Mashabiki wa Yanga Arachuga wamgeuzia kibao Zahera

Muktasari:

Obrey Chirwa amesaini mkataba wa kuitumikia Azam kwa mwaka mmoja ambapo  ametoa msimamo wake wa kuhakikisha timu yake hiyo inatwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara msimu huu

 Kitendo cha mshambuliaji Obrey Chirwa kuingia kandarasi ya mwaka mmoja katika Klabu ya Azam fc, kimewaacha midomo wazi wanachama wa klabu yake ya zamani (Yanga ) wasiamiani kilichotokea huku wakimtupia lawama kocha wao mkuu Mwinyi Zahera.

Chirwa aliyekuwa mfungaji bora wa msimu uliopita baada ya kutupia jumla ya mabao 13 akiitumikia Yanga, amefanikiwa kusaini kandarasi hiyo kama mchezaji huru akitokea nchini Misri alikokuwa anakipiga katika Kbalu ya No-goom El Mostakbal fc.

Baada ya kurudi nchini wanachama na mashabiki wa Yanga walitegemea mshambuliaji huyo angerudi kuendelea kuwatumikia lakini matokeo yake yakawa ndivyo sivyo kutokana na mabosi hao kushindwa kumlipa mshahara wake wa miaka mitatu.

Katibu mkuu wa Yanga tawi la Arusha Destrich Kateule alisema kuwa walitegemea Chirwa angerudi kuendelea kutumikia mkataba wake lakini hali imekuwa tofauti jambo wanaloamini limesababishwa na kocha wao mkuu Mwinyi Zahera.

“Kwenye timu kwa sasa hatuna matokeo mazuri kwenye mechi nyingi tulizocheza hivyo tulitegemea nafasi ya ufungaji ambayo imekuwa ikipwaya kila mechi na kocha kutafutia sababu hapo suluhu lingekuwa Kurudi kwa Chirwa lakini naona hali imekuwa ndivyo sivyo”

Ashura Mohamed alisema kuwa kuachwa kwa Chirwa kwenda kutumikia klabu nyingine wakati alikuwa ni mchezaji wao kitawagharama hali hiyo kutokana na mchezaji huyo bado alikuwa tegemezi kwao lakini matokeo ya haya yanayoendelea yatakuja kusababisha hata mgomo baridi kwa baadhi ya wachezaji.

“Hoja ya kocha kuwa Chirwa alikuwa hana nidhamu sijui undani wake lakini kama kosa ni kudai mshahara wake ni haki yake maana alikuja kucheza kulipwa hivyo busara ingetumika kumtuliza na kuanza kushughulikia swala lake maana udhaifu mkubwa kwa timu tuliyonayo ni hao washambuliaji akiwemo huyo aliyeachwa”

Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya mashindano ya Yanga Athumani Kihamia alisema kuwa swala la nidhamu lililotolewa na kocha kwa ajili ya kuachana na Obrey Chirwa ni la msingi kikubwa wazingatie usajili wa dirisha dogo lijalo kwa ajili ya kufanya maboresho ya nafasi zilizopwaya ikiwemo washambuliaji kwa ajili ya kuimarisha ngome.

“Yeye kocha afanye afanyavyo ila kitendo cha kulaumu wachezaji kila mechi ni utovu mkubwa wa nidhamu kufanya matokeo mabaya kama ni ngao  yake ya kujilinda maana haiwezekani kila mchezaji ni mbaya , hakuna asiyejua ubora wa wachezaji hawa kwa sasa”

“Mfano mzuri hivi karibuni anavyomvaa (Ibrahim) Ajibu wakati kwa sasa, hana wa kumkaribia kwa wachezaji wote nchini kwa ubunifu labda anafuatiwa kwa mbali na Chama na Fei Toto…, Mwisho atahamishia lawama kwa viongozi. Kutokana na hali halisi ya Yanga iliyopo kwa sasa wanahitajika makocha wazawa, vinginevyo ubingwa utakuwa ni ndoto. Timu haishambulii inalinda tu, utadhani imeshashinda kabla ya kucheza, Ni maoni yangu binafsi,” alisema Kihamia ambaye pia mjumbe wa kamati ya uwekezaji TFF.