Mastaa Yanga waoga noti

Tuesday February 19 2019

Kocha wa Yanga ,Mwinyi Zahera akitoa maelekezo

Kocha wa Yanga ,Mwinyi Zahera akitoa maelekezo kwa wachezajiwake kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza,jana ikiwa ni maandalizi ya kuwavaa wenyeji,Mbao FC.Picha na Michael Jamson 

By Khatimu Naheka

SIMBA imeondoka na pointi tatu katika mchezo dhidi ya Yanga, lakini vigogo wa klabu hiyo hawakuwaacha patupu vijana wao wakawajaza mamilioni kurudisha morali ikikutana na Mbao FC kesho Jumatano.

Baada ya mchezo dhidi ya Simba wachezaji wa Yanga walijikuta wakipokea Sh 18 milioni ikiwa ni mkakati wa kurudisha morali kuelekea mchezo dhidi ya Mbao.

Kiasi hicho kilitoka katika majumuisho ya makusanyo ya fedha kutoka kwa wabunge mashabiki wa klabu hiyo pamoja na baadhi ya vigogo wake ambapo, baadaye waliongeza Sh 2 milioni.

Mbali na hao pia kundi la mitandao ya kijamii ya ‘Whatsup’ kupitia viongozi wao nao walikuwa na michango yao katika fedha hizo.

Kiongozi wa wabunge aliyewasilisha fedha hizo Hawa Ghasia, ambaye ni Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM) aliwashukuru wachezaji hao kwa kujituma ingawa matokeo hayakuwa mazuri.

Ghasia alisema bado wanaimani na timu yao na kwamba fedha hizo ziwe morali kubwa kuhakikisha wanashinda mechi zao zijazo kuanzia ya kesho Jumatano pale CCM Kirumba dhidi ya timu ngumu inayowasumbua Mbao wakiwa nyumbani.

“Tunawashukuru wote waliokusanya fedha hizi, lakini niwaombe wachezaji tuna imani na timu kwamba licha ya kupoteza mnaweza kufanya vizuri zaidi mkapambane bila kujali matokeo yaliyopita,” alisema Ghasia katika taarifa yake.

Advertisement