Breaking News
 

Mapya yaibuka penalti ya Chirwa

Friday January 12 2018

OBREY CHIRWA: Staa huyu Mzambia ndiye kinara wa

OBREY CHIRWA: Staa huyu Mzambia ndiye kinara wa mabao ndani ya Yanga  akiwa amefunga mara sita kwenye mechi za Ligi Kuu Bara. Alikosa penalti yake ya kwanza klabuni hapo ambayo  nyuma ya pazia mengi yamejificha.  Penalti hiyo imeiondosha Yanga kwenye Kombe la Mapinduzi. 

By THOBIAS SEBASTIAN

UNGUJA. YAWEZEKANA Yanga ilijiamini kuwa historia ya staa wao, Obrey Chirwa  ya kufunga penalti ingeweza kuwabeba katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya URA lakini mambo yalikwenda tofauti na sasa mapya yameibuka. Mwanaspoti limebaini kuwa kitendo cha staa huyo kutoshiriki mazoezi ya kupiga mikwaju ya penalti katika mazoezi yao ya mwisho kabla ya  mechi yao na URA, ndiyo sababu iliyochangia Chirwa kupiga penalti ya ovyo iliyoigharimu timu yake nafasi ya kutinga fainali.

Yanga iliondoshwa na URA katika nusu fainali kwa penalti 5-4 na  kwa upande wa Yanga aliyekosa mkwaju huo ni Chirwa. Katika mazoezi hayo ya mwisho kabla ya mechi Yanga walifanya katika  uwanja wa Bumbwusudi nje kidogo ya mji wa Unguja na baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo walipiga mikwaju ya penalti lakini Chirwa hakuwepo.

Wachezaji Papy Kabamba Tshishimbi, Hassan Kessy, Gadiel Michael na Raphael Daud ambao walipiga penati za Yanga dhidi ya URA na kufunga alikuwa tu wakifanya mwendelezo wa kile walichokifanya mazoezini kwani nako walikuwa wakitupia kama kawa.

Chirwa kwa upande wake alitua visiwani hapa wakati tayari maandalizi ya mchezo huo wa nusu fainali yakiwa yamekamilika lakini aliwekwa kwenye orodha ya wachezaji watakaocheza kutokana tu na makali  yake kwenye mechi za Ligi Kuu ambazo hata hivyo mara ya mwisho kucheza ilikuwa mwishoni mwa Novemba mwaka jana.

Nyota huyo alikuwa kwao Zambia kushughulikia matatizo  ya kifamilia na taarifa zilidai kwamba alikuwa na mgomo baridi akishinikiza kupewa malipo yake jambo ambalo alikanusha.

Akielezea uamuzi wake wa kumpanga Chirwa wakati hakuwa fiti, aliyekuwa kamanda katika benchi la Yanga, Shadrack Nsajigwa alisema kama Chirwa alicheza akiwa hayupo fiti au alikuwa fiti, ni mambo ambayo yapo ndani ya timu na si kila kitu kinaweza kuongolewa na kuwekwa wazi. “Chirwa alicheza kama wachezaji wengine licha ya kwamba hakuwa na timu tangu mashindano yanaanza hilo ndilo ambalo naweza kusema,” alisema Nsajingwa. Sakata la Chirwa linafanana na lile na beki Mghana wa Simba, Kwasi ambaye alipangwa kwenye mchezo dhidi ya URA licha ya kwamba hakufanya mazoezi ya mwisho na wenzake.