Mashabiki 22,990 walishuhudia Simba, Yanga

Muktasari:

Idadi hiyo inakuwa ndogo tofauti na ilivyozoeleka kwa ukubwa wa mechi hiyo ambayo inakutanisha mashabiki wengi licha ya kutakiwa mashabiki 30,000 pekee.

Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza mapato yaliyopatikana kwenye mechi ya pili ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ni Sh269 milioni ambapo Simba iliichapa Yanga mabao 4-1 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumapili Julai 12, 2020 awali Serikali ilitangaza mashabiki 30,000 pekee ndio wataweza kuingia kutazama mchezo huo lakini leo Julai 14 TFF imesema watu 22,990 ndio waliingia kwa tiketi ambazo mapato yake ya jumla ni Sh269 milioni.

Taarifa ya TFF imesema fedha hizo zimekusanywa katika viingilio vya mlangoni, ambapo baada ya mgawanyo wote ikiwamo kodi, gharama za uwanja na makato mengineyo, Simba na Yanga zitagawana nusu kwa nusu ya fedha itakayosalia.

Katika mchezo huo kiingilio cha chini kilikuwa Sh 10,000, 20,000, 25,000 na cha juu kilikuwa Sh 30,000.

TFF imesema tiketi 93 za jukwaa kuu (VIP A) ziliuzwa na kuingiza Sh 2 milioni VIP B ziliuzwa tiketi 1,520 na kuingiza Sh 38 Milioni.

“VIP C ziliuzwa tiketi 1454 na kuingiza Sh 29 milioni na tiketi za bei ya chini ziliuzwa 19,923 na kuingiza Sh 199.2 Milioni” taarifa ya TFF imeeleza

Serikali iliruhusu mashabiki wachache licha ya Uwanja kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 kutokana na tahadhari zilizowekwa na Wizara ya Afya kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa corona.