Maproo hawa walikiwasha kweli kweli 2019-20

Muktasari:

Nilikuwa nikifuatilia kwa karibu Ligi Kuu Bara msimu huu na nakuletea kikosi cha wachezaji wangu 11, ambao wamefanya vizuri tangu kuanza kwa msimu mpaka sasa akiwa imebakia mizunguko kumi kabla ya kumalizika.

MAISHA bila ya mechi za mpira wa miguu yamekuwa magumu mno hasa kwa wapenzi wa soka katika maeneo yote duniani. Hakuna tena kukaa katika vikundi mbalimbali tukiwa makazini, vijiweni na hata maeneo mengine kubishana kuhusu soka na michezo mengine ambayo yote imesimamishwa.

Sababu kubwa iliyokwamisha michezo yote hii duniani ni kuhusiana na ugonjwa wa Corona.

Nilikuwa nikifuatilia kwa karibu Ligi Kuu Bara msimu huu na nakuletea kikosi cha wachezaji wangu 11, ambao wamefanya vizuri tangu kuanza kwa msimu mpaka sasa akiwa imebakia mizunguko kumi kabla ya kumalizika.

NURDIN BAROLA

Ni kipa chaguo la kwanza katika kikosi cha Namungo ambao walimsajili msimu huu kutokea Biashara United, yalikuwa mapendekezo ya kwanza ya kocha, Thierry Hitimana ambaye alimtaka mchezaji huyo ambaye msimu uliopita alimfundisha katika timu hiyo.

Msimu huu amecheza mechi zaidi ya 25, kati ya 28 ambazo Namungo wamecheza kwenye ligi na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 25, huku wao wakifunga 34, mpaka ligi inasimama kupisha janga hili na corona.

Barola amekuwa na upungufu kadhaa ikiwemo kuruhusu mabao yanayotokana na mipira ya krosi na kutokuwa na maelewano mazuri muda mwingine na mabeki wake. Lakini kiujumla ni moja ya wachezaji wazuri wa kigeni waliocheza vyema katika eneo hilo la kipa.

NICOLAS WADADA

Ukiachana na kiungo wa Simba Claytous Chama ambaye ametoa pasi nyingi za mabao kwa wachezaji wenzake wa Simba, anayefuatia ni beki wa kulia wa Azam ambaye naye amefanya kazi nzuri katika kuanzisha mashambulizi kwa kutoa pasi za mwisho zisizo pungua kumi kwa wenzake kufunga licha ya kwamba anacheza kama mlinzi wa kulia.

Wadada mbali ya ubora huo alionyesha ubora katika kuanzisha mashambulizi amekuwa muhimili imara katika safu ya ulinzi ya Azam kwani amecheza mechi nyingi katika kikosi hicho katika kiwango bora na kuwazuia mawinga wasumbufu.

Wadada ambaye pia yupo katika kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda, amekuwa nguzo imara katika kikosi hicho na muda wote tangu aliposajiliwa na klabu hiyo misimu miwili iliyopita amekuwa kwenye kikosi cha kwanza kutokana na ubora na kiwango cha hali ya juu alichonacho.

BRUCE KANGWA

Beki wa kushoto wa Azam, si mrefu lakini ukiangalia aina yake ya kucheza ni mchezaji ambaye muda wote yupo na utimamu wa mwili kwa maana ya kuwa fiti na mawinga au washambuliaji wa timu pinzani ambao wanacheza upande wake ni ngumu kumpita kirahisi kwani amekuwa imara.

Kangwa ni mzuri katika kuzuia mashambulizi hasa upande wake na kuna muda amekuwa akitoa msaada kwa mabeki wa kati kama watakuwa wamefanya makosa huku pia akihusika katika mabao kadhaa ya Azam msimu huu kutokana na kupanda mbele kusaidia mashamulizi na kupiga krosi zake matata.

Kutokana na umahiri huo wa kutimiza majukumu yake ya kwanza ya kukaba na kuwa na faida nyingine ya kuanzisha mashambulizi, Kangwa anaingia katika kikosi changu wachezaji wa kigeni waliofanya vizuri msimu huu mpaka sasa katika ligi.

JEAN MUGIRANEZA

Huyu aliwahi kucheza pia Azam FC. Kiasili ni kiungo mkabaji lakini tangu KMC walivyomsajili msimu huu ametumika kama beki wa kati ambaye amekuwa akifanya kazi nzuri licha ya kwamba timu yao kuwa katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi. Muda mwingine amekuwa akisumbuliwa na majeraha.

Mugiraneza amekuwa akicheza vyema katika eneo hilo la beki wa kati wa KMC akiokoa mipira mingi ya krosi na ile ya hatari.

Katika mechi ya KMC waliyokuwa nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar, walishambuliwa mara kwa mara kwa mipira mingi ya krosi na zile pasi za kupenyeza lakini Mugiraneza alikuwa katika kiwango bora na kuweza kuzuia mianya na nafasi hizo ambazo wapinzani wao walitengeneza.

Katika nafasi hii ya beki wa kati kama atakosekana Mugiraneza wa KMC, ambaye amekuwa na kiwango kizuri msimu huu lakini majeraha yamekuwa yakimsumbua, anaweza kuingia nafasi ya beki wa kati wa Simba, Pascal Wawa ambaye naye amekuwa nguzo na muhimili katika ngome ya ulinzi ya timu yake kwa muda wote msimu huu.

LAMINE MORO

Beki wa kati wa Yanga ambaye msimu huu mbali ya timu hiyo kukutana na msukosuko mbalimbali ya kifedha na hata kuna wakati kuamua kutimka kurudi kwao, ameweza kucheza katika kiwango bora kwa kuwazuia washambuliaji wasumbufu kama John Bocco, Meddie Kagere, Obrey Chirwa na wengineo kushindwa kufunga bao mbele yake.

Moro amekuwa beki mahiri na chaguo la kwanza katika kikosi cha Yanga na nadra sana kumuona akikosekana katika mechi yoyote ile bila ya kuwepo sababu ya msingi huku walinzi wengine wakiwa wanapishana kama Said Juma Makapu, Kelvin Yondan, Ally Sonso na Andrew Vicent ‘Dante’.

Uwepo wa Moro katika mechi nyingi za Yanga katika eneo lao la ulinzi linakuwa salama kutokana na umahiri wake wa kucheza mipira ya vichwa, kuokoa mipira ya chini lakini ni mzuri katika matumizi ya nguvu na hata umbile lake kumbeba kwani ni moja ya wachezaji wenye maumbile makubwa ya kibeki.

Katika eneo hili kama akikosekana Moro ambaye ni nguzo katika kikosi cha Yanga jambo ambalo kwenye mechi ambazo anakosekana timu hiyo kutokuwa salama anaweza kuingia beki wa kati wa Azam, Yakub Mohammed ambaye na amekuwa kwenye kiwango kizuri.

PAPY KABAMBA TSHISHIMBI

Nahodha wa Yanga hana mpinzani katika eneo hili la kiungo mkabaji kwani si msimu huu tu kucheza katika kiwango bora na cha juu katika miaka mitatu yote aliyoichezea timu hiyo amekuwa katika kiwango bora na muhimili akiweza kushindana na viungo wote wa timu pinzani.

Tshishimbi huwa hana mechi ndogo wala kubwa kwani akikutana na viungo wa Simba, Jonas Mkude na wengineo au wale wa Azam, Salum Abubakar na wengineo huwa anataka kuonyesha ubora wake na mara nyingi hufanikiwa kucheza katika kiwango bora dhidi yao hata kama timu yake itashindwa kupata ushindi.

Kiujumla Tshishimbi anatimiza majukumu yake ya kukaba vyema lakini muda mwingine huanzisha mashambulizi kwa washambuliaji kwa maana ya kupiga pasi ndefu na fupi ambayo huzaa matunda kwa maana ya kufunga mabao na hata muda mwingine hufunga mwenyewe mabao.

SERGE TAPE

Winga wa KMC alikuja nchini mwanzoni mwa msimu huu kwa ajili ya kujiunga na kikosi cha mabingwa watetezi wa ligi, Simba ambao walimkaushia wakamuunganisha na timu aliyopo sasa.

Anacheza kama winga lakini amekuwa akifanya vyema katika majukumu yake kwa kufunga mabao na pia kutengeneza nafasi za kufunga kwa washambuliaji wengine wa timu hiyo kama Hassan Kabunda, Sadala Lipangile na wengineo.

Muda mwingine Tape hushuka chini kusaidia kukaba na mpaka ligi inasimama ameingia katika kikosi cha wachezaji wa kigeni waliofanya vyema na huenda akaongezwa mkataba mwingine wa kusalia katika kikosi hicho baada ya ule wa awali wa mwaka mmoja kumalizika mwisho wa msimu huu.

INNOCENT EDWIN

Mshambuliaji wa Biashara United, raia wa Nigeria ambaye muda mwingine hucheza katika eneo la kiungo msimu uliopita alizifunga Simba na Yanga lakini msimu huu ameendeleza moto wa kuifunga tena timu kubwa nyingine hapa nchini ambayo ni Azam FC.

Edwin licha ya kucheza katika timu ya Biashara United, ambayo inaonekana kuwa timu ya daraja la kati lakini amefunga mabao muhimu katika kikosi hiko kama hayo dhidi ya timu kubwa na hata zile timu za madaraja yao kama Mbeya City ambao aliwafunga moja ya bao bora kabisa msimu huu.

MEDDIE KAGERE

Hakuna shaka wala mpenzi yoyote wa soka asiyetambua uwezo wa mshambuliaji huyu wa Simba, ambaye msimu uliopita alikuwa mfungaji bora kwa kumaliza Ligi Kuu Bara akiwa amefunga mabao 23, lakini msimu huu pia anaongoza katika mbio za ufungaji akiwa kinara kwa kufunga mabao 19, mpaka sasa.

Kagere amekuwa akifunga mechi kubwa na ngumu za ligi kama dhidi ya Yanga, Azam na nyingine lakini haiishii hapo kwani hufunga hata katika mashindano mengine timu yake ikiwa inacheza.

Mbali ya uwezo huo mkubwa wa kufunga mabao mengi hapa nchini ambao Kagere ameonyesha amekuwa ni nguzo muhimu katika kikosi hiko cha Simba kwani anapokuwa uwanjani mabeki wa timu pinzani ambao humkaba huwa makini naye wakati wote jambo ambalo muda mwingine hutoa nafasi kwa wachezaji wengine pia kufunga.

BIGIRIMANA BLAISE

Mshambuliaji wa Namungo alisajiliwa akitokea Alliance ya Mwanza, lakini mpaka sasa ameifungia timu yake mabao sita, na kuwa katika mbio za kuwania tuzo ya mfungaji bora msimu huu.

Ubora huo wa kufunga mabao wa Blaise umewafanya hata baadhi ya viongozi wa timu za Simba, Yanga na Azam kuvutiwa na mchezaji huyo na hata kumtamani kumsajili mara baada ya ligi kumalizika msimu huu.

Katika nafasi hii kama akikosekana Blaise anaweza kucheza kiungo mahiri wa Simba, Mzambia Clatous Chama ambaye mbali ya kutoa pasi nyingi za mabao msimu huu lakini muda mwingine hufunga mwenyewe akitupia mabao matano.

BERNARD MORRISON

Winga Mghana wa Yanga, amewahi kucheza klabu mbalimbali kubwa Afrika kama DC Motema Pembe, AS Vita za Congo na Orlando Pirates ya Afrika Kusini muda mfupi tu aliokuwa nchini ameingia katika kikosi cha wachezaji wa kigeni waliofanya vizuri.

Morrison akiwa na kikosi cha Yanga ameweza kutengeneza nafasi za kufunga kwa wachezaji wenzake na muda mwingine hutoa burudani kwa uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira.

Ubora wa Morrison ameonyesha pia katika kufunga kwani mpaka ligi inasimama amefunga mabao matatu likiwemo lile tamu alilofungwa kwa ‘frii-kiki’ kali dhidi ya Simba katika ushindi wa 1-0.