Mastaa Ulaya wana hatari ya majeraha

Muktasari:

  • Moja ya mechi iliyovutia ni ile iliyochezwa Jumanne ikishuhudia Croatia iliyofika fainali katika michuano ya Kombe la Dunia ikipata kipigo cha mabao 6-0 kutoka kwa Hispania.

Bara la Ulaya limeibuka na mashindano mapya yajulikanayo kama Europa National Leugue yaliyoanza kutimua vumbi tangu Jumamosi yakishirikisha nchi za bara hilo.

Moja ya mechi iliyovutia ni ile iliyochezwa Jumanne ikishuhudia Croatia iliyofika fainali katika michuano ya Kombe la Dunia ikipata kipigo cha mabao 6-0 kutoka kwa Hispania.

Ni ukweli mashindano haya yatatupa burudani Lakini kwa jicho la tatu la kitabibu linaona kama hakutakuwa na namna ya kukwepa ongezeko la majeraha ya miguu kwa wachezaji wa Ulaya.

Hii ni kutokana na wachezaji hao ambao baadhi wametoka kushiriki Kombe la Dunia mwaka huu, kushiriki pia mashindano hayo na huku wakikabiliwa na mashindano ya ndani ya klabu.

Mfano mchezaji wa Uingereza katika klabu yake ipo Ligi Kuu (EPL), Kombe la FA, Carling Cup na UEFA kwa klabu iliyokuwa katika nne bora.

Hivyo basi kwa mwaka huu pekee mchezaji mmoja anashiriki mashindano makubwa karibu matano yenye ushindani mkubwa na hivyo kumweka katika hatari ya kupata majeraha.

Wiki iliyopita nilieleza madhara yanayowapata wachezaji baada ya kutumika sana, leo tutaona katika soka la nchi zilizopiga hatua wanavyoweza kukabiliana na majeraha ya misuli.

Majeraha ya misuli ya miguuni ni kati ya majeraha yanayowasumbua wachezaji duniani. Hatua zifuatazo hutumika kuwapa nafuu na kusaidia kupona majeraha ya misuli ya miguu.

Kupunguza maumivu ya awali na uvimbe

Hatua za awali kabla ya kufika katika huduma za afya hupata huduma ya kwanza alipopatia jeraha ikiwamo eneo lenye jeraha kupuliziwa dawa ya maumivu na hulindwa ili asijijeruhi zaidi.

Hupewa usaidizi na kutolewa mchezoni na kupumzishwa, huwekewa barafu, hufungwa kwa bendeji yenye kuvutika na mguu hunyanyuliwa kuzidi kifua.

Katika hatua za mwanzoni majeruhi anaweza kutembea kwa kuchechemea, pale anapopumzishwa husaidia kuzuia shinikizo la uzito wa mwili katika mguu huo hivyo kuepusha madhara zaidi. Uvikaji wa vifaa tiba maalumu ikiwamo kiatu au nusu P.O.P, vibana misuli, vidhibiti vya goti, kutembelea kwa kiti au gongo maalumu ni moja ya mbinu za kuutuliza mguu ili asijijeruhi.

Ili kupungua uvimbe na maumivu barafu iliyowekwa katika mfuko wa plastiki huwekwa katika jeraha kwa dakika 10-20 kila baada ya saa 2-4, huwekewa mara tu wanapohisi joto linapanda katika jeraha.

Dawa za maumivu zakumeza au kuchoma hazitumiki mpaka baada ya masaa 48-72 isipokuwa Acetaminophen (Paracetamol), zingine zikitumika zinaweza kuchangia damu kuvuja katika jeraha .

Kadiri unavyoimarisha ukandamizaji kwa kutumia “clip bundage” husaidia kutoa nafuu kwa misuli iliyojeruhiwa, pia kuzuia damu kuvuja. Kuunyanyua mguu wenye jeraha kuzidi kifua majeruhi akiwa amelala chali, husaidia kurudisha damu kutoka eneo la mguu haraka hivyo kupunguza uvimbe mapema.

Kurudishia utendaji kazi wa misuli kama awali

Kama hatua ya kwanza itaenda vizuri kama inavyotakiwa ubora na ufanisi wa misuli hiyo huweza kurudi kama ilivyokuwa awali.

Ukarabati wa jeraha na kujiunga huchukua takribani wiki sita, wakati huu lengo ni kusaidia gamba la jeraha lilojiunda kuwa imara ili kusiwepo na kujirudia kwa majeraha.

Usingaji (massage), unyooshaji misuli, uimarishaji mishipa ya fahamu na damu kwa mazoezi mepesi ya viungo hufanywa ili kuliimarisha jeraha lililounga.

Kuweza kutembea bila maumivu wala kuchechemea na kuweza kufanya matendo mbalimbali ikiwamo mazoezi mepesi na kuinyoosha misuli ya mguu pasipo kikwazo ni ishara kuwa mchezaji amepona.

Kurudishia misuli ya mguu uwezo wa kunyanyua mwili

Ukakamavu na nguvu za misuli ya miguu huimarishwa taratibu kwa kuweka shinikizo la uzito kidogo mpaka hapo baadaye huongezewa kwa hatua.

Hii ina maana kama majeruhi alikuwa anatumia kifaa au alikuwa hautumii mguu kuukanyagia moja kwa moja hutakiwa kuacha na kuanza kutembea bila usaidizi wa chochote.

Baada ya wiki 1-2 huanza kutembea na kujinyanyua taratibu na kuuvuta mwili, baadaye huanza kukimbia kidogo kidogo na kurukaruka kiasi.

Majeruhi kuruka na kukimbia kwa nguvu ni wazi eneo hilo linapata shinikizo kubwa la uzito wa mwili hivyo ni ishara amepona na tayari kuanza programu ya mazoezi ya viungo na mafunzo.

Kurudishia uwezo wa misuli kudhibiti mijongeo

Misuli ya miguu ndiyo yenye kazi ya kafanya matendo muhimu ikiwamo kunyanyuka, kutembea, kukimbia, kuruka na kukudhibiti kudondoka au kukuvuta chini.

Hatari ya kujitonesa kwa misuli na kuchanika tena hutokea wakati wa unyooshaji misuli, ili kuepusha hali hii walimu wa mazoezi ya viungo hutoa muongozo wakati wa programa ya mazoezi ya viungo.

Miongozo hiyo humwezesha mchezaji kuhimili kujivuta chini kama vile kuchuchumaa, kupiga msamba, kukaa na kuruka kichura pasipo kujijeruhi na haya yanafanyika tu endapo hali ya jeraha itaruhusu.

Kudhibiti kujijeruhi wakati wa mazoezi

Mijongeo au matendo hayo ni pamoja na kuiwezesha misuli kuweza kukunjuka na kujikunja ili kuweza kukimbia kasi kwa umakini na ufanisi mkubwa.

Majeraha ya misuli ya miguu hujitokeza mara kwa mara panapokuwa na shughuli zinazohitaji kukimbia kasi hivyo kusababisha msukumo mkubwa mwilini hasa wakati wa kujikunja na kujikunjua kwa misuli.

Ili kuzuia kujirudia kwa majeraha wataalam wa viungo hutoa mwongozo maalum wa mazoezi na mbinu ili kujenga uwezo wa juu kama livyokuwa hapo awali kabla ya majeraha.

Kwa kawaida hatua hii itategemea na nafasi anayochezea mchezaji na kasi unayohitajika kuwa nayo, atapewa mazoezi na mafunzo ili kumwandaa na mazoezi mepesi.

Majaribio na kurudi rasmi kucheza

Baada ya madaktari kujiridhisha kuwa mchezaji amepona na yuko imara ndipo majaribio ya kiuchezaji huruhusiwa kufanyika.

Hujaribiwa kwa mazoezi maalum ikiwamo kuchezeshwa timu ya vijana au timu B na akifaulu hurudishwa rasmi kikosi cha kwanza. Anapofikia hatua hii hawamchezeshi dakika zote 90, anaweza kuingizwa kama mchezaji wa akiba dakika za mwishoni. Lengo la kufanya hivi ni kumlinda usipate majeraha mapema.

Wataalam wa mazoezi viungo huendelea kumfuatilia majeruhi na mwishowe kocha na benchi la ufundi huwatathimini kiwango cha uchezaji kabla na baada ya majeraha, je kimepanda au kimeshuka?

Pamoja na mbinu hizi majeraha ya misuli kwa wanasoka hayakwepeki hata kama mchezaji akicheza mashindano machache, tusubiri kuona mashindano haya Mapya ya ulaya yataleta matokeo gani.