Mashabiki wa Bongo kumshuhudia Ronaldo, Dzeko, Higuain

Muktasari:

Wapenzi na wadau wa soka nchini wamesogezewa karibu mshambuliaji Cristian Ronaldo, baada ya Ligi hiyo kuletwa nchini tena kwa lugha ya Kiswahili.

Dar es Salaam. WAPENZI na wadau wa soka nchini, wameletewa fursa ya kuangalia Kombe la FA Italia (Copa Italia) kwa lugha ya Kiswahili baada ya kampuni ya Star Media kupitia Star Times kupata haki za kuonyesha Mashindano hayo kwa miaka mitatu kuanzia msimu huu mpaka 2020/21.

Copa Italia ni moja kati ya mashindano yenye ushindani wa hali ya juu na msisimko wa aina yake barani Ulaya kwani huzikutanisha timu 16 zinazocheza katika ligi kuu ya nchini Italia maarufu kama Serie A, daraja la kwanza Serie B na Serie C ili katika mzunguko wa kwanza kutafuta timu 8 ambazo zitaungana na timu 8 za juu katika msimamo wa ligi kuu (Serie A) ili kucheza hatua ya 16 bora.

Afisa uhusiano wa StarTimes, Sam Gisayi, alisema mpira wa Kitaliano ni moja ya soka zinazovutia sana kutazama ndio maana tumewaletea wateja wetu kandanda hili la kusisimua. Pia ni katika mwendelezo wetu wa kuhakikisha hatuishiwi soka hata pale wengine wanapokaukiwa. Pia Italia kuna timu nyingi na bora ambazo zitashiriki katka Coppa Italia, Mfano Juventus, timu za jiji Milan, Napoli na AS Roma ambazo zitashiriki.

“Kwa hiyo wateja wetu wanao uhakika wa kumtazama Cristiano Ronaldo, Edin Dzeko, Gonzalo Higuain, Paulo Dybala na sasa kuna tetesi Msweden Ibrahimovich atarejea AC Milan hivyo burudani itaongezeka maradufu”. Aliongeza

Mbali na Coppa Italia, Disemba StarTimes watakuwa na michuano ya Club World Cup ambayo kwa kuanzia tarehe 12 kupitia chaneli zao za michezo. Kwa mara nyingine tena wateja wake wana nafasi ya kuwashuhudia Mabingwa Real Madrid wakijaribu kutetea taji hilo bila kuwa na Cristiano Ronaldo.

Ligi ya Italia imeongeza mashabiki duniani kote baada ya mshambuliaji Cristiano Ronaldo kutua katika kikosi cha Juventus inayoshiriki Ligi Hiyo.