Manula alimfanya nini yule dogo msenegali katili?

Wednesday June 26 2019

 

By Luqman Maloto na Dk Levy

HUKO Kijiweni kuna majanga mazito baada ya chama la Watanzania, Taifa Stars, kuchapwa na Senegal kwenye mikikimikiki ya Afcon 2019.

Kama kawaida yake buana, Luqman akaanza kumtibua Dk Levy kwa maswali yake ya kizushi na hapo ndipo timbwili likaanza.

LUQMAN: DK Levy hasahasa aliyekutibua wikiendi iliyopita ni nani?

LEVY: Amunike na wabunge waliojazana kule Misri.

LUQMAN: Hivi wabunge kwa umahiri wao kwa kugonga meza bungeni na kusema “ndiooooo”, wanadhani ndio wanaweza kushangilia uwanjani na kuwapa mzuka wachezaji? Hivi hasahasa Amunike tulimkosea nini?

LEVY: Amunike bana. Alimwacha Mwantika kwa kuwategemea Morris na Nyoni. Sasa Morris alipoumia kamwita Mwantika na kumwanzisha mechi ya kwanza Nyoni akiota jua kwenye benchi. Sasa mwanzoni si angemuacha Nyoni kabisa? Wabunge wale wameacha suala la muhimu kwa taifa ambalo ni bajeti wameafuata kuuza sura kwenye piramidi.

Advertisement

LUQMAN: Sasa unisaidie kujua. Wabunge wameenda Misri kushangilia Taifa Stars au wamemsindikiza chapombe wa Taifa, Pierre Liquid?

LEVY: Yote sawa tu... Au kwa lugha nyepesi tunasema wapo huko kuunga mkono vipigo... Maana sihitaji nguvu ya Marehemu Sheikh Yahaya Hussein kutabiri kuwa tutabagazwa mechi zote. Wanatimiza neno kilio cha wengi sherehe.

LUQMAN: Usikate tamaa mwanaume. Senegal wametuotea kwa taabu sana. Algeria na Kenya tutawabagaza hawataamini. Hivi ulimuona yule janki wa Senegal aliyetupiga goli la pili? Sura ya mbuzi yule, anaitwa Krepin Diatta, anacheza ligi moja na Samatta, Ubelgiji. Anakiputa Club Brugge.

LEVY: Yule dogo ni jamii ya jini Makata au jini Maimuna. Hafai, mashuti ya vile hupigwa na wachawi, wanga, mashetani au vibwengo. Hivi lengo lake afunge au aue mtu? Mtu kama yule ndo maana halisi ya soka. Sisi tunachojua ni siasa, ndo maana kule Misri wamejaa wanasiasa kuliko mashabiki wa soka.

LUQMAN: Wa kumuuliza ni Manula, alimkosea nini yule janki katili? Kabla ya kumlaumu mpiga shuti, tumhoji Manula kwanza. Alimchokozaje? Alimwita sura mbaya akakasirika? Alimwambia ni mweusi sana akamtibua? Alimpora demu wake ndo akapiga lile shuti la kuua?

LEVY: Hilo nalo neno. Ila kuna wakati tulicheza vibaya mpaka tukawachanganya Wasenegali, wakawa hawaelewi tunacheza soka au singeli michano? Halafu jamaa kocha wao mkuu ni mzawa msaidizi wake wamempa beberu sijui la kutoka taifa gani.

LUQMAN: Sijakuelewa. Senegal walituchezesha Singeli au sisi Taifa Stars ndio tuliwachezea singeli mpaka Senegal wakadata? Unataka kuniambia Amunike aliwapa mbinu wachezaji wetu kuwachezea singeli Senegal ndio tungewafunga?

LEVY: Ukinitajia hilo jina la Amunike naona tano zingine zilee zinakuja kwa Algeria. ‘Enewei’ tusilalamike sana. Kwa sababu sisi ni Tanzania ya viwanda siyo soka. Kwanza pale Misri wamezoea kutesa watu. Kawaulize Waisrael na Mussa wao walichofanywa. Mpaka ‘Saa God’ akaingilia kati. Sisi ni nani tusiteswe?

LUQMAN: Yule janki handsome mayai Fei Toto kukabana na lile jitu baya li-Diatta, hujaona kama Taifa Stars tulikuwa tunamchezea mkia Shetani? Ukimuona Amunike mwambie sina tatizo na ile sura yake wala ukoo wake. Tatizo langu ni mipango ndani ya uwanja. Matokeo ya jana nimemwachia Mungu.

LEVY: Stars ya kwenye magazeti utadhani Hispania ile ya kina Iniesta. Lakini uwanjani kama timu ya Bongo Movie. Kila mtu anakimbia anavyojua. Zahera kamponza Amunike kumuaminisha kuwa Fei Toto ni kiungo mkabaji. Akakutana na jitu lenye sura na matendo ya kikatili. Lazima atoweke.

LUQMAN: Wewe si umeninyima namba ya Amunike? Basi mfikishie ujumbe Afcon sio mashindano ya talent show. Kule hatuendi kuonesha vipaji. Tumekwenda kupambana. Tangu amefika anapuyanga tu, mara amchukue huyu, kesho anamuacha. Anajaribujaribu. Hajui hasa anataka nini. Timu uwanjani haijulikani inacheza mfumo gani. Umenisaidia kusema Stars ilicheza singeli.

LEVY: Wabongo bana tunavyolalamika. Utadhani sio sisi tuliokaa miaka 39 bila kushiriki hizo fainali. ‘Nekti taimu’ tupeleke ‘Timu Kiba au Timu Diamond’. Hivi hebu tuwe ‘siriaz’ kidogo, wale wachezaji ndo waliogomea mazoezi mpaka wapate Dola 300? Kama ndo wale wakirudi watazitapika.

LUQMAN: Wamtapikie nani? Uliingia uwanjani wewe? Kucheza na ile Misenegali unaona ni kazi rahisi? Kwanza Dola 300 hazitoshi. Ngoja tujadili mambo yenye tija kwa afya ya nchi. Jux unamweka kundi gani kutemana na Vanessa Mdee?

LEVY: Achana na Jux kwanza. Hivi Haji Manara ulisikia alichoongea kabla ya mechi? Ujue simwelewi. Kalipa nauli kisha anaacha kutupa moyo akasema eti Stars kuifunga Senegal ni hisani kubwa ya Mungu.

LUQMAN: Kama hutaki kumjadili Jux na Vanessa, na mimi simjadili Haji. Misri wamewaacha Mkude na Ajibu wamempeleka Pierre Liquid halafu unamlaumu Manara. Badala ya kupeleka washangiliaji, mnapeleka wabunge. Wachezaji wakacheza kipweke, hata hawashangiliwi. Tungepeleka ile mijitu inayopiga ngoma dakika 90, Senegal wangedata na singeli yetu. Tuache hayo, tujadili mambo yenye tija kwa dunia, nasikia P Diddy kamchumbia ex girlfriend wa mtoto wake. Sijui pesa zinamvuruga yule mzee au ndo anazeeka vibaya?

LEVY: Mtu anayeelekea kwenye miaka 50 bila ndoa ni sehemu ya upungufu. Wala siwezi kushangaa ndo kina R Kelly hao. Mwenzake Jay Z amekuwa bilionea tayari yeye kawa babalea.

LUQMAN: Ila mrembo ni wa moto huyo. Ana miaka 22. Modo anaitwa Lori Harvey. Mtoto wa supastaa Steve Harvey. Ila alikuwa usingizi wa mtoto wa Diddy, Justin Combs. Kwa hiyo Diddy akimuoa, Justin atakuwa anamwita mama ex girlfriend wake. Kwa kifupi Diddy anataka kuoa mkwe wake. Nakushangaa wewe hapo Diddy kuwa role model wako.

LEVY: Siwezi kujivunia hulka za mtu sampuli ya Diddy. Nitake radhi aiseee kabla sijaagizwa utupwe ndani siku saba kama dadaako kipenzi Wema. Hivi wewe na Kajala mmeshaenda kumwona Wema? Unakumbuka 13 milioni lakini?

LUQMAN: Kajala muone vilevile. Sura nzuri, umbo mashallah, lakini ngoja nikae kimya tu. Tangu Wema atupwe nyuma ya nondo mpaka alipoachiwa, tuliona Aunty Ezekiel ndiye mwenye kuumia. Kila siku anampost Wema. Ila Wema mzinguaji kwa mikasa yake, ila ana roho nyepesi kutusaidia sisi akina vampire, akipata matatizo yeye, tunamnyonya damu. Tunamsengenya na kumng’ong’a.

LEVY: Kweli Wema ni dadaako kipenzi kabisa, maana umeongea kwa uchungu mpaka machozi yamenilengalenga.

LUQMAN: Ujue Kajala si wa mchezomchezo eti.

LEVY: Hebu niache kwanza, sitaki kufanya kama Diddy nooo...

LUQMAN: Naona mwekezaji Simba ameanza kushindwa vita vya usajili. Wachezaji muhimu kama Okwi, Kotei, Niyonzima wanaondoka kweli? Aseme wazi hana pesa za kuwalipa.

LEVY: Hawezi kutoa hela wakati hati ipo kwa ‘Ze mani himu selfu’ Mzee Kilomoni. Hata hivyo, nimeshangaa leo hujatoa salamu kwangu, umeanza na miswali utadhani mashambulizi ya Senegal. Tujiandae na balaa la Mahrez tena. Kwa mwendo huu mpaka Stars wanarudi Bongo basi Amunike atakuwa kazeeka ghafla kama Mzee nanihiii.

Advertisement