Mashabiki nusu tu kuziona Simba, Yanga

Friday July 10 2020

 

By THOMAS NG'ITU NA ELIYA SOLOMON

MKURUGENZI wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo amesema wao kama serikali katika kuhakikisha wanajilinda na ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Serikali imepunguza idadi ya mashabiki katika mchezo wa nusu fainali za Kombe la Shirikisho la Azam baina ya Simba na Yanga, itakayochezwa keshokutwa Jumapili saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, uwanja wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000.
 Kupunguzwa kwa idadi ya mashabiki watakaoingia uwanjani ni njia mojawapo ya kuendelea kujilinda na ugonjwa huo ambao umepungua kwa kiasi kikubwa nchini hadi kufikia serikali kuruhusu shughuli za michezo kuendelea lakini kwa kuchukuwa tahadhali.
Singo amesema ulinzi utakuwa imara kuhakikisha suala hilo linafanyika kwa uangalizi mkubwa ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.
"Tiketi zitakazotoka ni 30, 000 tu hapo kwa maana ya nusu ya uwanja, mchezo uliopita ule watazamaji waliingia 59000 hivyo tumeona tupunguze kidogo,".
"Kwa wale ambao hawatopata tiketi huko zinapouzwa katika vituo basi wasije kabisa uwanjani kwa sababu hapa hazitouzwa kabisa maeneo ya uwanjani ili kuondoa mikusanyiko," amesema.
Singo ameongeza kwa kusema suala la ukatishwaji wa tiketi kwa muda huu utasimamiwa na Serikali.
"Selcom tumemaliza nao mkataba hivyo serikali kupitia Wilaya ya Temeke ndio watasimamia mchakato huu mzima wa uuzwaji wa tiketi,".
Viingilio katika mchezo huo VIP A  ni Sh 30000, VIP B Sh 25000, VIP C  Sh 20000 na mzunguko Sh10000.

Advertisement