Mara Paap! Vitani kuwakabili waajiri wao wa zamani

Monday February 11 2019

 

PARIS, UFARANSA.HAYA ule muda wa Ligi ya Mabingwa Ulaya umeshafika unaambiwa. Kesho Jumanne na keshokutwa Jumatano, mechi za raundi ya 16 bora kwenye michuano hiyo zitapigwa, lakini kitu kinachovutia ni kwamba kuna wachezaji kadhaa watakuwa na mtihani wa kuzikabili klabu zao za zamani kwenye hatua hiyo ya mtoano.

Hawa hapa, mastaa matata kabisa ambao watakabiliana na klabu zao za zamani katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

8. Klaas-Jan Huntelaar (Real Madrid vs Ajax)

Klass Jan Huntelaar alijiunga na Real Madrid mwaka 2009, lakini timu hiyo aliichezea kwa miezi sita tu. Aliondoka na kwenda akienda kutafuta timu itakayompa nafasi ya kucheza kutokana na kukutana na upinzani wa namba mbele ya Raul Gonzalez. Muda wake hapo, alifunga mabao manane katika mechi 20.

Lakini, hii si mara yake ya kwanza fowadi huyo wa Kidachi kuwakabili waajiri wake wa zamani. Mara yake ya kwanza aliwakabili kwenye hatua kama hiyo ya mtoano na alifunga mara mbili uwanjani Santiago Bernabeu. Sasa akiwa na umri wa miaka 35, Huntelaar pengine anaweza asiwe mshambuliaji tishio sana kwa Schalke, lakini bila ya shaka wanaweza kutumia bahati yake ya kuwafunga Real Madrid na wakamtumia kwenye mechi hiyo awapatie matokeo.

7. Matija Nastasic (Man City vs Schalke 04)

Beki wa Kiserbia, Matija Nastasic amejiandaa kiasi cha kutosha kuwakabili waajiri wake wa zamani wakati Manchester City itakapokabiliana na Schalke kwenye mechi ya hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Beki huyo alisema kitu kinachomfanya afurahi ni kupata nafasi ya kuwakabili Man City kwenye mikikimikiki ya Ulaya.

Nastasic aliwahi kuichezea Man City mechi 51 katika kipindi chake cha miaka miwili na nusu aliyodumu huko Etihad. Alihama kwenye timu hiyo Januari 2015 baada ya kushindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza na hapo alienda kujiunga na Schalke 04. Licha ya kwamba amekuwa akisumbuliwa na majeruhi mara kwa mara, staa huyo wa Serbia akiwa Man City alishinda ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2014, hivyo ana hamu kubwa ya kukabiliana nao.

6. Alvaro Morata (Juventus vs Atletico Madrid)

Kitu kisichoshtua wengi ni kwamba Alvaro Morata suala lake la kuondoka Chelsea lilikuwa likisubiri siku tu baada ya fowadi huyo kushindwa kufanya vyema huko Stamford Bridge. Kwa sasa fowadi huyo amekwenda kucheza kwa mkopo Atletico Madrid na ile ghafla tu atawakabili waajiri wake wa zamani Juventus kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kuwakabili Juventus kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya itakuwa mara ya kwanza kwa Morata kuikabili timu yake ya zamani baada ya kuwahi kutamba na timu hiyo kuanzia mwaka 2014 hadi 2016. Katika kipindi chake alichokuwa kwenye kikosi hicho, Morata alifunga mabao 27 katika mechi 93. Alishinda mataji mawili ya Serie A, mawili ya Coppa Italia na Supercopa Italiana na alicheza mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo Juve ilichapwa na Barcelona mwaka 2015. Kinachosubiriwa ni kuona kama Morata atafanya kitu tofauti katika mechi hiyo akiwakabili waajiri wake wa zamani.

5. Mario Mandzukic (Atletico Madrid vs Juventus)

Mechi ya Atletico Madrid dhidi ya Juventus itashuhudia mastaa kadhaa wakicheza dhidi ya timu zao za zamani. Mario Mandzukic wa Juventus atakwenda kumenyana na klabu yake ya zamani na hakika mechi hiyo itakuwa ya vuta nikuvute.

Straika huyo wa Croatia amecheza kwa msimu mmoja tu huko Atletico, lakini mashabiki bado wana kumbukumbu naye nzuri kutokana na uwezo wake wa kufunga hasa katika mechi ile ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya mahasimu wao Real Madrid. Katika msimu huu, Mandzukic alifunga mabao 20 katika mechi 43.

Miaka minne baadaye, Atletico sasa itakwenda kumenyana na straika kipenzi cha mashabiki wao, Mandzukic atakapokuwa upande wa Juventus katika mechi ya hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Atletico itaingia uwanjani kwenye mechi hiyo wakiwa na presha kubwa baada ya juzi Jumamosi kumkabili staa wake wa zamani Thibaut Courtois kwenye La Liga na wakachapwa 3-1 na Real Madrid. Wataweza kumkabili Mandzukic.

4. Xherdan Shaqiri (Bayern Munich vs Liverpool)

Xherdan Shaqiri anaonekana kufurahia wakati wake huko Liverpool. Staa huyo wa Uswisi msimu huu yupo kwenye vita kubwa ya kuhakikisha anaisaidia Liverpool kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England, ambapo itakuwa historia kubwa kwao.

Lakini, Shaqiri atakuwa na njaa tena ya kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuwahi kufanya hivyo alipokuwa na Bayern Munich, kipindi hicho akiwa kinda mwaka 2013. Shughuli ya Shaqiri ni kwamba kwenye hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu atakwenda kuchuana na Bayern Munich, timu ambayo aliwahi kuichezea na ndiyo iliyomfanya kuwa na medali ya ubingwa wa taji hilo. Mechi baina ya Liverpool na Bayern Munich inatajwa kuwa moja ya zile zitakazokuwa na mvuto mkubwa kwenye ligi hiyo ya mabingwa Ulaya msimu huu, lakini Shaqiri akiwa na mtihani mzito wa kwenda kuwakabili waajiri wake wa zamani katika mechi hiyo huko Allianz Arena.

3. Leroy Sane

(Schalke 04 vs Man City)

Katika mechi ambayo Klaas-Jan Huntelaar alifunga mbili dhidi ya Real Madrid, kinda Leroy Sane alicheza kwa mara ya kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na jezi za Schalke.

Kipindi hicho, Sane alikuwa na umri wa miaka 19 na kwa ubora wake wa uwanjani, alifunga bao pia kwenye ushindi wa 4-3 na hivyo kuifanya mechi yake ya kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kuwa na kumbukumbu ya kipekee.

Miaka minne baadaye, Schalke inakwenda kukabiliana na mtu hatari waliyemtengeneza wenyewe wakati itakapowakabili Manchester City kwenye hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, timu ambayo ndiyo anayoitumikia Sane kwa sasa.

Sane ni mmoja kati ya mawinga wanaohofiwa kwelikweli kwa sasa huko kwenye Ligi Kuu England na bila shaka atahamishia kiwango chake hicho bora kabisa katika mikikimikiki ya Ligi Kuu England atakapowakabili waajiri wake wa zamani.

2. Samuel Umtiti

(Lyon vs Barcelona)

Anatajwa kama mmoja wa mabeki wa kati bora kabisa duniani kwa sasa. Samuel Umtiti amekuwa mgumu ndani ya uwanja na kwenda mechi hiyo ya hatua ya 16 bora ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Umtiti atarudi kuwakabili waajiri wake wa zamani, Lyon.

Umtiti, aliibukia kwenye akademia ya Lyon na mwaka 2016 alikwenda kujiunga na Barcelona. Tangu wakati huo, Umtiti alishinda taji la Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Ufaransa na amekuwa na kiwango bora kabisa katika kikosi cha Barcelona akitajwa kuwa mmoja wa mabeki mahiri kabisa duniani.

Kwenye mechi hiyo, Umtiti atakwenda kuwakabili marafiki zake wa zamani kama Nabil Fekir na Anthony Lopes, ambao walikuwa pamoja. Shida amekuwa akisumbuliwa na majeruhi kwa siku za karibuni na haifahamiki kama atakuwa fiti kucheza mechi hiyo.

1. Angel di Maria

(Man United vs PSG)

Huko Old Trafford mashabiki wa soka watamshuhudia supastaa, Angel di Maria akirudi kuikabili timu yake ya zamani, Manchester United akiwa na kikosi chake cha sasa cha Paris Saint-Germain. Di Maria aliondoka Man United mwaka 2015 baada ya kuwa na msimu wa hovyo kwenye kikosi hicho. Lakini, tangu alipotua Ufaransa kwenye kikosi cha PSG, Muargentina huyo amekuwa moto kwelikweli.

Kitu kinachosubiriwa ni kuona mashabiki watampokea mchezaji huyo kwa staili gani kama watamshangilia kama walivyofanya kwa mastaa wengine kama David Beckham na Cristiano Ronaldo au atakumbana na kelele za kuzomewa. Kwenye mechi hiyo, PSG haitakuwa na huduma ya supastaa wake, Neymar, lakini kuna wasiwasi pia huenda Edinson Cavani akakosa mechi hiyo.

Advertisement