Mashabiki wa Simba SC wapagawa na Uwanja Bunju

Muktasari:

Mashabiki wamewaomba viongozi wa Simba kuweka taa kwenye uwanja huo ili wawe wanalala uwanjani hapo.

Dar es Salaam.Mashabiki wa Simba SC wameshindwa kuzuia hisia kutokana na maendeleo yaliyofanyika kwenye uwanja wa klabu yao uliyopo Bunju, Dar es Salaam.

Mashabiki hao walijitokeza kwa wingi uwanjani hapa majira ya saa 10:00 asubuhi na walikuwa wakifuatilia kila hatua ambayo ilikuwa ikiendelea uwanjani hapa.

Baada ya kuona wafanyakazi wakijivuta katika kutandika nyasi bandia, mashabiki hao waliamua kwenda katika kontena na kubeba wenyewe nyasi hizo.

Mashabiki hao wakati wanazibeba nyasi walikuwa wakisikika wakiimba "Simba, Simba, Simba" huku wakipeana morali katika ubebaji.

Licha ya kubeba nyasi hizo bado hawakuridhika badala yake walitaka kuzitandika wenyewe lakini wahusika hawakuwaruhusu kabisa kufanya hivyo.

Mashabiki hao walielezea namna walivyopokea kwa shangwe matengenezo hayo haswa kuweka nyasi bandia.

Salvatory Michael aliwaomba viongozi wa Simba kuweka taa kwenye uwanja huo ili wawe wanalala uwanjani hapo huku akifurahia kwa hatua uliofikia.

"Tulisubiria kwa muda mrefu kuona hatua hii ya uwanja kubandikwa nyasi bandia tunaishuhudia kwa macho sasa imekuwa, tunawaomba viongozi waweke taa ili tuwe tunalala hapa hapa," alisema Michael.

Katika tukio la kushuhudia kubandikwa nyasi bandia Uwanja wa Bunju halikushuhudiwa na mashabiki wa Simba walikuwepo na Yanga ambao waliwapongeza watani wao na kuitaka klabu yao kuiga mfano huo.

Shabiki wa Yanga aliyejitambulisha kwa jina la Mr Doni alisema licha ya kuwa yeye haipendi Simba, lakini anaipongeza kwa hatua waliofikia na kuwataka viongozi wa Jangwani kufanya mpango wa kuukarabati uwanja wa Kaunda.

"Ni hatua nzuri kwa kweli Simba na Yanga ni klabu kongwe ambazo zilitakiwa kuwa mfano dhidi ya timu zinazoshiriki ligi kuu, pia utatusaidia kuwaona mastaa ana kwa ana, nimefurahia," alisema.

Wapo mashabiki waliofika asubuhi na wengine waliendele kufika na magari na waliotumia usafiri wa pikipiki ili kushuhudia kama kweli uwanja huo umebandikwa nyasi bandia.

Wapo ambao hawakutaka kutaja majina yao lakini walisema wamepata ajira kupitia ukarabati wa uwanja huo.

 Ukiachana na uwanja walioweka nyasi bandia ule wa nyasi asilia nao unaendelea kufanyiwa marekebisho ambapo wapo ambao walikuwa wanaondoa majani na kumwagilia maji.

WADAU WAUZUNGUMZIA UWANJA

Mchezaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema Mohamed Dewji ameandika rekodi ambayo itakumbukwa na vizazi nenda rudi.

Alisema laiti kama angekuwa anacheza anaamini angefanya mambo makubwa akiwataka wachezaji kujitambua na kujiona wamefikia levo ya kimataifa.

"Uwanja wa Bunju uwe wa machinjioni timu zinazokuja kucheza pawe pa machinjioni, ule wa taifa uwe wa ugenini, niwakati wa wachezaji wa Simba, mashabiki kujidai kwa kufanya makubwa,” alisema Batigol.

Kocha wa zamani wa Stand United, Athuman Bilali 'Bilo'alisema walichofanya Simba kinaashiria soka la Tanzania kukua na kila timu ikiwa na uwanja wake ushindani utapatikani.