Mastaa hawa wanapaona motoni Simba,Yanga,Azam

Muktasari:

Makala haya yanakuletea wachezaji sita ambao walisajiliwa msimu huu katika dirisha kubwa lakini kufikia sasa wameshindwa kuonyesha makali yao na huenda wakaonyeshwa mlango wa kutokea.

UMEBAKI mwezi mmoja kabla ya dirisha dogo la usajili wa Ligi Kuu Bara kufunguliwa Desemba 16, kipindi ambacho pilika za timu kuongeza wachezaji wapya na kuachana na wale ambao wameshindwa kufanya vizuri huanza.

Wakati raundi 11 za ligi zimeshachezwa, kuna wachezaji wa kigeni katika timu kubwa nchini Simba, Yanga na Azam ambao licha ya usajili wao kuwa wa matumaini ya kuzibeba timu hizo lakini wameshindwa kufanya walichotarajiwa kufikia sasa.

Wachezaji hao wanaonekana kukalia kuti kavu kutokana na kukosa nafasi ya kucheza katika vikosi vya kwanza na wakati mwingine kukosa hata nafasi ya kukaa benchi na hivyo kuachwa tu jukwaani. Haitakuwa jambo la kushangaza ukisikia wamepigwa panga.

Makala haya yanakuletea wachezaji sita ambao walisajiliwa msimu huu katika dirisha kubwa lakini kufikia sasa wameshindwa kuonyesha makali yao na huenda wakaonyeshwa mlango wa kutokea.

WILKER DA SILVA

Straika Mbrazili wa Simba alisajiliwa kwa mbwembwe na kuamsha matumaini makubwa kwa wapenzi wa soka la Tanzania hasa wa timu hiyo wakiamini atakuja kuonyesha samba la Kibrazil.

Hata hivyo, mambo yamekuwa tofauti kwa Da Silva kwani timu ya Simba ikiwa katika maandalizi ya msimu Afrika Kusini mchezaji huyo alipata majeraha ambayo yalimuweka nje hadi msimu wa ligi ulipoanza huku akiwa amekosa mechi nyingi za kimashindano.

Aliporudi na kuanza mazoezi ya nguvu na timu alipata nafasi ya kucheza katika mechi moja ya ligi dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaibata Bukoba, lakini kiwango chake kilionekana kuwa cha kawaida.

Da Silva alicheza mechi za kirafiki dhidi ya Mashujaa, Bandari ya Kenya na zote alishindwa kuonyesha makali na tangu hapo hajacheza tena. Hivi sasa tayari tena ni miongoni mwa wachezaji majeruhi katika kikosi hicho.

Taarifa zilizopo, Simba inawafukuzia nyota wawili wa kigeni na ikiwapata, itamfungulia mlango wa kutokea Mbrazili huyo aliyeshindwa kuleta ushindani dhidi ya straika mwenzake Meddie Kagere, ambaye kufikia sasa ameshafunga mabao nane katika Ligi Kuu Bara.

ISSA BIGIRIMANA

Winga wa Yanga usajili wake ulikuwa na usiri mkubwa kutokana mchezaji huyo kuonekana ametoroka katika klabu yake ya APR ya Rwanda na kuja nchini kufanya mazungumzo ya kimya kimya na kusaini mkataba.

Wapenzi wengi wa Yanga waliamini Bigirimana ni miongoni mwa mawinga wenye kasi na wenye uwezo mkubwa wa kupiga krosi za maana na kutoa pasi za kufunga kwa washambuliaji kutokana na mahitaji ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mwinyi Zahera.

Zahera kabla ya kuanza kufanya usajili msimu huu alieleza wazi anataka winga mwenye kasi katika kushambulia, uwezo wa kupunguza mabeki, kurudi nyuma kusaidia kukaba na kupiga krosi tamu kwa washambuliaji, lakini matumaini hayo mpaka sasa yamekuwa tofauti.

Bigirimana mpaka sasa hajacheza mchezo wowote wa kimashindano tangu ametua Yanga kutokana na hilo ameingia katika orodha ya nyota ambao wamekalia kuti kavu.

MUSTAFA SULEIMAN

Yanga walimsajili kutokea Aigle Noir ya Burundi, wakiamini atakuwa mbadala sahihi wa mabeki wa kati walioondoka katika kikosi hicho, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Andrew Vicent ‘Dante’ ambaye yuko katika mvutano wa kimaslahi na klabu hiyo ya Jangwani.

Mambo yalikuwa tofauti kwa Suleiman kwani licha ya kuonekana alisajiliwa kama beki wa kati, lakini kocha wa timu hiyo Zahera alikuwa akimchezesha kama mlinzi wa kulia kutokana na Paul Godfrey ‘Boxer’ kuumia huku Juma Abdul alikuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza wakati huo.

Suleiman licha ya kusajiliwa kwa matumaini makubwa katika kikosi hicho lakini amekuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza Yanga na huenda kuna baadhi ya watu hata hawafahamu kuhusu uwepo wake.

SELEMANI NDIKUMANA

Msimu wa 2006-07, alisajiliwa na Simba na alionyesha makali yake akiwa na kikosi hicho akicheza mechi 36, na kufunga mabao 19, baada ya hapo aliondoka katika kikosi hicho cha Msimbazi na kwenda kuitumikia timu ya Molde ya nchini Norway.

Miaka 12 baadaye, Azam wamemsajili msimu huu. Hajaonekana kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na nafasi yake katika eneo la ushambuliaji amekuwa akicheza mara kwa mara Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Richard Djodi na Shaban Chilunda.

Mechi ya mwisho kucheza akiwa na kikosi cha Azam ilikuwa ya kirafiki dhidi ya African Lyon, ambayo alianza katika kikosi cha kwanza Oktoba 14, katika pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex na wakati huo amekuwa mchezaji wa kuishia benchi au jukwaani kabisa.

MAYBIN KALENGO

Tangu amesajiliwa katika kikosi cha Yanga msimu huu hakuwa anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara na katika eneo la ushambuliaji ambalo anacheza walikuwa wakipewa nafasi, Mnamibia Sadney Urikhob, Mcongo David Molinga na Mganda Juma Balinya.

Kalengo alicheza mechi chache za kimashindano na hata kiwango chake kilionekana kuwa cha kawaida tangu aliposajiliwa kutokea Zesco United ya Zambia.

Yanga wakiwa wanajiandaa kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika mzunguko wa kwanza dhidi ya Pyramids wakiwa kambini Mwanza Kalengo alivunjaka mguu na hadi sasa yupo nje ya uwanja akiendelea kupata matibabu.

EMMANUEL MVUYEKULE

Alisajiliwa na Azam akitokea KMC. Msimu uliopita alikuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza na alifunga mabao katika mechi muhimu akiwa nguzo kwenye safu ya ushambuliaji.

Baada ya kutua Azam, mwanzoni mwa msimu chini ya kocha Ettiene Ndayiragije ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Taifa Stars, alikuwa akipata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza lakini tangu kuondoka kwa Ndayiragije amekuwa si mchezaji tena wa kuanza.

Mvuyekule mabadiliko ya makocha katika kikosi cha Azam yanaweza kumuathiri kwani Ndayiragije alikuwa akimfahamu tangu wakiwa wote katika kikosi cha Mbao misimu mitatu iliyopita.

MOGELLA ATOA ANGALIZO

Mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella, alisema wachezaji wengi wa kigeni ambao wanasajiliwa nchini si kwamba wanafuatiliwa vya kutosha ndio maana kuna wengine licha ya kusajiliwa kwa mbwembwe na matumaini makubwa lakini wanashindwa kufanya vizuri.

Mogella alisema kila mchezaji wa kigeni kabla ya kusajiliwa anatakiwa kufuatiliwa vya kutosha na si kuangalia video zake mtandaoni bali kuona akiwa anacheza aina za mechi mbalimbali na hapo ndio unaweza kujiridhisha kwamba anafaa kucheza katika timu yako.

“Lakini pamoja na kuwafuatilia, hawa wachezaji wa kigeni wanatakiwa kuwekewa vipengele vya kuwabana katika mikataba yao kama wanashindwa kufanya vizuri au kufikisha idadi fulani ya mabao kama mshambuliaji anaweza kukatwa mshahara au mkataba wake kuvunjwa bila malipo,” alisema.

“Kama tukiwafuatilia vya kutosha na kuwapa mikataba ambayo inawabana na kuwaondolea mazingira ya raha muda wote, watakuwa wanaona uchungu na watafanya kazi iliyowaleta ipasavyo. Nadhani kwa aina hii ya mikataba tutakuwa tunapata wachezaji wazuri,” alisema nyota huyo wa zamani wa Taifa Stars.