Mastaa hawa kutoka Yanga watasumbua sana Azam FC

Thursday November 8 2018

 

By Doris Maliyaga

Dar es Salaam. Mzambia Obrey Chirwa ametua Azam FC na sasa atafanya kazi na pacha wake, Mzimbabwe Donaldo Ngoma chini ya Kocha Hans Pluijm 'Babu'.
Pluijm kocha wa zamani wa Yanga na Singida United ndiye amekamilisha usajili wa Chirwa ambaye anamjua vizuri baada ya kumfundisha ndani ya kikosi cha watoto hao wa Jangwani ili kutengeneza kombinesheni nzuri kwenye safu ya ushambuliaji ya Azam.
Chirwa na Ngoma mbali ya kuwa pamoja Yanga, waliichezea Platinumz FC ya Zimbabwe pamoja hivyo wanajuana vizuri.
Kimwonekano Chirwa ana mwili wa kawaida, ana uwezo wa kuchezea mpira (ball control), kufunga mabao ya mashuti na kichwa, ana kasi na ni mzuri zaidi anaposhambulia akitokea pembeni kwenye namba 10, 11 au 7.
Wakati, Ngoma ambaye ni mrefu wa umbo ni tishio zaidi anapocheza mshambuliaji wa mwisho yaani namba 9, kutokana na sifa yake ya upachikaji mabao ya aina yote na huwa hakosei.
Kutokana na aina yao ya uchezaji na uelewano wao uwanjani,  wataifanya kazi ya Pluijm ambaye kikosi chake kinaongoza msimamo wa ligi na pointi 30, huku timu za Simba na Yanga zikifata kila moja ikiwa na pointi 26,  kuwa rahisi.
Kabla ya kutua Azam, Chirwa na Ngoma walicheza pamoja ndani ya kikosi cha Yanga ilipokuwa inafundishwa na Pluijm misimu miwili iliyopita kabla ya kocha huyo kutimkia Singida United na baadaye Azam.
Wachezaji hao pia walifata kuondoka, Ngoma alijiunga na Azam FC na Chirwa alikwenda Misri katika Klabu ya Nogoom El Mostakbal Football Club.
Chirwa na Ngoma walikuwa na maelewano mazuri ya kiuchezaji ndani ya kikosi cha Yanga na wakaisaidia msimu huo wa mwaka juzi wakamaliza na ubingwa. Katika msimu uliopita, walishindwa kutetea taji lao na kutokana na kile kilichodaiwa ni ukata.

Advertisement