JICHO LA MWEWE: Mashabiki wa Yanga wanatembea na ‘Stress’ mfukoni?

KICHWA cha habari kinasadiki matukio yasiyo ya ajabu ambayo hatukuyaona wakati fulani Yanga ikiwa na kikosi kilichokuwa kinaleta raha uwanjani kila kukicha. Walirusha viti? Hapana. Walipiga mashabiki wa timu pinzani? Hapana.

Naikumbuka Yanga bora iliyowahi kutokea katika miaka ya karibuni. Ilikuwa na akina Thaban Kamusoko, Simon Msuva, Donald Ngoma, Amis Tambwe, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani katika ubora wake, Haruna Nizyonzima, Obrey Chirwa akaja baadaye.

Katika ubora wao waliwahi kucheza mpira mkubwa dhidi ya Al Ahly ugenini. Kwangu inabakia kuwa mechi bora zaidi kwa timu ya Tanzania dhidi ya timu kubwa ya nje katika uwanja wa ugenini. Sijawahi kuona soka kama lile.

Wakati ule Yanga walikuwa na utawala wa ndani wa soka letu. Walifunga kwa kadri walivyojisikia. Walipiga kandanda safi ambalo msemaji wao wa wakati ule, Jerry Muro alilipachika jina la ‘Kampa Kampa tena’. Thaban Scara Kamusoko alikuwa fundi mipango wa soka hili.

Yanga ingeingia uwanjani ikiwa haina hofu ya kumfunga kipa wa mtani wao wa jadi. Matokeo yangeweza kuja vyovyote vile lakini hawakuwa na timu ya kuwapa hofu dhidi ya adui yoyote yule. Awe Simba, awe Azam au awe Al Ahly.

Nakumbuka Yanga ikiichapa Simba 2-0 Uwanja wa Taifa (Mkapa). Donald Ngoma akamuachia kesi nzito, Hassan Kessy aliyemrudishia kipa wake mpira mfupi, Ngoma akauwahi, akamzunguka kipa na kufunga. Malimi Busungu akafunga bao la pili.

Wakati Yanga ile ikitamba hatukuwa na matukio ya kuona mashabiki wao ikiwapiga mashabiki wa timu pinzani kwa namna yoyote ile. Sana sana ilikuwa mashabiki wa watani wao ndio ambao waliwahi kutufanyia mambo ya ajabu. Nakumbuka walivyong’oa viti katika pambano dhidi ya Kagera Sugar pale Uwanja wa Benjamin Mkapa. Mabomu yakatuliza vurugu.

Wakati ule watani wao ndio walikuwa na msongo wa mawazo (Stress). Wao walikuwa na timu safi, kandanda safi, pesa nyingi kutoka kwa tajiri, Yusuf Manji na mengineyo. Leo kuna baadhi ya mambo yamehama. Timu safi imekwenda Msimbazi na wao ndio wanajitahidi kutengeneza timu safi.

Kwa sasa Yanga wanamuona kila mtu adui yao. Mashabiki wa timu pinzani ni maadui, waamuzi ni maadui, TFF ni adui. Wakati ule tabia hii ilikuwa Simba. nakumbuka kumuona rafiki yangu, Haji Manara akibeba seti ya televisheni kwenda nayo katika mkutano wa waandishi wa habari kuwalalamikia waamuzi. Leo hawezi kufanya vile. Hana stress. Timu yake inafanya vema.

Stress zimehamia Yanga. Majuzi katika pambano lao dhidi ya Coastal walimvamia Bibi mmoja shabiki mkubwa wa Coastal Union na kumuhisisha na imani za kishirikina. kisa? Kipindi cha kwanza walikosa mabao na waliamini yule bibi alikuwa anazuia mabao yao.

zamani wakati timu yao ipo fomu wasingefanya ujinga huu. walikuwa wanajua mabao yalikuwa suala la muda tu. Leo hawana uhakika sana. Msimu uliopita walikuwa na wachezaji wabovu, majuzi walikuwa na kocha mbovu. Mabao bado sio kitu cha uhakika sana. Kabla ya huyu bibi baadhi ya mashabiki wa Yanga walikuwa wakiwapiga mashabiki wa Simba katika pambano la Ligi Kuu pale Morogoro. Pambano dhidi ya Mtibwa. Hawakuwa na sababu za msingi sana zaidi ya Stress.

Baadaye kuna shabiki mmoja mjinga wa Simba alikuwa akisikika akitamba kwamba kazi yake ilikuwa ni kuhakikisha Yanga haipati ushindi. Nadhani tatizo lilikuwa wachezaji wa Yanga wenyewe lakini sio shabiki. Leo unaweza kujinasibu kwenda katika pambano la Simba dhidi ya Biashara kwa ajili ya kuhakikisha Simba hashindi?

Kabla ya hapo Yanga ilikuwa imemchania shabiki mmoja wa Simba jezi yake huku wakimdunda. ‘stress’ zao zilikuwa katika ubora wa hali ya juu. Shabiki mmoja wa Simba aliyekaa nao anawezaje kuihujumu timu yao? Anawezaje kumzuia, Tuisila Kisinda asikimbize mpira uwanjani?

Matukio haya yataondoka kwa sababu mbili. Kwanza ni kwa sisi wenyewe kukemea, lakini pili yataondoka pindi Yanga ikirudisha ubora wao uwanjani na kuanza kucheza kandanda safi lililopitiliza kama ilivyokuwa zamani. Hata hawa Simba ambao wamekuwa wastaarabu kiasi cha kupiga picha wakiwa na shabiki wa Yanga wakiwa na raha zao ni kutokana na matokeo na ubora wa timu yao. Kwao wanajua akina Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco wana uwezo wa kuiharibu timu yoyote na muda wowote.