Mapema tu Kagera waivamia Biashara

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema tayari kikosi kimeshatua mkoani Mara kwa kazi moja tu, kusaka ushindi ili kuanza vyema Ligi.

KIKOSI cha Kagera Sugar tayari kipo mjini Musoma kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Biashara United, lakini unaambiwa kazi ni moja tu kusaka pointi tatu.

Timu hiyo ya mjini Bukoba msimu uliopita ilikuwa na matokeo yasiyoridhisha, jambo ambalo ni tofauti na msimu huu kutokana na usajili ilioufanya wa nyota wenye uwezo.

Kagera Sugar inatarajia kushuka uwanjani kesho Jumamosi kuwakabili Biashara United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma mkoani Mara.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema tayari kikosi kimeshatua mkoani Mara kwa kazi moja tu, kusaka ushindi ili kuanza vyema Ligi.

Alisema anaamini mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na wapinzani walivyojipanga pamoja na kuwa uwanja wao wa nyumbani, lakini anaamini kutokana na uwezo wa nyota wake watafanya vizuri.

“Sina majeruhi, nimekuja na wachezaji wote kwa nia ya kusaka ushindi, hii ni Ligi najua wapinzani wamejipanga lakini tutakuwa makini kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema Maxime.

Kwa upande wao nyota wa timu hiyo, kiungo Abdalah Seseme na Evaligestus Mujwahuki walisema kwa mazoezi waliyoyafanya ikiwamo mechi za kirafiki zimewapa nguvu hivyo matarajio yao ni ushindi.

“Tutaenda kushambulia mwanzo mwisho kwa sababu nia yetu ni pointi tatu, tumejipanga vizuri na kila mmoja ana ari na morali kutokana na maandalizi tuliyoyafanya,” alisema Seseme ambaye kabla ya kutua Kagera aliwahi kuchezea Simba na Stand United..