Mastaa kupamba onyesho Twanga Pepeta

Muktasari:

Bendi ya muziki wa dansi Twanga Pepeta, inatarajiwa kufanya onyesho maalumu la kutimiza miaka 20 jijini Dar es Salaam.

Wanamuziki 18 wanatarajiwa kupanda jukwaani kutoa burudani katika onyesho hilo lililopangwa kufanyika Oktoba 27.

Dar es Salaam. Bendi ya muziki wa dansi African Stars ‘Twanga Pepeta’  imepanga kufanya onyesho kabambe la kuadhimisha miaka 20 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, kiongozi wa bendi hiyo Luiza Mbutu alisema onyesho hilo litafayika Oktoba 27 na litashirikisha wanamuziki 18.

Mwimbaji huyo alisema onyesho litafanyika viwanja vya Life Park (New World Cinema) na litatumika kutambulisha wanamuziki wapya.

"Sio jambo dogo bendi kufikisha miaka 20, tunahitaji kufanya kitu cha tofauti kwa wapenzi na mashabiki wa Twanga Pepeta," alisema Luiza.

Kiongozi wa wananenguaji wa Twanga Pepeta Hassani Mussa ‘Super Nyamwela’ alisema wamejipanga kutoa burudani ya nguvu katika onyesho hilo.

Twanga Pepeta imewahi kupata mafanikio katika muziki wa dansi baada ya kutamba na albamu mbalimbali zikiwemo Kisa cha Mpemba, Jirani, Chuki Binafsi, Mwana Dar es Salaam na Mtu Pesa.

Baadhi ya wanamuziki hodari waliowahi kutamba na kundi hilo ni Ally Choki, Rogert Hegga, Charles Gabriel ‘Chalz Baba’, Ramadhani Masanja ‘Banzastone’, Hamisi Kayumbu ‘Amigolas’ na Abuu Semhando.