Mastaa Bayern wapigwa mkwara

Muktasari:

Julai mosi  2019, Flick alianza kuitumikia  Bayern Munich  akiwa kama kocha msaidizi chini ya  Niko Kovač ambaye baada ya kufutwa kazi   akachukua mikoba yake kwa muda kabla ya Aprili mwaka huu kupewa mkataba wa kukiongoza kikosi hicho hadi   2023.

Munich, Ujeruman. Kocha wa Bayern Munich, Hans Flick amewaambia nyota wake  kwamba hawastahili kubweteka  baada ya kuifunga  Borussia Dortmund na kuhisi wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ujerumani msimu huu.

Bayern Munich wanaongoza msimamo wa Ligi hiyo ambayo ni maarufu kama Bundesliga kwa tofauti ya pointi saba mbele ya Dortmund huku ikiwa imesalia michezo sita kabla ya msimu kumalizika.

Flick  alisema hayo, ikiwa ni siku moja kabla ya mchezo dhidi ya Fortuna Dusseldorf ambao unatarajiwa kuchezwa leo, " Dusseldorf sio rahisi kucheza dhidi yao. Tunapaswa kucheza kwa kujituma kama ambavyo ilikuwa katika michezo yetu iliyopita."

Timu nyingi zimekuwa katika wakati mgumu kuhakikisha wanatumia vyema kucheza kwao nyumbani tangu kurejea kwa Ligi hiyo huku milango kwa mshabiki ikiwa imefungwa lakini wikiendi iliyopita Bayern ilitoa dozi ya mabao 5-2 dhidi ya Eintracht Frankfurt 5-2.

Baadaye kati kati ya wiki,  Joshua Kimmich akaifanya miamba hiyo ya soka la Ujeruman kuondoka na pointi tatu kwenye uwanja wa Signal Iduna Park, na Flick  anahitaji kuona wachezaji wake wakiendelea kufanya zaidi.

Fortuna Dusseldorf ambao ni wapinzani wa Bayern Munich  katika mchezo wa leo ambao utachezwa saa moja jioni, wapo katika hatari ya kushuka daraja hivyo mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani wa aina yake.

Hata hivyo Dusseldorf, wanaonekana kutokuwa na rekodi nzuri mbele ya Bayern, tangu mwaka 1992 hadi leo hawajawahi kuibuka na ishindi katika mchezo hata mmoja.