Mastaa wa maana wanaopaswa kuhama fasta timu za Top Six

Muktasari:

Hawa hapa ni mastaa wa maana kabisa, lakini sasa kwa msimu huu mambo yamekuwa magumu kwa upande wao kupata nafasi ya kucheza na matokeo yake kujikuta wakisugua tu benchi. Kutokana na hilo, mastaa hao hawana namna nyingine zaidi ya kufungasha tu virago vyao haraka na kwennda kutafuta timu nyingine zitakazowapa nafasi ya kucheza kila wakati.

LONDON, ENGLAND
KLABU za Top Six kwenye Ligi Ku England zina idadi kubwa sana ya wachezaji wa kiwango cha juu na jambo hilo linafanya ushindani wa namba kuwa mkubwa sana kwenye kikosi cha kwanza.
Hawa hapa ni mastaa wa maana kabisa, lakini sasa kwa msimu huu mambo yamekuwa magumu kwa upande wao kupata nafasi ya kucheza na matokeo yake kujikuta wakisugua tu benchi. Kutokana na hilo, mastaa hao hawana namna nyingine zaidi ya kufungasha tu virago vyao haraka na kwennda kutafuta timu nyingine zitakazowapa nafasi ya kucheza kila wakati. Hawa ndio mastaa waliopo kwenye vikosi hivyo vya timu za Top Six wanaopaswa kuhama haraka, pengine kwenye dirisha hilihili la Januari.

Liverpool - Simon Mignolet
Ujio wa kipa Alisson Becker huko Anfield kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana kimekuwa kama kifo kwa Simon Mignolet, hana tena nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Kipa huyo alikuwa na uhakika wa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Liverpool miaka miwili iliyopita, akicheza zaidi ya mechi 200, lakini sasa kila kitu kimekuwa tofauti na kocha Jurgen Klopp humwelezi kitu kwa Mbrazili, Alisson. Panga pangua yupo golini jambo linalomfanya Mignolet kuwa na chaguo moja tu la kufanya, kwenda kutafuta timu nyingine ya kuichezea.

Tottenham - Victor Wanyama
Victor Wanyama alipatwa na majeruhi ya goti kwenye mechi za kujiandaa na msimu huu na alirudi uwanjani baada ya miezi miwili, amepata maumivu mengine jambo lililomfanya ashindwe kabisa kupenya kwenye kikosi cha kocha Mauricio Pochettino. Kocha huyo wa Tottenham Hotspur anachokifanya kwa sasa ni kumpanga Eric Dier kwenye nafasi ya kiungo ya kukaba, jambo linalomfanya Wanyama kusugua tu benchi. Hali ni mbaya, kwani kwa msimu huu, staa huyo wa kimataifa wa Kenya, amecheza mechi nne tu na Spurs wanaripotiwa kwamba wapo tayari kumuuza kwa uhamisho utakaofaidisha pande zote mbili.

Man City - Nicolas Otamendi
Asikwambie mtu, maisha yanakwenda kasi sana. Msimu uliopita, beki wa Kiargentina, Nicolas Otamendi panga pangua alikuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Manchester City kilichobeba ubingwa wa Ligi Kuu England. Lakini, msimu huu mambo yamekuwa tofauti kabisa ambapo beki huyo amejikuta akisubiri tu kwneye benchi na kocha Pep Guardiola amekuwa akiwatumia zaidi mabeki wa kati, John Stones na Aymeric Laporte. Otamendi amecheza mechi 14 tu na hakika anahitaji kutafuta timu nyingine ya kwenda kujiunga nayo ili impatie muda wa kucheza zaidi kwenye kikodi cha kwanza kuliko kukaa benchi.

Chelsea - Victor Moses
Kuwasili kwa kocha Maurizio Sarri huko Chelsea kumefanya maisha ya Victor Moses kuwa magumu na hivyo winga huyo sasa benchi linamhusu. Moses haonekani kuwa kwenye mipango ya kocha huyo Mtaliano kutokana na mfumo wake anaotumia kutohitaji huduma ya Mnigeria huyo. Sarri mwenyewe alishasema wazi kwamba Moses yupo huru kuondoka na hilo limethibitishwa kwa idadi ya mechi alizocheza mchezaji huyo ambapo kwa msimu huu amecheza mara sita tu. Kwa hali ilivyo, Moses hana namna nyingine zaidi ya kuamua kuachana na maisha ya Stamford Bridge sasa kabla hajachelewa.

Arsenal - Aaron Ramsey
Aaron Ramsey ameshaweka mguu mmoja nje akitaka kuachana na Arsenal na huenda hilo likafanyika kwenye dirisha hili la Januari. Kiungo huyo aliambiwa wazi kwamba hataongezwa mkataba mpya baada ya huu wa sasa kufika tamati mwishoni mwa msimu, lakini kuhakikisha anaweka mambo yake sawa, Ramsey aachane tu na Washika Bunduki hao kwenye dirisha hili la Januari ili kufanya thamani yake kuwa kubwa kuliko kuondoka bure. Juventus, Paris Saint-Germain, Barcelona na Inter Milan ni miongoni mwa timu zinazohitaji huduma yake.

Man United - Matteo Darmian
Matteo Darmian amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia huko Italia kwenye Serie A tangu msimu uliopita, lakini ilishangaza baada ya Manchester United kuamua kumng'ang'ania mchezaji aliyekuwa akitaka kuhama. Beki huyo msimu huu ndio mambo yamekuwa magumu kabisa, akiwa amecheza mechi nne tu kabla ya mechi za jana na kwamba anachopaswa kufanya ni kutafuta tu timu nyingine itakayompa nafasi ya kucheza kuliko kuendelea kusugua benchi huko Old Trafford.