Mastaa wa Stars walisikitishwa kutekwa kwa Mo

Muktasari:

Leo asubuhi, MO aliyekuwa akielekea kwenye hotel ya Colosseum, alitekwa na wazungu wawili waliokuwa na gari aina ya suff na kutokomea kusikojulikana

Praia, Cape Verde. MASTAA wa kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania wameonyeshwa kusikitishwa na kitendo cha utekwaji kilichofanywa kwa tajiri wa klabu ya Simba, Mohamed Dewji leo alfajiri.
Thomas Ulimwengu aliongoza kundi la mastaa wa Stars akiomba Mo apatikane akiwa salama huku akiamini kwamba Vyombo vya Dola vya Tanzania vina uwezo mkubwa wa kufanikisha kupatikana kwa Mo ndani ya muda mchache.
“Nadhani Mo atapatikana akiwa salama kwa sababu kwa ninavyofahamu mimi Vyombo vyetu ni makini na vinaweza kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa ndani ya muda mchache tu.” Alisema Ulimwengu ambaye anakipiga katika klabu ya Al Hilal ya Sudan.
Naye nahodha msaidizi wa Stars, Himid Mao amedai kwamba kitendo cha Mo kutekwa ni mwanzo mbaya wa maisha ambayo Watanzania hawakuzoea katika historia yao na akataka waliofanya hivyo wakamatwe.
“Mimi nadhani Mo atapatikana akiwa salama lakini kinachonishangaza ni kwamba hilo ni tukio kubwa la kwanza kufanyika nchini kwa mtu kama Mo. Nadhani kwa sasa hatupo salama na mtu yeyote anaweza kutekwa.” Alisema Himd ambaye staa wa zamani wa Azam.
Abdi Banda anayecheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini ambako kumekuwa na matukio mengi ya utekaji na Ujambazi alitoa rai kwa vyombo vya dola kuanza kujidhatiti na matukio hayo kwa sababu tukio la Mo si la kawaida.
“Inaonekana waliofanya hivyo ni watu waliojiandaa sana. Sio kitu cha kawaida sana lakini Mungu atamsaidia Mo na atapatikana akiwa salama. Kule Afrika Kusini ni kitu cha kawaida lakini kwa Tanzania sio kitu cha kawaida.” Alisema Banda.