Manyama Kawachoma mkuki Yanga na Simba

Muktasari:

Miaka 5 imepita tangu Edward Manyama aichezee Yanga kwa mara ya mwisho kabla ya kuondoka

SIFA kubwa ya beki ni kulinda lango lake lisipatwe na madhara, lakini anapokuwa na uwezo wa kufunga huwa inamuongezea vitu vya ziada uwanjani.

Pamoja na mambo mengine sifa nyingine ya beki hasa wa kati ni kuwa na uwezo wa kucheza katika ubora wa juu kila mechi, uwezo wa kutilia umakini jambo moja, kuongea, kuwapanga na kuwahamasisha wenzake ili wasijisahau.

Pia, beki anatakiwa kuwa na akili, machale, hisia na kutambua hatari kabla haijatokea na kujipanga kwenye nafasi za kuzuia pasi zisifike kwa mshambuliaji.

Beki anatakiwa kuwa shujaa. Atahitajika kuingiza mguu au kichwa mahali ambapo anaweza kuumia (usiogope kuumia), pia kupata mwenza sahihi wa kucheza naye (combination).

Katika kikosi cha Namungo FC kwa sasa yupo Edward Manyama ambaye sio tu anahakikisha lango lake lipo salama, pia amekuwa akihakikisha lango la wapinzani lipo shakani kwa namna anavyokwenda kushambulia na kufunga. Ni mmoja wa mabeki wachache ambao wamekuwa na mabao msimu huu kwenye Ligi Kuu Tanzania akifunga mabao mengi kuliko hata washambuliaji ambao ndio kazi yao ya kufunga.

WAULIZE YANGA

Bahati yao. Ndio maneno ambayo watakuwa walisema mashabiki wa Namungo FC baada ya sare ya mabao 2-2, Juni 24 katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa Mkapa kati ya Yanga na Namungo FC. Katika mchezo huo, hadi dakika ya 77 wenyeji Yanga ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na beki wa Namungo FC, Manyama aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Jukumu Kibanda.

Manyama alifunga mabao yake dakika ya 52 baada ya kona safi iliyochongwa na Hashim Manyanya, huku bao la pili akifunga dakika ya 70 kutokana na juhudi zake binafsi ya kutoka ngome ya Yanga. Mabao ya Yanga yaliwekwa kambani na David Molinga dakika ya 80 na lile la dakika za nyongeza.

“Wakati naingia katika mchezo ule kocha (Hitimana Thierry) aliniambia napaswa kwenda kupunguza kasi ya mashambulizi ya timu pinzani huku tukiwa tunafanya mashambulizi ya kushtukiza. “Nilipoingia nikagundua Yanga ina upungufu zaidi upande wa kulia, ndio maana kila mpira niliokuwa nikiupata nilikuwa napeleka upande ule,” anasema Manyama.

ZAO LA YANGA

Manyama aliwahi kuitumikia Yanga katika msimu wa mwaka 2012 mwishoni akitokea JKT Ruvu (JKT Tanzania) hadi 2015, lakini kutokana na ushindani wa namba alitolewa kwa mkopo tena Ruvu hadi mkataba wake ulipomalizika.

“Yanga ilishindwa kuwa wavumilivu wakati nasajiliwa, maana umri wangu ulikuwa mdogo na nilisajiliwa na kina Said Makapu pamoja na Pato Ngonyani lakini ilionekana kutaka mafanikio ya haraka.”

Manyama pia amewahi kuichezea Ruvu shooting na Geita Gold ambayo ilifungiwa na kushushwa daraja kutokana na kosa la upangaji wa matokeo, sambamba na timu ya JKT Oljoro, JKT Kanembwa na Polisi Tabora.

MABAO YAKE

Manyama alitua kwenye kikosi hicho katika dirisha dogo la usajili mwezi Januari, mwaka huu, na mara nyingi alikuwa akianza kama mchezaji wa akiba kwa kocha Hitimana.

Tangu aitungue Yanga amekuwa gumzo na kama amefunguliwa baraka za kufumania nyavu kila baada ya michezo kadhaa amekuwa akifunga kama vile anacheza nafasi ya ushambuliaji wakati kazi yake ni ulinzi.

Bao lake la tatu alilifunga kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons mchezo uliofugwa Uwanja wa Majaliwa, Julai 18, akiitanguliza Namungo dakika ya 43 kisha Samson Mbangula akisawazisha dakika ya 64.

Manyama ndiye aliyeiwezesha Namungo kupenya fainali ya Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) kwa bao la dakika ya 79 katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Julai 11 dhidi ya Sahare All Stars ya Ligi ya Daraja la Kwanza (FDL).

Ameingia kwenye kitabu cha wachezaji waliowahi kufunga katika michezo ya fainali ya ASFC baada ya kufunga bao moja katika kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Simba iliyopata mabao kupitia kwa Luis Miquissone na John Bocco, mchezo uliochezwa Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.

Mchezaji huyo aliyebakiza miezi minne ili mkataba wake ufikie kikomo anasema anafunga kwa sababu anapenda kushambulia ndio maana kila wakati anakuwa kwenye lango la wapinzani.