Mashemeji Derby kupigwa Februari 10, Ratiba KPL hii hapa

Muktasari:

Mechi ya kwanza ya mashemeji derby kwa msimu wa 2018/19, kati ya mabingwa mara 17 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), klabu ya Gor Mahia dhidi ya watani zao, AFC Leopards itapigwa Februari 10, mwakani.

Nairobi, Kenya. Mabingwa wa soka nchini Kenya, Gor Mahia watafungua kampeni ya kusaka ubingwa wao wa 18 wa Ligi Kuu Kenya (KPL), Desemba 8, mwaka huu, kwa kuwakabili Bandari FC, ugenini katika dimba la Mbaraki, Mjini Mombasa.

Kwa mujibu wa ratiba ya msimu mpya wa soka, 2018/19, kutakuwa na jumla ya mechi sita siku hiyo, zote zikipigwa kuanzia saa tisa alasiri katika viwanja tofauti ambapo mshindi wa mechi ya mtoano kati ya Ushuru na Nakumatt FC, itakayopigwa mapema, atakutana na Sofapaka, ugani Ruaraka.

Mbali na mtanange wa kukata na shoka kati ya Kogalo na Bandari, wababe wengine watakaoshuka dimbani, Desemba 8, ni pamoja na AFC Leopards ambao watakuwa wenyeji wa Kariobangi Sharks (Machakos), huku Mathare United wakilianzisha dhidi ya Chemelil Sugar (Moi Kasarani).

Mjini Kakamega katika dimba la Bukhungu, wageni KCB, watakaribishwa kwenye ligi na Kakamega Homeboyz. Siku ya Jumapili, kwa mujibu wa ratiba hiyo, iliyotoka jana, kutakuwa na mechi tatu, huku mechi ya kwanza ya Mashemeji Derby, ikipangwa kufanyika Februari 10, mwakani, ugani Moi Kasarani.

Ratiba ya wikendi ya kwanza: Jumamosi, Desemba 8

Nakumatt/Ushuru Vs Sofapaka- Ruaraka

Mathare United vs Chemelil- Kasarani

Bandari vs Gor Mahia- Mbaraki

AFC Leopards vs Kariobangi Sharks- Machakos

Homeboyz vs KCB -Bukhungu

Posta vs Western Stima- Ruaraka

Jumapili, Desemba 9

Zoo vs Nzoia Sugar- Green Stadium Kericho

Sony Sugar vs Tusker FC Green Stadium Awendo

Vihiga United vs Ulinzi Stars- Mumias Complex