Mastaa Simba wabadili gia

Sunday October 18 2020
mastaa simba pic

MASTAA wa zamani wa Simba wanaamini kwamba timu hiyo msimu huu inarejea na maajabu yao kimataifa, lakini wakawasisitiza wenzao wa sasa lazima wabadili gia na kukaza zaidi ya wanavyofanya, na wala matokeo ya ndani yasiwavimbishe vichwa.

Wachezaji hao ambao wamewahi kukipiga Simba kwa mafanikio katika nyakati tofauti wanadhani mastaa wa sasa na viongozi wanapaswa kupigia hesabu kwanza makundi ya Klabu Bingwa Afrika halafu robo waingie na hesabu tofauti.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), ratiba kamili itatangazwa muda wowote kuanzia wiki ijayo lakini mechi za mtoano za ligi hiyo zitaanza Novemba 27-29, huku marudiano yakiwa Desemba 4-6. Raundi ya kwanza inaanza Desemba 22-23 na marudiano Januari 5-6, mwakani. Hatua ya makundi itaanza Februari 13-14 na robo fainali itapigwa Mei.

Kiungo mpaka rangi wa zamani Simba, Shekhan Rashid alisema: “Ukiangalia kwa sasa kwa timu za Tanzania, Simba ina kikosi kizuri, muhimu ni wachezaji wajiongeze kidogo ili waweze kurudia rekodi ya mwaka jana na hata kuivuka kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Lakini naamini kabisa inawezekana.

“Licha ya kwamba baadhi wanaweza wasiipe sana nafasi kwa madai wakati mwingine hawachezi vizuri kwenye ligi, lakini lazima wajue mpira ndio uko hivyo kuna wakati mnaweza kushinda bila kutandaza soka safi ambalo wengi wangelifurahia.”

Aliongeza kuwa, “tatizo kubwa walilonalo Simba ni uzuiaji mbovu wa mabeki, wanajisahau sana, hivyo wanachotakiwa kufanya ni kocha kuendelea kuwatumia Pascal Wawa na Joash Onyango ili waendelee kuzoeana kwani ni mabeki wazuri lakini kuanzia eneo la kiungo kwenda mbele hakuna tatizo.”

Advertisement

Naye kiungo Amri Kiemba alisema: “Simba imesajili vizuri kwani kwa ligi ya ndani wako vizuri na wanaweza kutwaa ubingwa kama walivyofanya msimu uliopita licha ya kwamba kuna upinzani mkubwa.

“Kwa Ligi ya Mabingwa wanatakiwa kujiongeza kidogo ingawa naamini wana uwezo wa kufika hatua ya makundi na kama watapita zaidi ya hapo, basi inakuwa kama bonasi kwao.

“Muhimu ni kujijengea mazingira ya kuhakikisha kuwa kutinga hatua ya makundi inakuwa sehemu yao na sio msimu huu mnafika huko, misimu mingine mitatu hampo.”

Alisisitiza kuwa, “uzuri wa sasa hivi mechi mbili tu unaweza kufika hatua ya makundi tena unaweza ukafika hatua hiyo bila kukutana na zile timu miamba ya Afrika, hivyo muhimu ni wachezaji wao kujituma kwani naamini wana kikosi chenye wachezaji bora ambao kama wakipandisha soksi kidogo watafanya makubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.”

Winga wa zamani wa Yanga na Simba, Thomas Kipese alisema: “Wana kikosi kizuri sana ambacho kinaweza kumpiga yeyote hata Mwarabu, kama wachezaji wakiamua kucheza kwa ubora wao. Naamini kama wachezaji wote wataonyesha viwango vikubwa hata fainali Simba wanafika safari hii.”

Advertisement