Masoud Juma: Nitapambana kulinda nafasi yangu Harambee Stars

Thursday June 6 2019

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Baada ya kubainika Kenya ingemkosa mshambuliaji Michael Olunga katika mchezo wa mwisho wa kusaka tiketi ya kwenda Misri dhidi ya Ghana, Straika pekee aliyebeba matumaini ya Harambee Stars ni Masoud Juma.

Zaidi ya mara moja amekuwa mkombozi palee inapobainika kuwa Olunga hatukuwepo, hata hivyo licha ya kuaminiwa na Kocha mkuu Sebastien Migne, kwa bahati mbaya sana, sehemu kubwa ya mashabiki, hawana imani naye. Hili analijua na linampa hasira sana.

Hata hivyo, hadithi hii ilikuwa tofauti mwishoni mwa mwaka 2017, alipopata fursa ya kwanza kuwakilisha bendera ya taifa. Alionesha uwezo mkubwa katika michuano ya CECAFA ambako alimaliza akiwa mfungaji bora huku akiiwezesha Kenya kutwaa uchampioni wa mashindano hayo.

Miaka ikasonga, na miaka miwili baadae, kila mtu sasa anahoji uwezo wa straika huyo wa zamani wa Kariobangi Sharks, ambaye kwa sasa hana timu. Akizungumzia hilo ambaye ni yupo kambini na Stars huko Paris Ufaransa, alisema.

“Mwaka 2016 nikiwa Sony Sugar, nilipotajwa kwenye kikosi cha Harambee cha U23, Wakenya waliniamini sana. Chuki zilianza nilipoenda Kariobangi Sharks," alisema na kuendelea

"Hali ilikuwa vivyo hivyo nikiwa Bandari, nadhani mashabiki hawana shida na mimi bali ni hii timu ambayo wengi wanaihusisha na Rais wa FKF, Nilijua mambo yataniendea poa Libya lakini vurugu vya kisiasa vimetibua mipango yangu, " alisema Juma.

Advertisement

Straika huyo, alisema anataka kutumia AFCON kurudisha imani ya wakenya juu yake, huku akisisitiza atapigania nafasi yake katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 kitakachoenda Misri kwa ajili ya fainali hizo zitakazoanza Juni 21 hadi Julai 19.

Juma ni sehemu ya washambuliaji wanne kwenye kikosi cha Stars watakaopigania nafasi kwenye kikosi kitakachoshuka dimbani kupimana nguvu na Madagascar kesho. Mastraika wengine ni John Avire, Michael Olunga na Christopher Mbamba.

Kikosi cha Migne, kitacheza mechi mbili za kirafiki ya kwanza, ikipigwa kesho (Juni 7), Jijini Paris dhidi ya Madagascar na ya pili ikiwa ni dhidi ya DR Congo, itakayopigwa Juni 15, Jijini Madrid.

Stars ambayo iko kundi C, itaanza kutupa karata yake Juni 23, dhidi ya Algeria, kisha itavaana na Tanzania (Juni 27) kabla ya kumalizana na Senegal,  Julai mosi. Mechi zote zitapigwa Cairo, katika uwanja wa June 30.

Kikosi cha Stars:

Makipa: Patrick Matasi, John Oyemba, Faruk Shikalo

Mabeki: Abud Omar, Joash Onyango, Joseph Okumu, Musa Mohammed, David Owino, Bernard Ochieng, Brian Mandela, Philemon Otieno, Eric Ouma

Viungo: Victor Wanyama, Anthony Akumu, Ismael Gonzalez, Ayub Timbe, Francis Kahata, Ovella Ochieng, Dennis Odhiambo, Eric Johanna, Paul Were, Cliffton Miheso, Johanna Omollo

Mastraika: John Avire, Masoud Juma, Christopher Mbamba, Michael Olunga

 

Advertisement