Masikini! Samatta ndiyo basi tena

Muktasari:

Mshambuliaji huyo amekuwa na kiwango cha juu msimu katika klabu yake ya Genk akiwa amefunga zaidi ya mabao 10 katika mashindano yote barani Ulaya

Dar es Salaam. ‘Hakuna ushindi usiokuwa na kilio’ hivyo ndiyo hali halisi kwa nahodha Mbwana Samatta baada ya kuiongoza Taifa Stars kuichapa Cape Verde kwa mabao 2-0, ataikosa mechi ijayo dhidi Lethoso ugenini.

Nahodha huyo wa Tanzania atakosa mechi mmoja baada ya kupata kadi ya tatu za njano katika mechi dhidi ya Uganda na michezo yote miwili dhidi ya Cape Verde.

Samatta amekuwa na mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji wa Taifa Stars hivyo kukosekana katika mchezo ujao dhidi ya Lethoso kutamlazimisha kocha Emmanuel Amunike kubadili mbinu.

Pengo la Samatta linaweza kuzibwa na washambuliaji Thomas Ulimwengu, John Bocco au Rashid Mandawa ambao watalazimika kutengeneza pacha mpya.

Tanzania ni lazima ishinde mchezo wake ujao ugenini ili kuweka uhai wa matumaini yake ya kufuzu kwa AFCON 2019 ikiwa ni mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo 1980 nchini Nigeria.

Mabao ya nahodha, Mbwana Samatta na Saimon Msuva yamefufua matumaini ya Taifa Stars kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwakani baada kuichapa Cape Verde 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

Mshambuliaji Difaa Jadidi, Msuva alifunga bao la kwanza kwa Stars akimalizia vizuri krosi ndogo ya Samatta aliyewatoka mabeki wanne wa Cape Verde na kupiga krosi iliyomkuta mfungaji.

Samatta alifanya kile walichosubiri mashabiki wa Tanzania katika kipindi cha pili kwa kufunga bao la pili kwa shuti kali akiwa ndani ya 18, baada ya kupokea pasi ya Mudhathir Yahya.

Ushindi huo unaifanya Taifa Stars kupanda hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi 5, wakati Uganda wakiongoza Kundi L kwa pointi 7, wakati Cape Verde ya tatu na pointi 4 na Lethoso ya mwisho ikiwa na pointi 2.