Manula aweka rekodi ya kibabe Ligi Kuu

Muktasari:

Manula alijiunga na Simba mwaka 2017 akitokea Azam FC ambayo aliitumikia kuanzia mwaka 2012 alipojiunga nayo akitokea Mkamba Rangers.

IKIWA kigezo cha kucheza idadi kubwa ya michezo bila kuruhusu nyavu kutikisika kitatumika, ni wazi kwamba nyota wa Simba, Aishi Manula ataibuka mshindi wa tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu msimu uliomalizika Jumapili, wiki iliyopita.

Hadi msimu unamalizika, Manula ndiye kipa ambaye nyavu zake hazikutisika katika idadi kubwa ya michezo ambapo amefanya hivyo katika jumla ya mechi 18.

Mechi hizo 18 ambazo Manula aliidakia Simba bila kufungwa bao lolote katika Ligi Kuu msimu huu ni dhidi ya timu za Prisons, Mbeya City, Ndanda, Singida, Kagera Sugar, KMC, Lipuli, Mwadui, Mtibwa, Azam, Biashara United na JKT Tanzania.

Wakati Manula akishika nafasi ya kwanza kwa kucheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa msimu huu, kipa anayeshika nafasi ya pili ni Daniel Mgore wa Biashara United ambaye amecheza jumla ya mechi 16 bila kufungwa bao.

Kipa wa Coastal Union, Soud Abdallah 'Dondola' yeye anashika nafasi ya tatu katika chati ya makipa waliocheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa ambapo amefanya hivyo katika jumla ya mechi 15 na anafuatiwa na Ally Mustafa wa Ndanda FC ambaye yeye amedaka jumla ya michezo 14 bila kufungwa bao.

Ukiondoa hao, wanaofuatia ni kipa wa Prisons, Jeremiah Kisubi ambaye amecheza mechi 13 bila nyavu zake kutikiswa akifuatiwa na Nurdin Barola wa namungo ambaye yeye nyavu zake hazijaguswa katika michezo 12 wakati kipa wa Polisi Tanzania, Mohamed Ally yeye amedaka katika mechi 11 bila kufungwa bao.

Kama atatwaa tuzo hiyo, Manula atakuwa anafanya hivyo kwa mara ya nne ambapo kabla ya msimu huu, aliwahi kuitwaa katika misimu ya 2015/2016, 2016/2017 na 2017/2018.

Manula angeweza kuweka rekodi ya kipekee kwa kuitwaa tuzo hiyo mara tano mfululizo ikiwa msimu uliopita ingetolewa kwani ndiye aliibuka kinara wa kucheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao ambapo alifanya hivyo katika michezo 18 ya Ligi Kuu msimu wa 2018/2019.