Mastaa Mbao FC waanza kunogewa

Muktasari:

Nahodha wa Mbao, Said Khamis alisema kwa sasa matokeo waliyonayo si mabaya wala mazuri, hivyo wanapaswa kuwa makini kuipigania timu ili kuepuka kushuka daraja.

MATOKEO mazuri waliyopata kwenye mechi zao za karibuni, yamewapa mzuka nyota wa Mbao FC waliodai kuwa, bado wana kazi ngumu kuhakikisha timu hiyo inamaliza ligi katika nafasi nzuri kutokana na vita ya kutoshuka daraja kuwa ngumu.

Mbao wanaoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa nne wana pointi 17 katika nafasi ya 10 baada ya kucheza mechi 13 na sasa wanajiandaa na mechi dhidi ya Lipuli FC itakayopigwa Desemba 29.

Hata hivyo, timu hiyo imetoa siku 10 kwa nyota wake kupumzika kabla ya kuendelea na mazoezi kwa ajili ya mwendelezo wa Ligi hiyo kuhakikisha wanafikia malengo.

Nahodha wa Mbao, Said Khamis alisema kwa sasa matokeo waliyonayo si mabaya wala mazuri, hivyo wanapaswa kuwa makini kuipigania timu ili kuepuka kushuka daraja.

“Vita ya pointi tatu ni kali, timu zinapambana bila kujali nyumbani na ugenini kusaka ushindi, hivyo nasi tumeshagundua namna ya kusaka matokeo mazuri,” alisema.

Kwa upande wake, straika Wazir Junior alisema wanachoangalia ni matokeo ya timu kwanza na mengine baadaye huku akiweka wazi kuwa lazima Mbao ibaki salama kwenye ligi.

“Lazima tupambane kila mechi kusaka ushindi na kinachotupa nguvu ni muunganiko wa timu kila mmoja anajituma,” alisema.