Mastaa wa kumbadili Ozil watakavyocheza Arsenal

Muktasari:

  • Hawa hapa mastaa wanaofaa kutua Emirates kuchukua mikoba ya Ozil kama ataachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu na vile Kocha Emery anavyoweza kumtumia kila mchezaji kwenye orodha hiyo atakapotua katika kikosi chake.

LONDON ,ENGLAND.MAISHA ya Mesut Ozil kwenye kikosi cha Arsenal yapo kwenye mashaka makubwa licha ya kusaini mkataba mpya miezi 12 tu iliyopita.

Kwa sasa kiungo huyo wa Kijerumani kitu anachokifanya kwa ufasaha zaidi kwenye kikosi cha Arsenal tangu msimu uanze wakiwa chini ya Kocha Unai Emery basi ni kusugua benchi.

Kwa maana hiyo, wachambuzi wa mambo ya soka wanaamini nyakati za Ozil kuendelea kutamba kwennye kikosi hicho cha Arsenal zimefika tamati. Kocha Emery anamwona Ozil kama mchezaji ambaye ameshapungukiwa mipango kwenye akili yake na kiwango chake kimeshadumaa, hana tena jipya analoweza kulifanya.

Ozil kwa wiki anapokea mshahara wa Pauni 350,000, hivyo si kitu kinachoweza kuvumiliwa kwa muda mrefu kumlipa mchezaji mshahara mkubwa wakati hachezi. Kutokana na hilo, hakuna ubishi itakapofika mwishoni mwa msimu huu na kama Ozil ataendelea tu kukaa benchi, basi Arsenal itafanya jambo moja kumuuza Mjerumani huyo na kutafuta mchezaji mwingine wa kuziba pengo lake, lakini atakayekuwa ikimlipa mshahara wenye unafuu.

Hawa hapa mastaa wanaofaa kutua Emirates kuchukua mikoba ya Ozil kama ataachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu na vile Kocha Emery anavyoweza kumtumia kila mchezaji kwenye orodha hiyo atakapotua katika kikosi chake.

James Rodriguez –Real Madrid

Kwa sasa, Rodgriguez anacheza kwa mkopo huko Bayern Munich. Chini ya Kocha Nico Kovac mambo yake yamekuwa magumu sana na kumfanya afikirie mpango wa kuachana na timu hiyo. Rodriguez alikuwa panga pangua kwenye kikosi cha Bayern Munich chini ya Kocha Jupp Heyneckes na kuisaidia timu hiyo kubeba ubingwa wa Bundesliga msimu uliopita, lakini tangu timu hiyo iwe chini ya Niko Kovac msimu huu mambo yamekuwa tofauti kabisa.

Mkataba wake wa miaka miwili ya kucheza kwa mkopo huko Bayern Munich utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na hakuna uhakika akirudi Bernabeu atakwenda kupata nafasi ya kucheza, hivyo safari ya kutua kwenye Ligi Kuu England itamhusu kama kutakuwa na timu itakayohitaji huduma yake. Arsenal inaweza kuchangamkia huduma ya kiungo huyo mshambuliaji, anayeweza kumudu vyema kucheza Namba 10.

Kama Arsenal itafanikiwa kumpata Rodriguez, basi atakwenda kuwapa faida ya kucheza fomesheni ya 4-2-3-1, ambapo atacheza katikati kwenye ile safu ya viungo watatu wa ushambuliaji, lakini akisimama nyuma ya mshambuliaji wa kati ili apige zile pasi zake za mwisho matata.

Kai Havertz – Bayer Leverkusen

Bayer Leverkusen imekuwa na historia nzuri kabisa ya kutengeneza viungo matata wenye ufundi, wakifanya hivyo kuanzia kwa Toni Kroos, Michael Ballack na Bernd Schuster, ambao wote walicheza soka la kiwango cha juu sana na kuweka juu majina yao juu wakati walipokuwa kwenye kikosi hicho cha Bundesliga.

Havertz ni kiungo wa miaka ya karibuni aliyeibukia kutoka kwenye akademia ya timu hiyo na hakika ameliweka jina lake kwenye chati cha juu kabisa.

Faida ya kuwa na kiungo huyo kwenye kikosi chako, atakufanya kutokuwa na mashaka katika kuutumia mfumo wa 4-4-2, huku akisimama upande wa kulia, mbele kidogo ya viungo wa kati, lakini nyuma kidogo pia ya washambuliaji wawili wa kati.

Isco – Real Madrid

Kitendo cha Isco kushindwa kupata namba kwenye kikosi cha Real Madrid kwa sasa bila ya shaka kitakuwa kinamshangaza hata shabiki wa kutupwa wa mahasimu wa timu hiyo kwenye La Liga, Barcelona.

Ukweli, Isco ni mmoja kati ya viungo wachezeshaji bora kabisa katika kizazi chake, hivyo kusumbukia namba kwenye kikosi cha Los Blancos, ikiwa ni kipindi kigumu zaidi tangu alipotua kwenye kikosi hicho mwaka 2013. Kocha wa sasa wa Madrid, Santiago Solari amekuwa na upendeleo wa kuwapanga viungo wengine kuliko hata mchezaji huyo jambo linaloonyesha pengine zama zake Isco kuendelea kukipiga kwenye kikosi hicho zimefika tamati.

Arsenal ikimnasa Isco itaweza kutumia fomesheni ya 4-1-2-1-2, ambayo kimsingi ni 4-3-3, lakini Isco atasimama nyuma ya washambuliaji wa wawili wa kati na Xhaka atakuwa kwenye kiungo ya kukaba, akisimama mbele ya mabeki wa kati.

Denis Suarez – Barcelona

Habari kubwa ya usajili wa Arsenal kwenye dirisha hili la Januari ni kumfukuzia staa wa Barcelona, Denis Suarez. Mwanzoni ulikuwa mpango wa kutoa pesa, lakini baadaye, Kocha Emery alikuwa akipiga hesabu za kumsajili kiungo huyo wa pembeni kwa mkopo. Emery anamtaka Denis Suarez kwa sababu anafahamu kiwango chake tangu wakiwa pamoja.

Mwisho wa msimu, Arsenal itampoteza Aaron Ramsey na bila ya shaka itakuwa hivyo hivyo kwa Ozil, hivyo suala la Arsenal kusajili wachezaji wa aina hiyo kama vile Denis Suarez halina kikwazo.

Kama Emery akifanikiwa kumpata Suarez, basi atakuwa na uwezo wa kuchezesha kwenye mfumo wa 4-2-3-1, akicheza kwenye ile safu ya wachezaji watatu, akicheza nyuma ya mshambuliaji wa kati, ambaye kimsingi anapaswa kuwa Lacazette, huku Aubameyang akishambulia akitokea upande wa kulia kwenye huo utatu wa nyuma ya mshambuliaji wa kati.

Nabil Fekir –Olympique Lyon

Kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, Nabil Fekir ilibaki kidogo tu atue Liverpool kabla ya kuripotiwa vipimo vya afya ndivyo vilivyotibua dili hilo. Chelsea pia ilimhitaji kiungo huyo mchezeshaji, lakini nayo ilishindwa kumsajili na akabaki kwenye kikosi chake cha Olympique Lyon.

Lakini, hakuna kificho Fekir atakuwapo sokoni tena kwenye majira haya ya kiangazi kwani mkataba wake utakuwa umebakiza mwaka mmoja tu. Fekir akitua kwenye kikosi cha Arsenal, atatumika kwenye namba 10, akicheza nyuma ya mshambuliaji wa kati kwenye ile fomesheni ya 4-4-2, lakini Emery akilazimika kuwatumia viungo wawili wa kukaba katikati ya uwanja, Granit Xhaka na Lucas Torreira kuweka balansi kwenye kikosi chake.

Yannick Carrasco –Dalian Yifang

Uamuzi wa Yannick Carrasco kutimkia zake kwenye Ligi Kuu China ulikuwa na maana nzuri kwake kutokana na kumwingizia pesa nzuri.

Ripoti zilifichua Man United inahitaji huduma yake, lakini hilo haliwezi kumzuia Kocha wa Arsenal, Unai Emery asifanye mpango wa kunasa huduma ya staa huyo wa Ubelgiji.

Usajili wa Carrasco utamfanya Emery kuwa na uwezo wa kucheza fomesheni ya 4-4-2, ambapo atatumika kama kiungo wa kulia, huku kasi yake ikitajwa kama ni silaha kubwa katika kuwapelekesha puta mabeki wa timu pinzani na kuhakikisha kina Lacazette na Aubameyang wanapata mipira.

Cristian Pavon –Boca Juniors

Januari mwaka jana, Arsenal kwa muda wote wa dirisha la usajili ilihusishwa na mpango wa kumnasa winga huyo wa Boca Juniors, Cristian Pavon baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa uwanjani. Akiwa tayari ameishachezea Argentina ikiwemo fainali za Kombe la Dunia 2018, staa huyo ameonyesha kiwango bora kabisa ambacho hakika kinafaa kabisa kwenye kupata nafasi kwenye kikosi cha timu makini kama Arsenal. Mashabiki wa Arsenal bila ya shaka wataupokea usajili wake kwa furaha na kumsubiri kuona kile atakachokifanya kwenye ligi.

Leon Bailey – Bayer Leverkusen

Kinda mwingine matata kabisa anayetamba huko kwenye Bundesliga.

Leon Bailey kiwango chake anachokionyesha huko Bayer Leverkusen kimezifanya klabu nyingi kubwa kupambana kuhangaikia saini yake kutokana na staili yake ya uchezaji, akitumia kasi na kushambulia bila woga. England ilijaribu kumwita kwenye kikosi chake kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia, lakini mwenyewe alishikilia msimamo wake wa kuitumikia Jamaica kwenye soka la kimataifa.

Wilfried Zaha – Crystal Palace

Kiwango cha Wilfried Zaha kwenye kikosi cha Crystal Palace kimekuwa matata kwelikweli, lakini bahati mbaya kwa Muivory Coast huyo ni kwamba atatumikia ubora wa soka lake akipambana timu isishuke daraja. Aliwahi kwenda Man United, lakini mambo hayakuwa vizuri.

Hata hivyo, inadaiwa kipindi kile Zaha alikuwa mdogo na sasa amepevuka, na ana miaka 26 akijitengenezea hadhi ya winga matata.