Mastaa waliofariki dunia na umaskini wao

Thursday March 14 2019

 

By Thomas Matiko

IJUMAA iliyopita, alipumzishwa rapa lejendari Chris Kantai, 'Chris Kantadda' nyumbani kwao Ngong. Kantadda aliyevuma miaka ya nyuma alifariki dunia yapata wiki tatu zilizopita akiwa na umri wa miaka 40.
Kifo cha Kantai kiliibua maswali mengi huku akiuma pamba akiwa mmoja wa mastaa wa burudani waliofariki dunia wakiwa maskini nchini. Hawa hapa pamoja naye waliofariki dunia wakiwa maskini pamoja na umaarufu wao mkubwa ndani na nje ya Kenya.
KANTAI
Japo anadaiwa kutokea kwenye familia ya kitajiri au ukipenda jamii ya watu wenye nafasi zao, Kantai hangeweza kujihesabu miongoni mwao.
Hakuwa na lolote la kujivunia zaidi ya umaarufu. Mmoja wa maswahiba wake wa siku nyingi guru wa burudani nchini Budhaa Blaze, kadai marehemu Kantai enzi za uhai wake mara kwa mara alihoji ni kwa nini mashabiki wake walimsifia kwa alivyokuwa mkali kwenye michano ila hakuwa anaona matunda ya muziki wake.
Kwenye makundi ya WhatsApp ya wasanii, Mashirika yao MCSK na MPAKE ambayo hukusanya fedha zitokanazo na utumikaji kwakazi za wasanii nchini kwa niaba yao, zilishindwa kueleza ni kwa nini hazikuweza kumlipa Kantai stahili ya kazi zake.
Kwenye wimbo wake wa ‘Issues’ Kantai alifunguka kuhusu maisha magumu aliyokuwa akipitia licha ya kuwa staa. Alikiri wazi wazi hakuna faida aliyopata kutokana na muziki wake au umaarufu.
Ugumu wa hali ya kimaisha ulimsukuma kuingilia ulevi hali iliyomvurugia kabisa uendelevu wa kimaisha na muziki.
MZEE OJWANG
Hata baada ya kuigiza kwa zaidi ya miaka 30 kwenye vipindi maarufu kama ‘Vitimbi’, ‘Vioja Mahakamani’ miongoni mwa zinginezo, mvunja mbavu, Benson Wanjau 'Mzee Ojwang' alimalizia maisha yake kwa mateso.
Ojwang anayetajwa kuwa mwanzilishi wa komedi nchini, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78, akiwa hana lile wala hili ila nafsi yake tu.
Shirika la habari la KBC lilishtumiwa kwa kumtimiza kwa zaidi ya miongoni 30 kisha kumtelekeza. Akifariki dunia, Mzee Ojwang alikuwa ameajiriwa na Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni na mshahara wake ulikuwa umepanda hadi kufikia Sh50,000 katika miaka yake ya mwisho.
Licha ya kazi hiyo aliyoifanya kwa zaidi ya miaka 17, ukiongeza na kipato alichopiga kupitia uigizaji pale KBC, bado Mzee Ojwang aliishi maisha ya kawaida sana. KBC ilipoamua kumfuta kazi Julai 2014, inasemekana haikumlipa hata senti moja ya kiinua mgongo wake.
Umaskini wake ulikuja kudhihirika alipougua kutokana na umri mkubwa na kushindwa kugharimia matibabu yake kwa ukosefu wa fedha. Hapo ndipo serikali iliingilia kati baada ya ishu yake kuangaziwa na vyombo vya habari. Alifariki dunia mwaka mmoja baadaye
AYEIYA
Mvunja mbavu Emmanuel Makori 'Ayieya' alifariki dunia Aprili baada ya kuhusika kwenye ajali mbaya ya barabarani.
Kifo chake kiliibua mdahalo mkubwa kuhusu ikiwa komedi inalipa nchini kwa sababu Ayeiya alifariki dunia maisha yake yakiwa kama tu ya yakhe.
Baada ya kifo chake, msheshi Rapcha The Sayantist alijitokeza na kumkashifu Churchill kwa kumlipa visenti vidogo Ayieya licha ya kuchangia mafanikio ya Churchill Show na vichekesho vyake. Alifariki akiwa maskini.
Kabla ya kifo chake Ayieya alikuwa amerejea kwenye Churchill Show aliyokuwa amejitoa kwa kile kilichosemekana mapato duni. Alirejea baada ya kushauriana na Churchill lakini hakudumu sana kifo chake kilipojiri.
ACHIENG ABURA
Oktoba 2016, kwenye sherehe ya Mashujaa Day mwanamuziki wa Afro Pop na jazz Abura aliuma pamba akiwa katika Hospitali ya Nairobi alikokuwa akipata matibabu.
Kabla ya kifo chake, Abura alifanya mahojiano na mwandishi wa gazeti la Bussiness Daily, Jackson Biko na alikiri kupitia kipindi kigumu cha kifedha.
Abura alimwambia Biko alikuwa amehusika sana kuwasaidia wenzake, ila alipowahitaji kumsaidia kuchangisha pesa za matibabu yake, wote walimkimbia.
Abura alisema aliandaa michango kadhaa lakini ni watu wachache sana waliomsapoti. Kilichomuumiza moyo zaidi, hata wale aliodhania walikuwa watu wake wa karibu sana ambao walikuwa watu wenye nafasi na riziki kubwa, walitoweka. Aliamini wengi wao walitaka kujihusisha naye kwa sababu ya umaarufu wake.
SHAVEY
Pamoja na msanii mwenzake Slice, walihiti yapata mwongo uliopita walipoachia hiti ya ‘Gyal’ kipindi muziki aina ya dancehall uilikuwa umeanza kushika kasi.
Wasanii hao walikuwa chini ya lebo ya Ulopa Ngoma. Kwa pamoja kama kundi walirekodi kazi nyingi chini ya Ulopa ambazo Slice aliwahi kusema hazikutoka kwa kubaniwa na Ulopa.
Shavey alifariki dunia mwaka jana baada ya kugongwa na Matatu barabarani.
Hata hivyo, kabla ya kifo chake kulisambaa video aliyorekodiwa akiikashifu Ulopa kwa kuwatumia vibaya na kisha kuwaachanisha wakiwa hawana lolote. Shavey alisema hawakuwahi kuifaidika kutokana na kazi zao. Hadi wakati wa kifo chake, Shavey alikuwa ameachana na muziki naye mwenzake Slice akirejea vijijini.

Advertisement