Mastaa Yanga wakiona Moro

Friday July 19 2019

 

By Mwandishi wetu, Morogoro

KAMBI ya Yanga mjini hapa imezidi kunoga baada ya Mwenyekiti wa klabu hiyo Dk Mshindo Msolla jana kuvamia mazoezini ili kujionea tizo, lakini unaambiwa kile kinachoendelea kwa sasa chini ya Kocha Noel Mwandila kimewatoa jasho nyota hao.

Issa Birigimana aliyetua akitokea APR ya Rwanda, amekiri mazoezi yanayoendelea ndani ya kambi hiyo ya maandalizi ya msimu mpya sio ya kitoto, ila akidai ugumu wanaoupata sasa utawarahisishia kazi kwenye mechi zao wakati wakatakapoliamsha.

Straika huyo alisema dozi wanayopewa kambini, sio ya kawaida na ubora wao msimu ujao utatengenezwa na kambi hiyo.

Bigirimana alisema mazoezi yao chini ya makocha Noel Mwandila na Peter Manyika kama ni mchezaji legelege na asiye na malengo unaweza kuishia njiani, lakini kwa wanaojielewa ni hatua nzuri kwani wanazidi kukomaa.

“Haya mazoezi ni makali sana, lakini yana faida kubwa kwa mustakabali wa kikosi chetu kwa baadaye kwa vile tunawiva kisawasawa,” alisema Bigirimana na kuongeza;

“Sijakutana na mazoezi ya aina hii, hii kwa mara ya kwanza kuyafanya na inaonyesha msimu ujao tukifankiwa hapa hakuna atakayetusumbua iwe Ligi Kuu ama katika michuano ya kimataifa.”

Advertisement

Alisema anajua siri moja ya soka la Tanzania linahitaji nguvu na hana wasiwasi na hilo yuko tayari kukutana na beki yoyote.

ATUNISHA KIFUA

Akizungumzia kitendo cha kupewa jezi namba 10 iliyoachwa na nahodha wa zamani wa klabu hiyo, Ibrahim Ajibu aliyerejea Simba, Bigirimana alisema anamjua fundi huyo lakini hana wasiwasi katika uzito wa jezi hiyo kupitia kazi yake ya msimu uliopita.

Bigirimana alisema mpaka Yanga imemsajili imemwamini uwezo wake na atapambana kuhakikisha anaitendea haki jezi ya klabu hiyo.

“Yanga ina timu nzuri ambayo inakupa changamoto kama mchezaji kujituma mwenyewe ushindani utakuwa mkubwa kila mchezaji anajua hapa nina imani tutafanya vyema.”

Bigirimana ni moja ya washambuliaji watano waliotua Jangwani kati ya nyota 13 wapya waliosajiliwa na Yanga kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na michuano mingine watakayoshiriki.

Mastraika wengine waliotua nao ni Mnamibia Sadney Urikhob, Mzambia Maybin Kalengo, Mnyarwanda Patrick Sibomana na Juma Balinya kutoka Uganda.

Advertisement