Mastaa Azam wanaota medali tu

WACHEZAJI wapya wa Azam FC, Awesu Awesu na Ayubu Lyanga wanatamani kuvaa medali msimu huu, kwani timu yao ina uwezo wa kutimiza ndoto zao za muda mrefu, ambapo waliishia kuzitazama kwa mastaa wa Simba na Yanga wakitamba nazo.

Azam FC inayoongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 15 ikiwa imecheza mechi tano na kushinda zote, ilimsajili Lyanga kutoka Coastal Union ya Tanga ili kuongeza nguvu ndani ya kikosi hicho ambacho kilichukua taji la ligi hiyo msimu wa 2013/14.

Alisema kuvaa medali kwa mchezaji yeyote duniani baada ya kumalizika msimu ni jambo la heshima na ni kama kifuta jasho, hivyo ana matarajio makubwa kuona mwaka huu timu hiyo inanyakua taji la ligi hiyo, litakalomwezesha kutimiza ndoto yake.

“Kwa muda niliokaa na Azam tangu nijiunge nao msimu huu, nimegundua ina maono makubwa yaliyonipa imani ya kuvaa medali, kwani ninaamini tunachukua taji la ligi, ndio maana kila mechi kwetu ni kama fainali,” alisema Lyanga. “Mcha-

nganyiko wa wachezaji wa kigeni na wazawa unaleta ushindani ambao utatusaidia kufikia malengo kwa msimu huu, ukiachana na kuvaa medali pia itanifanya nionekane na timu za nje ambazo ndio ndoto yangu nyingine kwenda kucheza huko.”

Naye kiungo Awesu ambaye alisajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Kagera Sugar, alisema anafurahi kucheza ndani ya timu yenye uwezo wa kushindania taji la Ligi Kuu, jambo linalompa urahisi wa kuvaa medali ya pongezi.

“Azam ni timu kubwa, ina wachezaji wenye uzoefu utakaofanya tuchukue taji la ligi msimu huu na hilo ndilo lilikuwa lengo ama tamaa yangu kucheza klabu nitakayoweza kuvaa medali, ambazo kwa muda mrefu tunaona wanatamba nazo mastaa wa Simba na Yanga,” alisema Awesu.

Alisema timu yao imeanza vyema kwenye ligi, jambo linaloendelea kuwapa morali na kuongeza umakini wa kujituma kwa bidii, ili kuyafikia yale ambayo wanayapanga msimu huu.

KOCHA APANIA

Kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba amesema amezidi kufurahishwa na kiwango ambacho wanakionyesha wachezaji wake katika mechi za kirafiki na anaamini watatimiza lengo la kumaliza ligi wakiwa katika nafasi ya kwanza kwenye msimamo.

“Tunataka kumaliza ligi tukiwa katika nafasi ya kwanza na hilo ndilo jambo letu, wachezaji wangu wanajituma kuhakikisha kwamba kila kitu kinaenda kama ambavyo tumepanga.”

Katika mechi tano hadi sasa, Azam FC imeendelea kubaki kileleni na pointi 15.