Mashabiki bana, eti Ole hafiki Krismasi

Muktasari:

Man United itaingia Desemba kwa kumenyana na Tottenham, kisha siku nne baadaye itakipiga na mahasimu wao Manchester City. Baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa, watarudi kukipiga na Everton, Watford, Newcastle, Burnley na Arsenal kwenye siku ya Mwaka Mpya.

MANCHESTER, ENGLAND. MASHABIKI wa Manchester United wanaamini kwamba kocha wao Ole Gunnar Solskjaer yatamkuta kama yaliyomkuta Jose Mourinho na atafutwa kazi kabla ya Krismasi.

Ratiba ya msimu mpya wa Ligi Kuu England imeshatoka ambapo Man United wanakabiliwa na shughuli pevu kwenye mechi ya kwanza tu wakimenyana na Chelsea uwanjani Old Trafford.

Lakini, suala la kumaliza mwaka na kuingia Mwaka Mpya ndicho kitu kinachosubiriwa kwa hamu kuona kama Ole ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho.

Man United itaingia Desemba kwa kumenyana na Tottenham, kisha siku nne baadaye itakipiga na mahasimu wao Manchester City. Baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa, watarudi kukipiga na Everton, Watford, Newcastle, Burnley na Arsenal kwenye siku ya Mwaka Mpya.

Msimu uliopita ulishuhudia Mourinho akifutwa kazi dESEMBA 19, akiacha Man United kwenye nafasi ya sita ikiwa ni mwanzo wa hovyo zaidi kwenye historia yao katika michuano hiyo tangu mwaka 28.

Katika kuelekea kufutwa kazi, Mourinho alikuwa ameshinda mechi moja tu kati ya sita na kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Liverpool kilihitimisha maisha yake kwenye kikosi hicho. Na mashabiki wa timu hiyo wanaamini Solskjaer naye yatamkuta kama hayo huko Old Trafford.

Shabiki mmoja alisema: "Solskjaer anafukuzwa kazi Novemba."

Mwingine aliongeza: "Shikeni maneno yangu baada ya kuona ile ratiba ilivyo, Ed Woodward ataendelea na kazi yake ya kuwalipa makocha fidia za kuwafukuza. Solskjaer atafukuzwa kabla ya Krismasi."

Kuna mwingine aliandika: “Oktoba 21: Ole Gunnar Solskjaer ataondoka Manchester United baada ya maafikiano.” Kuna aliyetabiri: "Walau tunaweza kutambua tarehe ambayo Ole atafutwa kazi, baada ya kipigo cha 2-0 kutoka kwa Norwich, Oktoba 26."

Kama Ole atafutwa kazi kipindi hicho, basi kocha atakayekuja atakula bata kwenye mechi nane za mwisho ambapo itakuwa dhidi ya Sheffield United, Brighton, Bournemouth, Villa, Southampton, Palace, West Ham na Leicester City.