Mashabiki, Mo Dewji na msimu mpya England

Saturday September 12 2020

WIKI hii imeshuhudia mjadala mkubwa –hasa katika mitandao ya kijamii, mara baada ya klabu ya Simba kumtangaza Barbara Gonzalez, kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wake.

Barbara anachukua nafasi ya Senzo Masingiza ambaye sasa anatumika katika klabu ya Yanga. Uteuzi huu haukuwa umetarajiwa na wengi na mimi ni miongoni mwa walioshtushwa na uteuzi huo.

Hata hivyo, katika mambo haya ya mijadala; kuna mambo mawili ambayo nimejifunza katika miaka ya karibuni. Jambo la kwanza ni kutambua endapo unaweza kushinda huo mjadala endapo utaingia na la pili ni kuangalia nini hasa kilichomo kwenye mjadala husika. Kwenye mjadala, ni muhimu kujua kama utashinda kwa sababu kuingia katika mjadala unaojua hutaweza kushinda ni kufanya jambo la kupoteza muda na wakati mwingine kupoteza marafiki na watu ambao pengine mnaheshimiana katika mazingira ya kawaida.

Kwa sasa, kwa washabiki wengi wa Simba, ni vigumu sana kuwa tofauti na Mohamed Dewji na ukaeleweka. Washabiki wanajua kwamba yale yote ambayo wamefanikiwa kuyapata katika kipindi cha miaka mitatu hadi minne iliyopita, kwa kiasi kikubwa yamesababishwa na uwepo wa mfadhili huyo.

Ninawafahamu washabiki wa mpira na ninaelewa kwamba saikolojia yao inaathiriwa na jambo moja kubwa; matokeo ya uwanjani. Ili mradi Simba inashinda na mashabiki kufurahi, hakuna shabiki atakayetaka jambo jingine zaidi ya hilo.

Inajulikana kwamba suala la uuzwaji wa klabu ya Simba haujakamilika. Inajulikana pia kwamba Mohamed hajatoa zile bilioni 20 zitakazomwezesha kumiliki Simba kwa asilimia 49. Jambo moja kubwa ambalo viongozi wa Simba hawajaweza kuliweka vizuri kwa umma –ingawa inaonekana mashabiki wa klabu hiyo wanalielewa japo si kwa namba na maelezo rasmi, ni kwa vipi Mo ni muhimu kwa Wekundu wa Msimbazi.

Advertisement

Ninafahamu kwamba Simba inalipa mishahara ya wachezaji na wafanyakazi wengine inayozidi Sh.300 milioni kwa mwezi. Uwezo wa klabu kukusanya fedha kupitia viingilio na wadhamini wengine hauzidi Sh.200 milioni kwa mwezi. Hii maana yake ni kwamba klabu inahitaji walau Sh.100 milioni kila mwezi kutoka kwa Mo ili ilipe mishahara.

Kiasi hicho hakijumuishi gharama za kusajili wachezaji na kuwalipia kwa ajili ya mambo tofauti ikiwamo vibali vya kazi, nyumba za kuishi na matibabu pale wanapokuwa wanaumwa.

Hizi ni gharama ambazo kimyakimya Mo anazibeba kabla hata hajakabidhiwa timu. Hii ina maana kwamba endapo Dewji ataacha kuwa mfadhili leo, Simba itaanza kupata taabu ya kulipa mishahara ya wachezaji wake katika mwezi wa kwanza tangu aondoke. Hapo sijazungumzia usajili wa nyota mahiri na matumizi mengine.

Uwepo wa Dewji ndani ya Simba una faida pia ya kuvutia wachezaji mahiri pale watakapojua kwamba wanatakiwa na timu inayomilikiwa na milionea na hawatakuwa na tatizo la mishahara.

Mashabiki wa Simba wanajua tatizo la mishahara likianza, klabu yao huwa na hali gani. Mashabiki hao wanajua kwamba wakishindwa kusajili nyota wa bei mbaya, hawataweza kutamba mbele ya mahasimu wao – Yanga.

Kwa hiyo, mjadala wa aina yoyote unaoonyesha kwamba Mo hana faida kwa Simba, hauwezi kupokewa vema na mashabiki.

Suala la pili linahusu kilichomo ndani ya mjadala. Katika dunia ya kisasa, kuna mambo yanayoendana na usasa. Ninapozungumzia usasa nazungumzia masuala kwa mfano ya kusaidia watu wanaoitwa wa makundi ya pembezoni. Makundi haya yanajumuisha watu kama wanawake, walemavu, vijana na watu wengine ambao kwa sababu za kihistoria tu, hawakuwa wakipewa nafasi kubwa huko nyuma. Klabu za mpira ni miongoni mwa zile ambazo mfumo dume umetamalaki sana.

Barbara ni mwanamke kijana. Anaangukia katika kundi la watu wanaoweza kuitwa wa pembezoni. Mtu aliye mwanamume mtu mzima, huonekana ana tatizo wakati anapokosoa uteuzi wa mmoja wa watu wanaowekwa katika kundi hili la wale ambao hawakubebwa na mfumo.

Unaweza kuwa na mtazamo hasi lakini kwa sababu aliyepewa nafasi ni mtu anayetoka katika makundi maalumu, wakati mwingine busara ni kuunga mkono au kupinga kwa kukaa kimya. Hili ni somo ambalo nimelisoma vizuri wiki hii.

Ligi Kuu England. Ni jambo la furaha kwamba Ligi ya EPL inarejea tena wikiendi hii. Nafahamu kwamba mashabiki wa soka duniani wanasubiri kwa hamu kipute.

Advertisement