Marealle afariki dunia

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho hilo,Dk Paul Marealle.

Dkt Marealle alifariki jana usiku Oktoba 13 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili huku chanzo cha kifo chake kikiwa bado hakijawekwa wazi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TFF iliyotumwa kwenye vyombo vya habari imesema Rais karia ametuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu jamaa, marafiki na wanafamilia wote wa mpira wa miguu kutokana na msiba huo mkubwa.

Karia amesema Dk Marealle alikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya mpira wa miguu na atakumbukwa kwa mambo mengi aliyoyafanya.

"Tumempoteza mtu ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika mpira wa miguu hasa katika eneo la Tiba,na mchango wake bado ulikuwa unahitajika sana", amesema Karia.

Hadi mauti inamkuta Dk Marealle alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF,Mwenyekiti wa kamati ya Tiba TFF na Mjumbe wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Mbali Na TFF klabu mbalimbali Ligi Kuu zimetuma salamu za rambirambi familia ya Marealle aliyekuwa mdau wa soka nchini.