Mastaa wa zamani sasa wanamiliki klabu za soka

Muktasari:

  • Hata hivyo, wapo baadhi ya wachezaji ambao wameamua kuwekeza katika timu mbalimbali kwa kuzinunua.

NEW YORK, MAREKANI.MARA nyingi wachezaji wengi hugeukia kazi ya ukocha huku na uchambuzi ambayo imekuwa ikishamiri kwa kasi kubwa kutokana na kuibuka kwa vituo vingi vya televisheni.

Hata hivyo, wapo baadhi ya wachezaji ambao wameamua kuwekeza katika timu mbalimbali kwa kuzinunua.

David Beckham - Inter Miami CF

Staa wa zamani wa Manchester United, Real Madrid na AC Milan ambaye alitengeneza pesa nyingi katika mchezo wa soka baada ya kutumika katika matangazo mengi ya biashara kufuatia mvuto aliokuwa nao katika soka.

Kwa sasa Beckham anamiliki wa klabu ya Inter Miami FC ya jijini Miami kule Marekani. Klabu hiyo inatazamiwa kushiriki Ligi Kuu ya Marekani msimu ujao. Kabla ya hapo Beckham ambaye ni mume wa mwanamuziki mahiri wa Uingereza, Victoria Adams alikuwa amefikiria kutumia jina la Miami FC lakini tayari jina hilo lilikuwa limechukuliwa na timu nyingine.

Paolo Maldini - Miami FC

Ndiye aliyelichukua jina la Miami FC. Staa wa zamani wa AC Milan na Timu ya Taifa ya Italia, Paolo Maldini ambaye aliwahi kucheza sambamba na Beckham katika kikosi cha AC Milan wakati Beckham alipotua hapo kwa mkopo akitokea LA Galaxy. Awali Beckham alitegemea kuchukua timu hiyo lakini rafiki yake Maldini akawahi na kulichukua.

Didier Drogba - Phoenix FC

Sio tu staa huyu wa kimataifa wa Ivory Coast amevunja rekodi nyingi kama mchezaji klabuni hapo lakini pia kwa sasa ni mchezaji na mmiliki wa klabu hiyo. Ameingia katika rekodi kama mchezaji wa kwanza kumiliki huku akicheza pia. Ameinunua Phoenix Rising, lakini bado anaendelea kuichezea timu hiyo hata wakati huu akiwa amepitisha miaka 40.

Eden Hazard na Demba Ba - San Diego 1904 FC

Mastaa wawili, mmoja anatamba Chelsea na mwingine alipita hapo ni miongoni mwa watu wanne walioanzisha timu hii sambamba na mastaa wenzao wa soka, Yohan Cabaye na Moussa Sow. Waliinua klabu hii kwa lengo icheze NASL mwaka 2018, lakini kwa sababu ligi hiyo iliondolewa wameweka malengo yao katika kucheza USL.

Giggs, Scholes, Nicky Butt, Nevilles- Salford City FC

Mastaa hawa wa zamani wanajulikana zaidi kwa jina la Class of 92. Ni kikosi cha vijana kilichoundwa na Sir Alex Ferguson ambacho mwaka 1992 kilitwaa ubingwa wa FA wa vijana na wote wakapandishwa katika kikosi cha kwanza cha United.

Urafiki uliwapa wazo la kumiliki timu mara baada ya kustaafu soka na wote wakaanzisha timu ambayo waliita Salford City ambayo kwa sasa ipo madaraja ya chini.

Hata hivyo, wana matumaini muda si mrefu watatinga katika Ligi Daraja la Pili huku wakiwa katika njia ya kuipeleka Ligi Kuu.

Ronaldo Nazario

Mmoja kati ya washambuliaji bora wa muda wote duniani. Ronaldo Luiz Nazario De Lima alitoka katika umaskini uliotopea kwao Brazil. Baada ya kutamba katika soka katika nchi za Ulaya na kwao, Ronaldo aliibuka na utajiri mkubwa.

Haujitumbukiza na kazi ya ukocha na badala yake kwa kushirikiana na bilionea wa Brazil, Carlos Wizard wameamua kuinunua timu ya Real Valladolid ya Ligi Kuu ya Hispania.