Mashabiki watano kuishangilia Taifa Stars Afcon

Tuesday June 11 2019

 

Dar es Salaam. Watanzania watano wameshinda safari ya kwenda Misri kuishangilia timu ya taifa ‘Taifa Stars’ katika mashindano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Africa (Afcon) 2019.

Mashabiki hao wameshinda katika shindano la Benki ya Exim litwalo “Deposit & Win – Twende Tukaliamshe Misri” ilikuwa inatoa fursa kwa wateja wa benki hiyo kulipiwa gharama zote za safari na malazi ili waweze kushuhudia mechi za timu ya taifa, Taifa Stars katika mashindano hayo.

Washindi hao ni Musa Mohamed (Mtwara)  Athumani Hassani (Manyara), Deogratius Kessy (Arusha), Msimu Ngaruka (Dar es Salaam) pamoja na Justine Tembo (Arusha) wamepatikana kupitia droo kubwa ya kampeni hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo chini ya uangalizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT)

Akizungumza baada ya kupatikana kwa washindi hao Mkuu wa huduma ya rejareja wa benki ya Exim, Andrew Lyimo alisema washindi hao watapata fursa ya kuungana na Taifa Stars katika mashindano Afcon nchini Misri huku wakiwa wamelipiwa gharama zote za safari ikiwemo gharama na Visa, tiketi ya ndege, gharama za tiketi ya kushuhudia mechi hizo pamoja na fedha za kujikimu.

Lyimo alisema ili kushiriki katika kampeni hiyo, wateja wapya walipaswa kufungua Akaunti ya Akiba na kuhakikisha kila mwezi ina kiasi kisichopungua Sh 500,000 au zaidi au kufungua akaunti ya Current/biashara ikiwa na wastani wa kila mwezi wa Sh 10,000,000 au hifadhi ya amana maalum (Fixed deposit) yenye thamani isiyopungua Tshs 5,000,000.

“Kwa wateja ambao tayari wana akaunti ya benki ya Exim walichotakiwa kufanya ni kuongeza akiba kwa kiasi cha Sh 500,000 au zaidi kwa Akaunti za Akiba au kuongeza kiasi cha Sh 10,000,000 kwenye akaunti zao za Current/biashara au kuwa na hifadhi ya amana maalum (Fixed deposit) yenye thamani isiyopungua Sh 5,000,000.’’ alibainisha

Advertisement

Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, Stanley Kafu alisema kampeni hiyo inatoa nafasi kwa washindi hao kuweza kushuhudia Taifa Stars ikitimiza ndoto zake za kushiriki katika mashindano ya AFCON baada ya zaidi ya miaka 30 kupita.

Kafu alisema kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa kibenki katika kutafuta kesho bora kwa wateja wake na jamii kwa ujumla ambapo pamoja na mambo mengine benki hiyo imekuwa ikiunga mkono agenda za kitaifa ikiwemo suala zima la michezo.

 

 

Advertisement