Mashabiki wa Yanga Mwanza waunga mkono Zahera kutimuliwa

Muktasari:

Zahera ameiongoza Yanga katika mechi nne za Ligi Kuu msimu huu akishinda miwili, sare moja na kupoteza moja na kuvuna pointi saba wakiwa nafasi 17 katika msimamo wa ligi.

Mwanza. Saa chache baada ya Uongozi wa Yanga kuvunja mkataba na aliyekuwa Kocha wake Mkuu Mwinyi Zahera wanachama na mashabiki wa timu hiyo jijini Mwanza wamepongeza hatua hiyo.

Zahera ameiongoza Yanga katika mechi nne za Ligi Kuu msimu huu akishinda miwili, sare moja na kupoteza moja na kuvuna pointi saba wakiwa nafasi 17 katika msimamo wa ligi.

Mwenyekiti wa Yanga, Mkoa wa Mwanza, Saleh Akida amesema watamkumbuka kocha huyo kwa mazuri aliyofanya, lakini wanaunga mkono uamuzi ya viongozi.

Alisema Zahera alikuwa kocha mwenye mapenzi na Mkoa wa Mwaza, lakini lazima wakubaliane na matokeo kwani asilimia kubwa Yanga inahitaji ushindi katika mashindano yoyote.

“Tunakubaliana na uamuzi, pia niwaombe mashabiki na wanachama tuendelee kuungana kwa pamoja ili timu yetu ifanye vizuri hata katika viporo tulivyonavyo katika Ligi Kuu,”alisema Akida.

Shabiki wa timu hiyo, Haroun Manpopat alisema uamuzi hayo ni sahihi, kwani mashabiki wanachohitaji ni furaha kwa timu yao kupata matokeo mazuri uwanjani.

“Timu ni ya wananchi ambao ndio sisi, ina maana uamuzi hayo ni kutokana na kukosa furaha, hata usajili wa wachezaji wapo ambao kwa ujumla hawana kiwango cha kuwa Yanga walioletwa na kocha huyo,”alisema Manpopat.