuzungumza kuhusu mshambuliaji huyu aliyeng’ara wakati akiwa Kagera Sugar.

Kushindwa kutamba akiwa na Azam na hata Namungo hatimaye kumemrudisha kwa timu iliyowahi kumng’arisha, Kagera Sugar ambayo ametua kwenye dirisha la usajili lililopita. Kazi iliyopo kwake ni kutaka kurudisha upya makali yake kupitia timu hiyo.

Mohammed Ibrahim-Kagera Sugar

Nini kimemkuta? Mohamed Ibrahim aliwahi kuwa kiungo mshambuliaji matata mno wakati akiwa na Mtibwa Sugar iliyomfanya asajiliwe na ‘wekundu wa msimbazi’ Simba, alifanikiwa kufanya vema akiwa na mabingwa hao mfululizo wa taji la ligi kuu na uwepo wa mastaa wengi kikosini hapo, msimu uliopita alitolewa kwa mkopo Namungo ambayo alishindwa kutoboa.

Namungo haijaona kipya kutoka kwake na kuachana naye kabla ya Kagera Sugar chini ya kocha Mecky Mexime kumsajili na sasa anasubiriwa kurudi kwenye ubora wake, kasi yake na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti ndicho kinachosubiriwa na wapenzi wa soka nchini.

Reliants Lusajo-KMC

Wakati Namungo wakitarajiwa kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kombe la shirikisho msimu huu, taarifa za mfungaji wao bora wa msimu. Reliants Lusajo kutimkia timu ya KMC zilishtua wengi akiwemo Hitimana Thierry-kocha wa Namungo, awali ilikuwa kusaini Yanga au kubaki lakini haikuwa hivyo.

Lusajo aliyeziba pengo la Charles Ilanfya aliyetua Simba, sasa anakabiliwa na kazi mpya ya kuendeleza pale alipoishia akiwa na Namungo na anasubiriwa kuendeleza ubora wake wa kuzifumania nyavu za timu pinzani ili kuthibitisha kwamba hakubahatisha msimu uliopita.

Ibrahim Ahmada Hilika-Mtibwa Sugar

Ukienda visiwani Zanzibar, mshambuliaji huyu ni maarufu mno kwa uwezo wake mkubwa wa kuzifumania nyavu za timu pinzani, usumbufu wake, ubabe awapo uwanjani dhidi ya mabeki wa timu pinzani na hata kufunga mabao ni sifa inayombeba Hilika.

Mchezo wa kirafiki aliocheza dhidi ya Mtibwa Sugar wakati wa maandalizi ya msimu huu, uliwakuna vichwa mabosi na kocha wa timu hiyo, Zubeir Katwila ambaye hakufanya ajizi akamsajili, sasa kazi iliyopo mbele yake ni kufanya aliyozoea kuyafanya kule ligi kuu Zanzibar.

Shizza Kichuya-Namungo

Taarifa za kuwa kwake Namungo hazikueleweka kwa wengi ambao walidhani amepelekwa kucheza kwa mkopo akitokea Simba, haikuwa hivyo. Kichuya alimaliza mkataba wake wa miezi sita aliokuwa nao pale Simba, Namungo ikamsainisha mkataba halali akiwa mchezaji huru.

Kichuya aliyetamba akiwa Simba na kumpa fursa ya kusajiliwa kucheza soka la kulipwa nchini Misri, bado hajaonyesha ubora wake kama aliokuwa nao Mtibwa na baadaye Simba, kazi aliyonayo msimu huu akiwa na Namungo ni kurudisha ubora wake ambao wengi wanausubiria.

Carlos Carlinhos-Yanga

Aliingia dakika za mwishoni kwenye mchezo wa “Wiki ya Mwananchi” dhidi ya Aigle Noir na baad aya hapo hakucheza mchezo uliofuata wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons kabla ya kuingia kipindi cha pili mchezo uliofuata dhidi ya Mbeya City na akapiga kona iliyozaa bao lililofungwa na beki Lamine Moro.

Bado haijatosha kukata kiu ya mashabiki wa soka ambao wanasubiri kuona nini atakifanya msimu huu, kulingana na mapokezi aliyopokea kutoka kwa wapenzi wa timu hiyo.