Mastaa 6 Wapya Simba ya Kimataifa

Muktasari:

Tayari Simba imeshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na leo itacheza mechi yake ya mwisho ya ligi kwenye ardhi ya Dar es Salaam dhidi ya Alliance na itatoa nafasi kwa mashabiki kupiga picha na kombe kuanzia saa 6 mchana.

MABOSI wa Simba wanafikiria kuingiza sura sita mpya kikosini kujiweka sawa na msimu mpya hasa wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopangwa kuanza baadaye mwaka huu.

Tayari Simba imeshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na leo itacheza mechi yake ya mwisho ya ligi kwenye ardhi ya Dar es Salaam dhidi ya Alliance na itatoa nafasi kwa mashabiki kupiga picha na kombe kuanzia saa 6 mchana.

Mmoja wa vigogo wa Simba, ambaye hakupenda kutajwa gazetini, aliidokeza Mwanaspoti jana kwamba hawatafanya mabadiliko makubwa bali wataingiza sura za kazi lengo likiwa kuongeza ushindani kimataifa.

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema usajili wa msimu huu hautahusisha wachezaji wengi kama ilivyozoeleka, lakini kuna maeneo machache ambayo yana upungufu na hapo ndio wataweka mkwanja mrefu kunasa mastaa wakubwa.

“Kueleza wachezaji gani ambao tutawasajili kwa sasa hilo ni suala la uongozi kwani, tulianza kulifanyia kazi siku nyingi nyuma ila muda mwafaka ukifika kila kitu kitakuwa wazi kwani, tutasahili wachezaji bora wenye na uwezo wa kuongeza makali ya kikosi chetu msimu ujao,” alisema Sven na kugoma kuweka wazi idadi na majina.

Wakati Sven akieleza hayo Mwanaspoti lina taarifa za ndani kutoka Simba kuwa, tayari wako kwenye hatua za mwisho kuwanasa nyota watatu kutoka ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Mwanaspoti linafahamu kwamba, wachezaji hao ambao mpaka sasa Simba wameshamalizana nao kwa kiasi kikubwa ni Bernard Morrison (Yanga), David Kameta ‘Duchu’ wa Lipuli na Charles Ilanfya kutoka KMC huku wakipambania dili la Bakari Mwamnyeto (Coastal Union), ambaye wakala wake ndiye anayebipu watani wa jadi akitaka dau lipande.

Mastaa wengine wawili kutoka DR Congo yumo Mukoko Tonombe na Yannick Bangala Litombo wote kutokea AS Vita dili lao na Simba limekufa kutokana na ubora wa Gerson Fraga na Jonas Mkude kwa sasa.

Kama Simba watafanikiwa kuwapata mastaa hao sita maana yake watakwenda kupangua kikosi cha kwanza na makali yao yataongezeka.

Mchambuzi mahiri wa soka mwenye ukurasa wake ndani ya Mwanaspoti, Mwalimu Alex Kashaha alisema kiwango ambacho wameonyesha Simba msimu huu katika mashindano yote ya hapa ndani ni bora kuliko timu nyingine nyingi ambazo wamekutana nazo kwani, walionekana kuwazidi maeneo mengi.

“Simba wana wachezaji imara ambao wengine hawatumiki katika kikosi chao mara kwa mara na kama ingetokea kwenda timu nyingine basi wangepata nafasi ya kucheza mechi nyingi hivyo, sioni kama wanatakiwa kufanya usajili mkubwa,” alisema.

“Simba wanatakiwa kuangalia mashindano ya kimataifa msimu uliopita walifeli wapi na wakaondolewa katika hatua ya awali, lakini wanatakiwa kusajili wachezaji bora wataokwenda kushindana na wale wa timu za mataifa makubwa Afrika ili kusaka ubingwa wa Afrika,” aliongeza.