Mastaa Manchester United wamtaja kocha anayefaa

Muktasari:

Kutokana na hilo kuna masupastaa saba wa zamani wa Man United juu ya mtazamo wao wa kocha wa kudumu wa kuinoa timu hiyo kama wanadhani ni nani anafaa, Pochettino au Solskjaer na haya ndiyo yaliyoonekana kuwa ni machaguo na maoni yao juu ya kocha mpya wa wababe hao wa Old Trafford.

MANCHESTER, ENGLANG. ILE fungate ya kocha Ole Gunnar Solskjaer huko klabuni Manchester United imefika kikomo baada ya usiku wa juzi Jumanne kukumbana na kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Paris Saint-Germain kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kipigo hicho kutoka kwa mabingwa hao wa Ufaransa kimeonyesha wazi kiwango cha Man United kilivyo na uwezo wa kocha Ole Gunnar Solskjaer na kuona kama kweli anafiti kuvaa buti za Jose Mourinho za kuwa kocha wa kudumu katika kikosi hicho chenye maskani yake Old Trafford.

Wakati Solskjaer akidaiwa kwamba huenda akapewa kazi ya kudumu kutokana na bodi ya Man United kufurahishwa na uwezo wake, lakini kuna kocha wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino anahusishwa na kibarua hicho cha kudumu cha kuinoa Man United.

Kutokana na hilo kuna masupastaa saba wa zamani wa Man United juu ya mtazamo wao wa kocha wa kudumu wa kuinoa timu hiyo kama wanadhani ni nani anafaa, Pochettino au Solskjaer na haya ndiyo yaliyoonekana kuwa ni machaguo na maoni yao juu ya kocha mpya wa wababe hao wa Old Trafford.

1.Wayne Rooney - Pochettino

Kinara wa mabao wa muda wote wa Manchester United chaguo lake la kocha wa kudumu kwenye kikosi hicho kuwa ni Mauricio Pochettino, anayeinoa Tottenham Hotspur kwa sasa. Sawa, Rooney kwa sasa anavutiwa na kiwango cha Ole Gunnar Solskjaer, lakini bado anaamini Pochettino atakuwa chaguo sahihi na kuifikisha mbali zaidi timu hiyo. Rooney hatakuwa kwenye machungu sana kama Solskjaer atapewa kazi ya kudumu, lakini chaguo lake limekuwa wazi.

2.Ryan Giggs - hajui

Gwiji wa Wales, Ryan Giggs ameamua kuweka siasa kwenye suala la kocha mpya wa kudumu kwenye kikosi cha Manchester United.

Kibarua hicho kwa sasa kipo chini ya Solskjaer kwa muda, lakini Pochettino naye anatajwa kwenye kupewa kazi kurithi mikoba ya Mourinho. Giggs alipoulizwa anadhani ni kocha yupi hapo anafaa kupewa, Giggs hakutaka kumtaja yeyote si Pochettino wala Solskjaer.

3.Gary Neville - Pochettino

Beki na nahodha wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, mtazamo wake kwenye suala la kumpata kocha mkuu wa timu hiyo kwamba kazi hiyo apewe Mauricio Pochettino arithi mikoba ya Jose Mourinho.

Kikosi hicho kwa sasa kinanolewa na Solskjaer kwa muda na mwisho wa msimu itafahamika kama kibarua hicho kitakuwa cha kudumu au mzigo utakwenda kwa Pochettino kama anavyotaka Neville.

4.Rio Ferdinand -sio Solskjaer

Beki wa kati wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand aliwahi kukiri huko nyuma kwamba hafurahishwi na uamuzi wa kumpa kazi kocha Solskjaer, licha ya kukubali kwamba amevutiwa na mwanzo mzuri katika kikosi hicho. Ferdinand alizungumzia kipigo ilichokutana nacho Man United kwa PSG ni somo ambalo amepewa Ole kujielewa kuhusu kikosi chake alichokuwa nacho licha ya kwamba kwa sasa ajira yake inatambulika kuwa ni ya muda tu.

5.Dimitar Berbatov - Solskjaer

Straika wa zamani wa Manchester United, Dimitar Berbatov amevutiwa na kazi anayofanya Solskjear kwenye kikosi hicho na kuamini kwamba anastahili kupewa kibarua cha kudumu kwenye kikosi hicho cha Old Trafford. Katika kumtaka Solskjaer abaki Man United, Berbatov amemtaka Mauricio Pochettino abaki Tottenham Hotspur, asiondoke. Makocha hao wawili ndiop ambao wanaibua mjadala katika kibarua hicho cha kuinoa Man United.

6.Paul Ince- sio Solskjaer

Kiungo mkorofi Paul Ince hajawahi kuvutiwa kabisa na Ole Gunnar Solskjaer licha ya mwanzo mzuri wa kocha huyo wa muda kwenye kikosi hicho.

Solskjaer hakuwa amepoteza mechi yoyote hadi hapo usiku wa juzi Jumanne alipochapwa 2-0 na Paris Saint-Germain kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya huko Old Trafford. Ince anadai kwamba Man United inapaswa kuajiri kocha mwenye uzoefu na si Solskjaer.

7.Wes Brown - Solskjaer

Beki wa zamani wa Manchester United, Wes Brown yeye ameonekana kuwa yupo kwenye kambi ya Ole Gunnar Solskjaer akiunga mkono mchakato wote wa kumfanya fowadi huyo wa zamani wa Old Trafford kupewa kibarua cha kudumu cha kuinoa timu hiyo.

Usiku wa juzi Jumanne, Solskjaer alikutana na kipondo cha kwanza tangu achukue mikoba ya kuinoa timu kutoka kwenye mikono ya Jose Mourinho.

Brown anataka Solskjaer apewe timu moja kwa moja.