Mashabiki Simba waililia Serikali ya Tanzania

Muktasari:

Juni Mosi ndiyo tarehe rasmi ambayo Serikali ilitangaza kurejea kwa michezo nchini hususani soka baada ya kusimama kwa zaidi ya miezi miwili

BAADHI ya mashabiki wa klabu ya Simba, wameiomba Serikali kuongeza idadi ya mashabiki watakaoruhusiwa kuingia viwanjani mara baada ya Ligi Kuu Tanzania Bara kurejea.

Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alitangaza utaratibu wa mechi kuchezwa kwa vituo pindi ligi zikirejea lakini pia kuruhusu idadi ya mashabiki wasiozidi 20 kwa ajili ya kushangilia.

Uamuzi huo ulitangazwa kama miongoni mwa hatua za kukabiliana na ugonjwa wa Covid19 unaosababishwa na virusi vya Corona

Akizungumza na Mwanaspoti Mtendaji Mkuu wa Tawi la Simba la Wekundu wa Terminal la Ubungo  Justine Joel amesema, ni vyema Serikali iliangalie suala hilo la mashabiki 10 wa kushangilia kuingia uwanjani kwa kuwa ni wachache  sana.

Anasema, licha ya ligi kusemekana kuchezwa bila ya mashabiki lakini kwa idadi hiyo ni ndogo sana, hivyo wajitahidi waongeze walau wafike watu 150 yaani kwa kila kundi la Ngoma liwe na watu 50 hivyo waruhusu makundi matatu kwa kila timu.

 "Timu mgeni na timu mwenyeji wakipewa nafasi hiyo ya vikundi vitatu vya Ngoma ambavyo vinakuwa na wanakikundi 50 hivyo mechi moja itakuwa imeingiza watu 300 ambao hata wakikaa mita 200 au 300 watakuwa mbalimbali na janga hili la Corona," alisema Joel

Joel anasema, watanzania wanatambua ugonjwa huo kuwa upo na ndio maana katika katika maisha ya kawaida uraiani wanapanda daladala kwa idadi ya viti tofauti na zamani.

"Ugonjwa huu upo, na cha kushangaza sio wa kuisha leo wala kesho unaonekana utakuwa endelevu hivyo hatuna budi kuyaendeleza maisha huku tukijikinga kwa kufuata maelekezo ya Serikali na viongozi wa wizara ya Afya," alisema Joel

Tayari hadi sasa timu mbalimbali zimeanza kuingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya kumalizia lala Salama iliyosalia, baada ya kukaa nyumbani kwa takribani miezi miwili kupisha kuenea kwa virusi hivyo.

Serikali ilitangaza vituo viwili hapa nchini Dar es Salaam kwa ajili ya kombe la FA na Ligi Kuu huku Jijini Mwanza Daraja la kwanza na la pili.