Mastaa ghali mwaka huu, Chelsea wanne

LONDON, ENGLAND. CHELSEA imeingiza wachezaji wanne kwenye orodha ya kikosi cha kwanza cha mastaa ghali zaidi waliosajiliwa katika dirisha hili la uhamisho wa majira kiangazi huko Ulaya.

The Blues ilitumia zaidi ya Pauni 230 milioni wakati, Frank Lampard alipohakikisha anatengeneza kikosi matata baada ya kutumikia adhabu ya kusajili kwa mwaka mzima.

Na sasa, wachezaji wanne wameingia kwenye kikosi hicho cha mastaa waliosajiliwa kwenye pesa nyingi katika dirisha la majira ya kiangazi ya mwaka huu. Licha ya kuwapo kwa janga la corona, klabu za England, zimetumia zaidi ya Pauni 1 bilioni kunasa vipaji vipya.

Baada ya makosa mengi ya kipa ghali duniani, Kepa Arrizabalaga kocha Lampard aliamua kumnasa huduma ya kipa mwingine, Edouard Mendy ambaye ada yake ya Pauni 24 milioni ni ghali zaidi kwa makipa walionaswa kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kwenye kikosi hiki, Mendy anasimama golini, huku mabeki wake ni Ben Chilwell, aliyenaswa kwa Pauni 50 milioni, Nathan Ake, aliyesajiliwa kwa Pauni 41 milioni na Ruben Dias, aliyenyakuliwa kwa Pauni 64.5 milioni. Kwenye sehemu ya kiungo yupo Thomas Partey, aliyenaswa kwa zaidi ya Pauni 45 milioni, Arthur kwa Pauni 75 milioni na Miralem Pjanic kwa Pauni 55 milioni, huku wawili hao wakibadilishana klabu.

Namba 10 ni Kai Havertz aliyesajiliwa kwa Pauni 70 milioni, huku washambuliaji watatu ni Timo Werner, aliyenaswa na Pauni 48 milioni, Leroy Sane kwa Pauni 55 milioni na Victor Osimhen, ambaye huduma yake imegharimu Pauni 63 milioni na wanaamini sasa watakuwa na kikosi imara.