Mashindano ya Taifa yapelekwa Arusha

Monday December 10 2018

 

By Yohana Challe

BAADA ya danadana nyingi, hatimaye Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) limetangaza Mashindano ya Taifa ‘Ngorongoro National Open Championship 2018’ yatafanyika mkoani Arusha mwishoni mwa wiki hii.

Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday alisema awali mashindano hayo yalikuwa yafanyike jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa lakini kutokana na maombi ya mdhamini wa mashindano hayo, Mamlaka ya Ngorongoro (NCAA) wameamua kuyapeleka Arusha.

“Tunafahamu tupo nyuma ya kalenda ya Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF) lakini tumeandika barua IAAF na wameturuhusu kufanya hivyo japo kwa onyo kali, tumeamua kufanya mashindano ya wazi na kila mmoja anakaribishwa kushiriki,” alisema Gidabuday.

Aliongeza awali walipendekeza mashindano hayo yafanyike Dodoma au Singida lakini kuna mapungufu yalijitokeza katika viwanja ambavyo vilitakiwa kutumika.

Mashindano hayo yatafanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Desemba 14 na itakuwa njia moja wapo ya kuisaidia RT kufanya uchaguzi wa timu za taifa kwaajili ya mashindano mbalimbali kwa watakaojitokeza na kuonyesha uwezo wao siku hiyo.

“Mwaka uliopita hatukuweza kufanya, kutokana na kutekeleza kalenda yetu iliyotubana zaidi, hivyo tumeona vyema mwaka huu vijana wakapata nafasi hii muhimu kuonyesha viwango vyao.”

Alisema washindi watakaofanya vizuri watapata fursa ya kushiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwamo kwenda Japan, kusaka viwango vya kufuzu mashindano ya kimataifa hasa yale ya dunia yatakayofanyika Doha mwaka ujao na yale ya Olimpiki ya 2020 kule Tokyo.

Awali, RT ilipanga mashindano ya taifa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Novemba 16 kabla ya kuahirishwa ili kupisha yale ya Taifa ya Wanawake yaliyofanyika kwenye uwanja huo Novemba 24 na 25.

Michezo itakayoshindaniwa ni mbio za kupokezana vijiti, miruko, kurusha tufe, kurusha mkuki pamoja. Huku zawadi zitakazotolewa Gidabuday, alisema mshindi wa kwanza atapata medali na kitita cha Sh150,000, mshindi wa pili medali na Sh100,000 na mshindi wa tatu atapata na medali pamoja Sh 50,000.

Advertisement