Mashine nne fungakazi zinatua Yanga, yumo mrithi wa Tshishimbi

Friday August 14 2020

 

By KHATIMU NAHEKA

YANGA kupitia mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Hersi Said imethibitisha kuwa wamebaki wachezaji wanne funga kazi.

Hersi ameliambia Mwanaspoti kuwa wamemaliza usajili wa wachezaji wa ndani ambapo wa mwisho ni winga wa kushoto, Farid Mussa aliyesaini mkataba juzi. Farid alisaini mkataba wa miaka miwili akitokea Tenerife ya Hispania iliyompa mkono wa kwaheri mwezi uliopita sambamba na wenzake sita.

“Ikitokea kama tutasajili mchezaji wa ndani labda kwa dharura, hatudhani kama hilo litatokea, sasa hesabu zetu hapa ndani ni kama tumezikamilisha, kila tuliyemtaka tumeshamchukua,” alisema.

Hersi alisema wanataka kukamilisha usajili wa wachezaji wa kigeni ambapo wamebakiza nafasi zisizozidi nne.

“Tunahitaji washambuliaji wawili wa kati, tayari tuna mmoja mpaka sasa Yacouba (Sogne) ambaye ameshasaini mkataba wa miaka miwili, kuna haja ya kuwa na winga wa kulia ambaye atakuja kuongeza kasi kule mbele, kuna mbadala wa Tshishimbi (Papy) atakayekuja kucheza kama kiungo mkabaji.” Ingawa Said hakufafanua kwa majina, lakini Mwanaspoti linafahamu Yanga itamalizana na winga wa kulia, Tuisila Kisinda, kiungo mkabaji Mukoko Tonombe wote kutoka AS Vita ya DR Congo huku washambuliaji wakiwa bado hawajajulikana.

Alisema kwamba mpango wa kuwa na kambi ya maandalizi nje ya nchi hautakuwepo kutokana na muda mfupi uliosalia kabla ya kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu, Septemba 6.

Advertisement

“Tulikuwa tunafikiria tuipeleke sehemu maalumu timu kwa ajili ya maandalizi, lakini mpaka sasa hatujamtangaza kocha mpya na mchakato huenda ukakamilika wiki hii,” alisema.

“Utaona pia muda si rafiki sana uliosalia kabla ya kuanza ligi, ni mchache na bado hata wachezaji wote hawajakutana kama timu, tuna tamasha la Wiki ya Mwananchi, hivyo uwezekano wa timu kuandaliwa hapahapa ndani ni mkubwa.”

Advertisement