Mastaa Bongo wafunguka Samatta kutua Aston Villa

Muktasari:

Samatta, 27, atakuwa mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kucheza Ligi Kuu England.

MASTAA mbalimbali wa Kitanzania, wamemtakia kila la kheri nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye yuko mbioni kukamilisha usajili wake wa kujiunga na Aston Villa ya Ligi Kuu England.
Saimon Msuva, ambaye anaichezea Difaa El Jadida ya Ligi Kuu Morocco, alisema Samatta ameendelea kuwa mfano kwa wachezaji wa Kitanzania hivyo, kutua kwake England ni ishara tosha ya kuzidi kufungua milango kwa Watanzania kucheza ligi hiyo kubwa duniani.
"Tangu tukiwa wadogo tumekuwa wafuatiliaji wazuri wa EPL. Kupata nafasi ya kucheza ligi hiyo sio jambo jepesi, anastahili pongezi na kwa kweli Samatta ni mwanzo kuna kundi lingine la wachezaji kutoka Tanzania linakuja," alisema  Msuva.
Msuva, ambaye hivi karibuni alikuwa akihusishwa kujiunga na Benfica ya Ureno, aliongeza kwa kusema: "Sina shaka na uwezo wa Samatta, haitokuwa ajabu akiendelea kufanya vizuri kama ilivyokuwa Ubelgiji."
Eliuter Mpepo ambaye anaichezea CD Costa Do Sol ya Msumbiji, alisema, "Siku zote Mungu hamtupi mtu mwenye dhamira ya kweli, alionyesha Samatta na hatimaye milango ya kheri imemfungukia. Hongera kwake."
Adi Yussuf, ambaye anaichezea Boreham Wood kwa mkopo akitokea Blackpool ya Daraja la Pili England, alisema wataendeleza kwa pamoja usemi wao wa haina kufeli ambao, wamekuwa wakipenda kuutumia.
"Nimefurahishwa na ujeo wake. Atafurahia maisha ya England na ushindani wa ligi, niliwahi kumshawishi na kutaniana naye kuwa umefika muda wa kuja England, alikuwa akicheka na kusema tusubiri muda sahihi," alisema Adi.
Upande wake aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Ammy Ninje ambaye kwa sasa yupo England, alisema Samatta ana ubora wa kumudu mikiki ya ligi hiyo.
"Alionyesha katika mchezo dhidi ya Liverpool tena katika mashindano makubwa ya Ligi ya Mabingwa, namwona kama mkombozi wa Aston Villa, anaweza kuchangia kwa timu hiyo isishuke daraja," alisema Ninje mwenye taaluma ya ukocha.