NI NOMA: Mastaa waliofunga mabao mengi kwa mpishi mmoja

Muktasari:

Wafuatao ni mastaa ambao wametupia mabao mengi zaidi kupitia mpishi mmoja ndani ya timu.

LONDON, ENGLAND.NYUMA ya kila staa mahiri wa kutupia nyavu kuna mpishi ambaye inawezekana haimbwi sana katika vyombo vya habari. Wafuatao ni mastaa ambao wametupia mabao mengi zaidi kupitia mpishi mmoja ndani ya timu.

Christian Eriksen kwa Harry Kane – 15

Miongoni mwa mastaa ambao waliwasili Tottenham dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2013 kwa ajili ya kupunguza maumivu ya pengo lililoachwa na mkali Gareth Bale aliyekuwa ameuzwa Real Madrid. Ni staa wa kimataifa wa Denmark, Christian Eriksen kwa kiasi kikubwa ndiye aliyechangia kuibua makali ya Harry Kane kwa kumpigia pasi murua za mabao. Mara 15. Sio mbaya kujiuliza mambo yangeanza vipi kwa Kane katika maisha yake ya soka Tottenham bila ya Eriksen.

Thierry Henry kwa Freddie Ljungberg – 15

Muosha huoshwa. Thierry Henry alikuwa mfungaji mahiri Ligi Kuu England pia alikuwa mpishi mahiri vilevile. Msimu mmoja wa Ligi Kuu aliwahi kuweka rekodi ya kupika mabao mengi zaidi. Mabao 20 ndani ya msimu mmoja.

Mmoja kati ya wachezaji ambao wamewahi kunufaika sana na kasi ya Henry ni staa wa kimataifa wa Sweden, Ljungberg wakati akiwa katika ubora wake. Alifunga mabao 15.

David Silva kwa Sergio Aguero – 16

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ameipeleka kombisheni ya wawili hawa katika anga nyingine kabisa. Tayari walikuwa wameibadili Man City kwa muda mrefu lakini sasa wanaibadili zaidi. Aguero amekuwa mfungaji bora wa muda wote katika historia ya Manchester City. Katika idadi ya mabao mengi aliyofunga Ligi Kuu ya England mabao 16 aliyafunga kwa pasi za David Silva.

Nolberto Solano kwa Alan Shearer – 16

Mfungaji bora wa muda wote katika Ligi Kuu ya England akistaafu soka akiwa na mabao 260 kibindoni. Alifunga mabao akiwa na Southampton, Blackburn Rovers na Newcastle lakini mabao mengi aliyafunga akiwa na Newcastle United. Na katika mabao hayo alinufaika zaidi na ubora wa staa wa kimataifa wa Peru, Noberto Solani ambaye alimpikia mabao 16.

Robert Pires to Thierry Henry – 17

Moja kati ya kombinesheni bora kuwahi kutokea katika Ligi Kuu ya England. Katika orodha hii Henry anatokea mara mbili kuthibitisha jinsi gani alikuwa bora uwanjani wakati wa zama zake. Kwanza alitokea katika kupiga pasi za mwisho kwa Fredrick Ljungberg lakini hapa anatokea kama mmaliziaji wa pasi za mwenzake. Kombinesheni ya Kifaransa kati yake na Robert Pires ilikuwa tishio uwanjani na ilimuacha Henry akinufaika na pasi 17 za mwisho za Pires uwanjani.

Kuna wakati waliwahi hata kupasiana penalti katika pambano dhidi ya Manchester City lakini wakachemsha.

Steve McManaman to Robbie Fowler – 20

Awali walijulikana zaidi kama Spice Boys kutokana na tabia yao ya kupenda kuvaa vizuri na kujirusha nje ya uwanja. Kombinesheni ya Steve Mcmanaman na Robbie Fowler ilikuwa tishio uwanjani Anfield na kwingineko. Katika kipindi cha miaka sita ambayo walicheza wote McManaman alipiga pasi za mwisho 20 kwa Robbie Fowler ambaye alifunga. Kama si kuondoka kwa McManaman kuelekea Real Madrid si ajabu kombinesheni hii ingeweza kuongoza katika ukurasa huu.

Darren Anderton to Teddy Sheringham – 20

Kwa jinsi ambavyo majeraha yalivyomuandama katika kipindi kirefu cha maisha yake ya soka, inashangaza kumuona Darren Anderton katika orodha hii.

Moja kati ya kombinesheni bora kuwahi kutokea katika Ligi Kuu ya England ni hii hapa ya Tottenham Hotspurs. Anderton alimtengea Teddy pasi 20 za mabao. Ukizingatia Teddy pia alitamba akiwa na Manchester United inakupa picha Anderton alikuwa mtu wa namna gani kwake. Bila ya kuwa na majeraha ya mara kwa mara kwa Anderton si ajabu kombinesheni hii ingeweza kuongoza katika ukurasa huu.

Frank Lampard kwa Didier Drogba – 24

Wanaochukua heshima ya juu katika orodha hii ni mastaa hawa wawili kutoka Chelsea. Wanaheshimika klabuni hapo kutokana na ubabe waliotembeza chini ya utawala wa pesa za Roman Abramovich. Wote wawili kwa pamoja wametwaa kwa heshima mataji makubwa 12 klabuni hapo.